UFAULU KIDATO CHA 6 JUU

UFAULU katika mtihani wa Kidato cha Sita mwaka jana, umeongezekakwa asilimia 8.13 huku shule za mikoani zisizo na majina makubwa zikichomoza katika orodha ya kumibora.Matokeo hayo yalitangazwa jana naBaraza la Mitihani Tanzania (Necta),huku yakionesha baadhi ya shule kongwe kama vile Tambaza ya jijiniDar es Salaam, zikiwa zimeshika mkia.

Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema katika mtihani huo uliofanyika kati ya Mei5 na 21, mwaka jana, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 8.13 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana.

Jumla ya watahiniwa 38,905 sawa na asilimia 95.98 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu. Mwaka jana wanafunzi waliofaulu walikuwani 44,366 sawa na asilimia 87.85.

Kaimu Katibu Mtendaji alisema wanafunzi waliofaulu, wasichana ni 12,080 sawa na asilimia 97.66 wakati wavulana ni 26,825 sawa na asilimia 95.25.

Shule Bora

Katika matokeo hayo, shule zilizofanya vizuri ni Igowole (Iringa), Feza Boys (Dar es Salaam),Kisimiri (Arusha), Iwawa (Njombe), Kibaha (Pwani), Marian Girls (Pwani) Nangwa (Manyara), Utawa (Mbeya), Kibondo (Kigoma) na Kawawa (Iringa).Ufaulu wa shule hizo umepangwa kwa kutumia kigezo cha wastani wapointi (Grade Point Average – GPA)na mchanganuo kwa kuzingatia idadi ya watahiniwa wasiopungua 30.

Kumi za mwisho

Kwa upande wa shule 10 za mwisho, pamoja na Tambaza, Dk Msonde alizitaja nyingine kuwa ni Ben Bella (Unguja), Fidel Castro (Pemba), Muheza High School (Tanga), Mazizini (Unguja), Mtwara Technical (Mtwara), Iyunga Technical (Mbeya), Al-Falaah Muslim (Unguja), Kaliua (Tabora) naOsward Mang'ombe (Mara).Wanafunzi BoraAkizungumzia walivyopatikana wanafunzi waliofanya vizuri zaidi, Kaimu Katibu Mtendaji huyo wa Necta, alisema waliangalia wastani wa GPA kwenye masomo ya tahasusi pamoja na wastani wa alama za jumla walizopata.Wanafunzi hao waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kitaifa na shule zao kwenye mabano ni Isaack Shayo (St. Joseph Cathedral),Doris Noah (Marian Girls), Innocent Yusufu (Feza Boys), Placidl Pius (Moshi), Benni Shayo (Ilboru), Abubakar Juma (Mzumbe),Mwaminimungu Christopher (Tabora Wavulana), Chigulu Japhaly (Mzumbe), Hussein Parpia (Al-Muntazir Islamic Seminary) na Ramadhani Ally Msangi (Feza Boys).

Kwa upande wa wasichana 10 bora kwa masomo ya sayansi kitaifa, watano wametoka Shule ya Marian.Nao ni Doris Noah, Monica Mtei, Wema Kibanga, Deborah Mlawa na Doreen Kashushura.

Wengine ni Frida Mbilinyi, Gloria Kweka (Msalato), Aisha Mnjovu, Mulhat Said (Feza) na Heavenlight Munis (St Mary Goreth). Wavulana 10 bora kwa masomo ya Sayansi kitaifa na shule zao kwenye mabano ni Isaack Shayo (St Joseph Cathedral), Innocent Yusuf, Ramadhan Msangi (Feza), Placid Pius (Moshi), Benini Shayo (Ilboru),Abubakar Juma (Mzumbe), Mwaminimungu Christopher (Tabora Boys), Chigulu Japhaly (Mzumbe), Hussein Parpia (Al Muntazir Islamic Seminary) na Lusekelo Kihesya (Mpwapwa).

10 bora

Biashara Watahiniwa 10 bora kwa masomo ya Biashara ni Jovina Leonidas (Nganza), Nestory Makendi (Kibaha), Imma Anyandwile (Umbwe), Thersia Marwa na Grace Chelele (Loyola), Betria Rugila (Baobab), Jaqueline Kalinga (Weruweru), Tajiel Kitojo (Arusha), Shiriya Ramaiya (ShaabanRobert) na Mwanaidi Mwazema (Weruweru).

Lugha, Sanaa

Watahiniwa kumi bora wa masomoya Lugha na Sanaa ni Lisa Mimbi (St. Mary Goreth), Rosalyna Tandau(Marian Girls), Joseph Ngobya (St. Joseph Cathedral), Aneth Mtenga na Idda Lawenja (Marian Girls), Edna Mwankenja( Kisimiri), Catherine Kiiza ( St. Mary Mazinde Juu), Nancy Adonswai (Mwika), Mohamed Salmin (Mwanza) na Idrisa Hamisi (Mwembetogwa).

Ubora wa ufaulu

Msonde alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 30,225 sawa na asilimia 85.73 wamefaulu katika madaraja I - III wakiwemo wasichana 9,954 sawa na asilimia 90.59 na wavulana 20,271 sawa na asilimia 83.53.

Daraja kwa Kwanza ni wanafunzi 3,773, wavulana 2,232 na wasichana 1,541, Daraja la Pili ni wanafunzi 9,631ikiwa wavulana ni 6,179 na wasichana 3,452.Daraja la Tatu ni wanafunzi 16,821 ikiwa wavulana ni 11,860 na wasichana 4,961, Daraja la IV: wanafunzi 4,420 ikiwa ni wavulana 3,474 na wasichana 946 na Daraja 0: wanafunzi 612, wavulana wakiwani 524 na wasichana 88.

Ufaulu Kiswahili

Msonde alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo yote 14 ya msingi umepanda ikilinganishwa na mwaka 2013. Ufaulu wa juu kabisa ni ule wa somo la Kiswahili ambao ni asilimia 99.88 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hilo wamefaulu.Alisema ufaulu katika masomo ya Sayansi (Physics, Chemistry, Biology na Advanced Mathematics)umeendelea kuimarika kwa kulinganisha na ufaulu wa masomohayo mwaka 2013.

Gredi za ufauluAlisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni wanafunzi 34,645 sawa na asilimia 98.26 ya waliofanya mtihani, wasichana wakiwa ni 10,900 ambayo ni asilimia 99.2 na wavulana 23,45 sawa na asilimia 97.84.

Mwaka 2013 watahiniwa 40,242 sawa a asilimia 93.92 ya watahiniwa wa shule walifauu mtihani huo. Mtahiniwa anahesabiwa kuwa amefaulu somo kwa kupata angalau gredi D (alama 30) katika somo husika.Hivyo, kiwango cha juu cha ufaulu katika somo ni gredi A na cha chinikatika somo ni Gredi D. "Ufaulu katika gredi A, B+, B na C utakuwa ni Principal Pass," alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Necta.Kulingana na mpangilio huo, Daraja la Kwanza ni poiti 3-7, la Pili8-9, Tatu 10-13 na Daraja la Nne mtahiniwa atakuwa amefaulu kwa kuwa na angalau D mbili au principal pass moja.Aliyepata Sifuri ni aliyepata ufaulu chini ya D mbili. Uzito wa alama katika Gredi; A=1, B+= 2, B=3, C=4, D=5, E=6 na F=7.

Watahiniwa wa Kujitegemea Alisema watahiniwa wa Kujitegemea waliofaulu ni 4,260 sawa na asilimia 80.73 ya watahiniwa 5,277 waliofanya mtihani.Mwaka 2013 watahiniwa wa kujitegemea 4,124 sawa na asilimia 53.87 walifaulu mtihani huo. Msonde alisema Baraza limezuia matokeo ya watahiniwa 150 wa shule ambao hawajalipa ada ya mtihani hadi watakapolipa, watahiniwa tisa waliopata matatizo ya kiafya."Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa katika Mtihani wa Kidato cha Sita Mei, 2015.

Alisema watahiniwa 29 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote. Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya Mtihani wa Kidato cha Sita Mei, 2015.

Msonde alisema Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa wawiliwaliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani. Matokeo Ualimu Katika hatua nyingine, matokeo ya walimu waliofanya mtihani mwaka 2014 yanaonesha watahiniwa katika ngazi ya Cheti, Stashahada na Stashahada ya Ualimu Ufundi, hakuna mwanafunzi aliyepata alama za juu.Dk Msonde alisema watahiniwa 4,161 sawa na asilimia 85.71 ya watahiniwa 4,899 waliofanya mtihani wa Stashahada ya Ualimu mwaka 2014 wamefaulu.Kati ya watahiniwa hao, wasichana ni 1,401 sawa na asilimia 83.64 na wavulana 2,760 sawa na asilimia 86.79.Alisema katika hao waliofaulu, hakuna aliyepata daraja la juu (distiction). Waliopata daraja la credit ni watano, pass 4,156, wanaorudia mtihani ni 658 na waliofeli ni 36.Akizungumzia matokeo ya mtihani wa Stashahada ya Ualimu Ufundi, Msonde alisema "watahiniwa wote watatu waliofanya Mtihani wa Stashahada ya Ualimu Ufundi wameshindwa baadhi ya masomo, hivyo watarudia masomo waliyoshindwa katika Mtihani wa Mei 2015.

Bofya hapa Kuangalia matokeo http://www.necta.go.tz/matokeo2014/ACSEE.htm