TANZANIA NA ALGERIA KATIKA UBIA WA GESI

TANZANIA na Algeria zinakamilisha majadiliano ya kuanzisha kampuni ya ubia, itakayohusika na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme.


Pia, itaanzishwa kampuni ya ubia ya kujenga mtambo wa kusindika gesi ya majumbani (Liquefied Petroleum Gas-LPG) na kuiuza kwawananchi kwa kutumia mitungi.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika ziara ya kikazi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na ujumbe wake nchini humo.


Ziara hiyo ya waziri, inalenga kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya awali ya kushirikiana katika kubadilishana uzoefu kwenye masuala yanayohusu sekta za nishati na madini, kutokana na Mkataba wa Makubaliano ya ushirikiano uliosainiwa Desemba 2 mwaka jana nchini humo.


Kwa mujibu wa makubaliano katika mkutano baina ya Mawaziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Muhongo na wa Nishati na Migodi wa Algeria, Youcef Yousfi, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na la Algeria (KAHRIF) yameagizwa kukamilisha majadiliano ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme.


Aidha mawaziri hao wenye dhamana ya nishati na madini, waliagiza kampuni za mafuta na gesi, likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kukamilisha majadiliano yakuanzisha kampuni ya ubia ya kujenga mtambo wa gesi na kuuza gesi hiyo kwa wananchi kwa kutumia mitungi. TPDC pamoja na kampuni za mafuta na gesi za Algeria ambazo ni Naftal na Sonatrac, zimeambiwa kampuni zote za ubia zinatakiwa kuanza kazi ifikapo Januari mwakani.

Katika ziara hiyo, Waziri Muhongo na ujumbe wake wamepata nafasi ya kutembelea mtambo wa kufua umeme wa kutumia gesi asilia wa Hamma, ambao unamilikiwa na serikali ya nchi hiyo kwa asilimia 100.


Mtambo huo una uwezo wa kuzalisha megawati za umeme 418, na uwezo wa kutumia mafuta ya dizeli na gesi kwa nyakati tofauti.

Miongoni mwa maofisa walioongozana na Waziri Muhongo ni pamoja na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme, Luoga na wataalamu kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), TPDC na Tanesco.