JESHI LA POLISI LAWASHIKIRIA ASKARI WATATU KWA TUHUMA ZA MAUAJI

Jeshi la polisi kanda maalum ya Tarime na Rorya, linawashilia askari wake watatu kwa tuhuma za kumpiga hadi kumuua kijana mmoja Kitandika Ryoba mkazi wa Sirari, baada ya kumkamata kwa madai ya kumkuta akivuta bangi na kucheza kamali katika eneo hilo la Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya.


Jeshi hilo la polisi limechukua hatua hizo siku chache tu baada ya mamia ya wananchi wa mji huo mdogo wa Sirari kufanya vurugu na maandamano makubwa huku wakichoma tairi za magari katika barabara kuu ya Sirari, Tarime -Mwanza, vurugu ambazo zililenga kulitaka jeshi hilo kueleza chanzo cha kifo cha kijana huyo, anayedaiwa kuuawa kisha mwili wake kwenda kuhifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya wilaya ya Tarime bila ya ndugu na jamaa zake kujulishwa kuhusu tukio hilo.

Kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Tarime na Rorya kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi Justus Kamugisha, amesema jeshi hilo linawashikilia askari wake hao watatu kwa mahojiano ambao walimkamata kijana huyo kabla ya kuuawa kwa kipigo, wakati jeshi hilo likisubili majibu ya uchungizi wa sehemu ya mwili wa marehemu ambayo yamepekelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali.

Wakizungumza katika mazishi ya kijana huyo, ambayo yamefanyika katika mji mdogo wa Sirari,baadhi ya viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime na vyama vya siasa, wamewataka askari wa jeshi hilo kubadilika katika utendaji wao wa kazi, kwani wamesema kitendo cha polisi kuua ovyo raia kwa kisingizi kuwa ni watuhumiwa kinachochea chuki kati ya jamii na jeshi hilo.