WATU NANE WASHIKILIWA NA POLISI WAHUSIKA WA UTUPWAJI MABAKI YA BINADAMU

JESHI la Polisi Kanda ya Dar es Salaam linawashikilia na kuwahoji watu wanane kwa kutupa viungo vya binadamu katika bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaan Suleiman Kova amesema hayo leo Ofisi kwake wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Amesema kuwa watu hao wakimemo madaktari wa International Medical and Technological University (IMTU) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukiri kuhusika na tukio la utupaji wa viungo vya binadamu katika eneo hilo.

Kamishna Kova amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji na kufanya uchunguzikuona kama wahusika wamefanya kosa linalohitaji kuchukuliwa hatua za kisheria au hawana kosa.

Ameongeza kuwa kufuatia tukio hilo tayari Jeshi la Polisi Kanda Maalum limeshafungua jarada la uchunguzi kubaini ikiwa wahusika wametenda kosa linalohitaji kufikishwa kwenye vyombo vya sharia kwa hatua zaidi.

Kamishna huyo amesema kuwa katika kutekeleza jambo hilo tayari jopo la wachunguzi likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jaffar Mohamed linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha watu hao kutupa viungo hivyo katika eneo hilo na idadi ya watu kulingana na viungo vilivyotupwa.

Aidha Kamishna Kova amewasihi wananchi wasiwe na wasiwasi kwani viungo vilivyookotwa havina uhusianona mauaji ya watu wengi na wala havihusiki na masuala ya ushirikina.

Amewaahidi wananchi kutoa taarifa kamili mara tu upepelezi utakapokamilika.

Viungo vya binadamu vikiwemo mikono, miguu, vichwa , mapafu na mioyo viligundulika jana (21.7.2014) jioni vikiwa vimehifadhiwa katika mifuko ya plastiki 85 na kutupa katika bonde la MbweniMpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni.

Mara baada ya kugunduliwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni walivichukua na kuvipeleka katika Hospitali ya Taifa kwa uchunguzi zaidi.