WANAKIJIJI WAFANYA UHARIBIFU MALI KWA KUMTUHUMU UCHAWI MWANAFAMILIA

Wakazi wa kijiji cha Nguruka wilayani Uvinza mkoani Kigoma, wamechoma nyumba nne za familia moja yenye zaidi ya watu ishirini na kuteketeza vyakula na mali nyingine zenye zaidi ya shilingi milioni mia moja baada ya kumtuhumu mmoja wa wanafamilia kwa ushirikina.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mkoronga katika kijiji cha Nguruka Matei Charle ambaye alimuokoa mtuhumiwa wa uchawi aliyetambulika kwa jina la Siyajui Ahmad, amesema mama huyo alianza kushambuliwa akiwa katika msiba wa kijana Masoud Vyombo ambaye alifariki ghafla ambapo wakazi wa kijiji hicho waliomtuhumu kumuua kwa njia ya ushirikina walianza kumshambulia kabla ya kuokolewa ambapo mamia ya wananchi waliamua kuteketeza nyumba yake pamoja na nyumba tatu za kaka zake na wazazi wake, huku Siyajui Ahmad aliyetuhumiwa akieleza kuwa familia hiyo imepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni mia moja na kwamba alilazimika kutoroka ili kuokoa maisha yake.

Kamanda wa polisi mkoani Kigoma Frasser Kashai amesema jumala ya watu kumi na watano wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku kwa upande wake katibu mwenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Uvinza Majaliwa Zuberi akitoa wito kwa wananchi kutochukua sheria mkononi na akiitaka kamati ya maafa ya wilaya kuzisaidia familia nne zilizoathirika ambazo kwa sasa zinalala nje na hazina chakula, mavazi na mahitaji mengine ya msingi.