MWANAMKE ALIYEFICHA MTOTO KWA NJIA ZA KISHIRIKINA AFIKISHWA MAHAKAMANI

MKAZI wa kijiji cha Marambeka wilayani Bunda, Minza Pama (80), anayetuhumiwa kuiba mtoto kwa njia ya ushirikina na kumficha uvunguni mwa kitanda chake kwa muda wa siku saba, amefikishwa katika mahakama ya wilaya hiyo nakupelekwa mahabusu kwa kukosa dhamana.

Mwanamke huyo amefikishwa katika Mahakama hiyo juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Safina Simufukwe na kusomewa mashitaka ya kuiba mtoto kwa nia ya kutaka kutenda kosa.

Mwendesha mashitaka wa polisi, Masoud Mohamed alidai mshitakiwa huyo anatuhumiwa kumuiba Yateke Ramadhan (9) na kumficha nyumbani kwake uvunguni mwa kitanda kwa muda wa siku saba, bila kumpa chakula chochote.


Mtoto huyo baada ya kupotea katika mazingira ya kutatanisha akiwa matembezini, wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani walianza msako wa kumtafuta na Julai 3, mwaka huu, walimkuta akiwa amefichwa uvunguni mwa kitanda cha kikongwe huyo akiwa hajitambui.

Baada ya kumpata wananchi walianza kushambulia mwanamke huyo, ambapo aliokolewa na polisi waliowahi kufika katika eneo hilo, ambapo pia askari polisi mmoja alijeruhiwa kwa bahati mbaya kwa kupigwa jiwe kichwani na wananchihao waliokuwa na jazba.


Aidha, ilielezwa kuwa wananchi hao walimwamru kikongwe huyo kumzindua mtoto huyo ili aweze kurudia hali yake ya kawaida na ndipo akammwagia dawa kichwani na kuzinduka.

Mtuhumiwa huyo alikana mashitaka yake na kupelekwa mahabusu baada ya kushindwa masharti ya dhamana, ambapo kesi yake itatajwa tena mahakamani hapo Julai 22, mwaka huu.


Chanzo: Habari leo