Kukamatwa kwa Manyika kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas lakini hakuwa tayari kusema chochote juu ya kuwekwa rumande kwa askari huyo.
"Ni kweli tulimkamata (Manyika) baada ya kufanya uchunguzi na kugundua kuwa silaha waliyokutwa nayo majambazi ni mali yake," alisema bila ya kufafanua chochote.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya jeshi la polisi vilisema kuwa Manyika alikamatwa Julai 9 mwaka huu akiwa kazini Ngorongoro, baadaya kubainika kuwa silaha hiyo ilikuwa mali yake.
Habari ziliendelea kusema kuwa Manyika ambaye ni dereva wa gari kubwa la FFU anamiliki silaha aina ya shotgun namba A 947514 M – Pump Action iliyotengenezwa Marekani.
Siku ya tukio la kuuawa kwa majambazi hao watatu ambao walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 762 CWE, walikuwa wanakwenda kupora fedha katika kampuni ya Arusha Ceramic Centre inayojishughulisha na utengenezaji wa vigae.
Majambazi hao waliuawa Julai 4 mwaka huu saa 10:20 jioni jirani na Kiwanda cha Bia (TBL) eneo la Njiro Jijini Arusha na silaha hiyo ilikuwa na risasi tatu.
Majambazi hao walitambuliwa kwa majina ya Selemani Walii(25) mkazi wa Kaloleni Jijini Arusha, Walter John (30) na mdogo wake Fred John (21) wote wakazi wa Sekei wilayani Arumeru mkoani Arusha.