UKAWA WABADILIKA

VIONGOZI wanaounda kile kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesema hawako tayari kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka kesho huku nchi ikiwa na Katiba ya zamani, hivyo keshokutwa wanatarajiwa kuingia katika mazungumzo kunusuru mchakato mzima wa Katiba.

Wameeleza kuwa, kwa kutambua muda mfupi uliobaki kati ya mchakato wa Katiba kumalizika na Uchaguzi Mkuu, watafanya mazungumzo hayo kwa faida ya Taifa na wananchi waliojitokeza kwa wingi kuwasihi warejee katika Bunge Maalumu la Katiba linalotarajiwa kurejea kwa siku 60 kuanzia Agosti 5, mwaka huu.

Awamu ya kwanza ya Bunge hilo ilikutana kwa siku 70, lakini kutokana na wajumbe kusigana kwa mambo kadhaa, yakiwemo ya kiitikadi na kutoaminiana, liliahirishwa Aprili 25 mwaka huu ilikupitisha Bunge la Bajeti bila kuwepo na sura ya kukamilika karibuni.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mmoja wa viongozi wa umoja huo ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wana imani kuwa taifa linahitaji Katiba mpya hivyo watajadili katika mazungumzo hayo ya Jumatatu ili kuwawezesha kupatanjia mbadala iwapo mchakato huo utakwama.

Akifungua kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, Mbowe alisema kwa niaba ya uongozi wa Ukawa wanapongeza hatua ya taasisi, viongozi wa dini na watu mbalimbali kuwasihi kurudi katika Bunge la Katiba, na kwamba wako tayari kufanya mazungumzo kuhusukurejea bungeni.


Alisema hata kama kwenye mazungumzo hayo watakubaliana kurejea bungeni na wakiwa katika bunge hilo kutajitokeza maamuzi yakutaka kulivuruga bunge, hawatasitakuchukua hatua kama ya awali.

"Napenda kuwataarifu wananchi kuwa Ukawa tuko tayari kwa mazungumzo kwa nia ya kunusuru mchakato wa Katiba kuendelea kama walivyotusihi watu mbalimbali, lakini tutaenda katika mazungumzo hayo Jumatatu kwa kuhakikisha mchakato huo hautanajisiwa," alisema.


Alidai kuwa wao kama chama cha siasa wamepata habari za ndani zinazodai kuwepo kwa njama za kuvuruga mchakato huo ili kuendelea kutumika kwa Katiba ya zamani, jambo alilodai kuuliza dhamira hizo katika mazungumzo hayo.

"Sisi hatuko tayari kuona uchaguzi ujao unafanyika kwa kutumia Katibaya zamani na tume ya uchaguzi iliyopo, hivyo tutahakikisha tunakwamua hali hii ili mchakato uendelee," alisema Mbowe na kuongeza kuwa, watu mbalimbali wamekuwa wakiwasihi Ukawa kurejea bungeni bila kuzungumza kwa nini waliamua kutoka nje ya bunge na kwanini mchakato huo unatishia kukwama.


Alisema viongozi wa Ukawa wamejadiliana na kufikia maamuzi kuwa hawakatai mazungumzo, bali wanachopinga ni kurudi Bungeni kabla sababu iliyowafanya watoke haijafanyiwa kazi huku akieleza kuwa mwenye mamlaka ya kuokoa mchakato huo ni Rais Jakaya Kikwete.

"Hatuwezi kuwa wanasiasa wa kuzirabali mazungumzo ni kitendo cha uungwana wa kawaida katika uongozi pale inapotokea kutoelewana kwa kuangalia tatizo nakufanyia kazi kwa ajili ya kunusuru mchakato na kurudi katika mchakato," alisema.


Alisema katika mkutano wa awali kujadili jinsi ya kunusuru mchakato huo walikubaliana kila chama kuweka bayana vikwazo vya mchakato ambapo chama tawala na Ukawa kila moja walitoa sababu zao.

Mbowe alisema baada ya kutoa taarifa zao watazijadili katika kikao hicho cha kamati kwa siku mbili, ikiwa ni pamoja na hali ya siasa nchini, mchakato mzima wa katiba pamoja na suala la uchaguzi wa serikali za mitaa na kisha kutoa taarifa kesho.


Naye, Mjumbe wa Kamati hiyo, Profesa Mwesiga Baregu alisema jambo la msingi ni Ukawa kurejea bungeni na kukubaliana katika bunge hilo kuongozwa na agenda zilizo chini ya sheria kwa kujadili kilichopo katika Rasimu ya pili na kujadili nje ya rasimu ni kuvunja sheria.

Alisema pia Ukawa wanatakiwa kuwa makini na wanaotaka warejee bungeni kwani siyo kila mmoja nia yake ni njema.

Chanzo: Habari leo