ISRAEL: HATUONDOKI GAZA MPAKA TUYAHARIBU MAHANDAKI

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema kuwa Israel imeamua kuyaharibu kabisa mahandaki na njia za chini yaardhi zilizojengwa na wapiganaji wa Palestina-Hamas, katika mipaka yake huko Gaza.

Amesema uharibifu huo utatekelezwa na majeshi ya Israeli kukiwa au kutokuwa na muafaka wa kusitisha mapigano.

Netanyahu amesema hayo huku Serikali ya Israel ikishikia kani kuwa kuwa itaendeleza mashambulizi katika eneo la Gaza licha ya shutma za kimataifa kufuatia shambulizi la shule moja ya umoja wa mataifa ambapo takriban watu 15 walipoteza maisha yao.

Msemaji wa serikali ya Israel amesema kuwa wataomba msamaha iwapo watabaini kwamba shambulizi hilo, lilitekelezwa kimakosa na wanajeshi wa Israel.

Umoja wa mataifa umesema kuwa ni wazi kwamba ni jeshila israel ndilo lililorusha kombora hilo katika shule hiyo ambapo zaidi ya raia elfu tatu wa Palestina walikuwa wameomba hifadhi.

Licha ya malalamiko kutoka kote duniani kuhusiana na idadi kubwa ya vifo vyaNjia za chini kwa chini za Hamas ambazo Israeli inalenga kuharibu

Mashambulizi ya Israel kutoka angani na nchi kavu yamerindima kwa milipuko ya mizinga na ndege za kivita.

Na sasa Israel inajiandaa kwavita zaidi baada ya kuwaamuru wanajeshi wa akiba kujiunga na jeshi la taifa. Katika ukanda wa ngazani kilio na majonzi makubwa...

AJALI YAUA 19

JUMLA ya watu 19 wamekufa katika ajali mbili tofauti zilizotokeamkoa wa Dodoma na Arusha jana.

Ajali hizo mbili zimesababisha majeruhi zaidi ya 70.

Ajali ya kwanza mbaya ilihusisha basi la abiria na lori ambapo watu 17 walikufa na wengine 56 kujeruhiwa. Katika ajali hiyo basi laabiria na lori yaligongana uso kwa uso.

Aidha, katika ajali ya Arusha, madereva wa magari mawili yaliyogongana maeneo ya Sadeki wilayani Arumeru, walikufa na wakati huo huo watu 14 wamejeruhiwa.

Basi Morobest

Ajali ya mkoani Dodoma ilihusisha basi la Morobest lililokuwa likitoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam, na ilitokea eneo la Pandambili, Wilaya ya Kongwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi jana. Kati ya 17 waliopoteza maisha, wanaume ni 12.

Basi hilo lenye namba za usajili T258 AHV likiendeshwa na Said Lusogo, liligongana na lori namba T820CKU/ T390CKT likitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, likiendeshwa na Gilbert Nemanya. Madereva wote wawili wamekufa.

Kwa mujibu wa Kamanda Misime, kufikia jana mchana miili 11 ilikwishatambuliwa. Majina ya waliokufa Waliotambuliwa ni dereva wa lori hilo, Nemanya pamoja na utingo wake, Mikidadi Zuberi. Wengine ni dereva wa basi la Morobest, Lusogo na kondakta wake, Omary Mkubwa.

Marehemu wengine waliotambuliwa ni Merina Malikeli,Nasib Machenje, Wilson Suda, Gabriel Mejachiwipe, Justine Makasi na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina moja la Christina.

Kwa mujibu wa Misime, watu 56 wamepata majeraha mbalimbali na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori kutokuwa na hadhari kwa magari yaliyokuwa yanakuja mbele yake wakati anapita gari lingine.

Majeruhi

Majeruhi 23 wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Majina yao ni Frank Raymond, Patricia Ngamwai, Amos Chiwaga, Mary Mateo, Safari Jonas, Suzan Charles, Gasper Shao,Felician Rite, Felister Mathias, Amos Jonas, Edina Lwande, Seleman Kaseni, Nazareth Kasua, Saimon Msoloka, Juma Mtezi na Swalehe Bakari.

Wengine ni Naseria John, Getruba Kombo, George Njelewa, Manase Makuja, Chibago Mchiwa, Nicholous Roger na Michael Chibwela.

Ajali Arusha

Kwa upande wa ajali ya mkoani Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema ilitokea juzi saa 3 usiku maeneo ya Sadeki kwa Fundi.

Alisema gari aina ya Subaru lenye namba za usajili T842 CCP lililokuwa likiendeshwa na David Natal (35) liligongana na gari ya Nissan Mini Bus lenye namba za usajili T355 CGA lililokuwa likiendeshwa na aliyetambuliwa kwa jina moja la Joshua.

Alisema ajali hiyo ilitokea wakati Natal aliyekuwa anatoka Arusha mjini kwenda Makumira, alipojaribu kupita gari lililokuwa mbele yake ndipo lilipogongana nagari lililokuwa linatoka Usa River kwenda Arusha mjini.

Mbali na vifo vya madereva hao, ajali hiyo ilisababisha majeruhi 14 waliokuwa kwenye gari aina ya Nissan Mini Bus.

Majeruhi hao ni Frida Joseph (18), Elisante Mungure (45), Lilian Mathias (29), Juma Mohamed (42), Silvia Kelvin (26), Charles Massawe (40), Kelvin Charles (29), Emmanuel Adedia (29), Zainabu Issa (40), Regard Joseph (30), Elirehema Abrod (29), Alfred Lucas(21), Gipson Tackson (3) na Salma Abdallah (44).

Kamanda alisema majeruhi hao wanatibiwa katika Hospitali ya Tengeru na Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

AJINYONGA BAADA YA MKEWE KUMUACHA

MKAZI wa Kijiji cha Vikonge, Kata ya Mpandandogo wilayani Mpanda,Joseph Lukato (52) amejinyonga kwa kujitundika mtini akitumia mtandio wa mkewe baada ya kughadhabika na kuachwa naye.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Focas Malengo, alisema tukio hilo lilitokea Julai 27,mwaka huu saa mbili asubuhi kijijini hapo ambapo alijinyonga katika shamba la jirani yake.

Kamanda huyo alisema Lukato alikuwa na ugomvi wa muda mrefuna mkewe Mary Joseph (42) aliyekuwa akimtuhumu kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwingine kijijini hapo.

Alisema siku ya Julai 19, mwaka huu, Lukato alirejea nyumbani kwake saa nane mchana akitokea shambani na kula chakula ambapo alimlalamikia mkewe kuwa kilikuwa kibichi.

Alisema hatua hiyo ilizua ugomvi baina ya wanandoa hao ambapo Lukato alimwambia mkewe kwamba amempikia chakula kibichi kwa kuwa alichelewa kurudi nyumbani kutoka mwanaume huyo mwenye uhusiano naye wa kimapenzi.

Kamanda Malengo alisema mke waLukato alijitahidi kujijitetea kwa mumewe kuwa hakuwa ametoka nyumbani kwake siku hiyo na kumhakikishia mumewe kuwa chakula kilikuwa kimeiva.

Inadaiwa Lukato hakukubaliana na utetezi wa mkewe na aliendelea kumshutumu na baadaye akaanza kumpiga katika ugomvi uliochukua muda mrefu hatua iliyomfanya mke wa Lukato kurudi nyumbani kwa wazazi wake kwa kuhofia usalama wa maisha yake.

"Lukato alijitahidi kufanya jitihada za mara kwa mara za kumshawishi mkewe arudi nyumbani kwake ili wakaendelee kuishi kama walivyokuwa wakiishi awali lakini mkewe alikataa kurejea, hatua iliyomfanya Lukato kujinyonga," alisema Kamanda.

Alisema mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Chanzo: Habari leo

AJIRA ZA UHAMIAJI ZAFUTWA

Imeelezwa kuwa kufutwa kwa ajira hizo kunatokana na madai ya kuwa kuna upendeleo ulifanyika.

MASHAMBULIZI YAANZA TENA GAZA

Ndege za kivita za Israel zimeshambulia maeneo matatu tafauti kwenye Ukanda wa Gaza, kwa kile jeshi la nchi hiyo linachosema ni kujibu kombora moja lililorushwa na Hamas na kuangukia kwenye mji wa pwani wa Ashkelon, kusini mwa Israel hivi leo.

Majibizano ya risasi yalisikika kati ya pande hizo mbili, licha ya kutajwa kwamba zimesitisha mapigano kwa muda kupisha siku tatu za Sikukuu ya Eid al-Fitr zilizoanza leo, baada ya kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Juhudi za kimataifa zimeongezeka kusitisha mapigano hayo ya wiki tatu kwenye Ukanda wa Gaza. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano hayo mara moja na bila ya masharti yoyote.

"Baraza la Usalama linaunga mkono kikamilifu wito wa washirika wa kimataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitishwa mapigano mara moja na bila masharti yoyote ili kuruhusu uwasilishwaji wa bidhaa zinazohitajika haraka kwenye kipindi hiki cha Eid al-Fitr na hata baada ya hapo," amesema Eugene-Richard Gasana, ambaye ni balozi wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa na rais wa sasa Baraza la Usalama.

Jioni ya jana, Rais Barack Obama wa Marekani alimpigia simu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kumueleza wasiwasi wake juu ya idadi kubwa ya Wapalestina waliouwa na kujeruhiwa. Tayari Wapalestina 1,030 na Waisraili 43 wameshauawa hadi sasa.

USALAMA WAZIDI KUZOROTA LIBYA

Kiasi ya watu 150 wameuawa katika ghasia ambazo zimezuka upya katika miji ya Benghazi na Tripoli katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kufuatia makabiliano makali kati ya wanajeshi na makundi hasimu ya wanamgambo.
Wizara ya afya ya Libya imesema tangu makabiliano hayo kuzuka wiki mbili zilizopita, kiasi ya watu 94 wameuawa katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na zaidi ya wengine 400 wamejeruhiwa wakati wa mapambano kati ya wanajeshi na wanamgambo wanaong'angania kuudhibiti mji huo.
Kiasi ya wengine 55,wengi wao raia wameuawa katika mji wa Benghazi mwishoni mwa juma katika makabaliano mengine kati ya jeshi na makundi ya wanamgambo wa kiislamu.

Maroketi yalenga mapipa ya mafuta
Shirika la taifa la mafuta limesema maroketi yaliyokuwa yakirushwa, yalilenga matangi ya kuhifadhia mafuta karibu na uwanja wa ndege wa Tripoli hapo jana na kusababisha moto mkubwa ambao wazima moto wameshindwa kuuzima. Matangi hayo yalikuwa yanahifadhi kiasi cha lita milioni sita za petroli na yako karibu na mengine yanayohifadhi gesi na diesel.
Abiria wakisubiri kusafiri katika uwanja wa ndege wa Miitiga
Abiria wakisubiri kusafiri katika uwanja wa ndege wa Miitiga
Wizara ya mafuta na nishati imewaonya raia wanaoishi karibu na maeneo ya matangi hayo kuondoka mara moja kuepusha majanga ya kibinadamu na kimazingira kufuatia kuzuka kwa moto huo mkubwa.
Mapigano hayo ya wiki mbili ndiyo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu kung'olewa na baadaye kuuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa tafa hilo Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Marekani,Umoja wa Mataifa na Uturuki zimewaondoa wafanyakazi wa balozi zao kutoka taifa hilo la kaskazini mwa Afrika. Marekani iliwahamishia wafanyakazi hao katika nchi jirani ya Tunisia siku ya Jumamosi chini ya ulinzi mkali baada ya mapigano kupamba moto karibu na ubalozi wake mjini Tripoli.
Msafara wa magari yaliyokuwa yamewabeba maafisa wa Uingereza ulishambuliwa jana katika jaribio la utekaji nyara nje ya mji wa Tripoli ulipokuwa ukielekea Tunisia na ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa katika kisa hicho, magari yaliharibiwa.
Wajumbe maalumu wa jumuiya ya nchi za kiarabu kuhusu Libya,Marekani na umoja wa Ulaya wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali inavyozidi kuzorota nchini Libya na kusema hali hiyo imefikia hatua ngumu na kutaka mapigano kusitishwa mara moja.

Nchi za magharibi zawataka raia wake kuondoka

Ujerumani, Uingereza ,Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Misri na Uturuki nimiongoni mwa nchi nyingine ambazo zimewataka raia wao walioko Libya kuondoka nchini humo mara moja kwa sababu ya kudorora kwa hali ya usalama.
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Misrata
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Misrata

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema raia wa Ujerumani walioko Libya wako katika hatari kubwa ya kutekwa nyara na kuuawa kwa sababu sio rahisi kutabiri hali nchini humo itachukua mkondo gani.
Bunge jipya la Libya lililochaguliwa mwezi Juni mwaka huu linatarajiwa na nchi za magharibi kuwa litaweza kumaliza mzozo huo kwa kufikiana makubaliano ya kisiasa wakati wabunge watakapokutana kwa kikao cha kwanza mwezi ujao.
Miaka mitatu baada ya kung'olewa kwa Gaddafi,ndoto ya Libya kuifikia demokrasia imezongwa na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe ya kisiasa na mapigano ya mara kwa mara kati ya makundi hasimu ya waasi waliosaidia kumuondoa Gadafi madarakani ambayo yanataka kuidhibiti miji mikuu na viwanda vya mafuta.

MAREKANI WAFUNGA UBALOZI LIBYA

Marekani imefunga ubalozi wake wa Libya kwa muda na wafanyakazi wake wote wamehamishiwa nchi jirani, Tunisia.Walipelekwa huko kwa magari huku wakilindwa na ndege za Marekani.

Wizara ya mashauri ya nchi za nje ya Marekani piya imewasihi raia wote wa Marekani waondoke nchini humo.

Jengo la ubalozi wa Marekani mjini Tripoli liko katika eneo ambalo limeathirika na mapambano kati ya makundi ya wapiganaji yanayozozana, ambayo yamekuwa yakigombania kudhibiti uwanja wa ndege wa kimataifa wa Libya.

Waziri wa mashauri ya nchi za nje, John Kerry, alisema kulikuwa na hatari hasa ikiwakabili wafanyakazi wa ubalozi huo, lakini alisisitiza kuwa shughuli za ubalozi zinasimamishwa kwa muda tu.

Miaka miwili iliyopita balozi wa Marekani aliuwawa pale ofisi ndogo ya ubalozi wa Marekani katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya, iliposhambuliwa na wapiganaji Waislamu.

MUUZA BANGI AKWEPA JELA, ALIPA FAINI

MUUZA JI wa bangi, Ferdinand Makundi (40) amenusurika kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada kulipa faini ya Sh 100,000 kwa kosa la kukutwa na kilo mbili za bangi.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama yaWilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, Ramadhani Rugemalira alimhukumu mkazi huyo wa kijiji cha Mkole wilayani humo kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh 100,000 baada ya kukiri kosa.

Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi, Hamimu Gwelo alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 14 mwaka huu saa 7:00 mchana akiwa nyumbani kwake kijijini Mkole.

Alipotakiwa kujitetea, mshitakiwa aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa ana watoto kumi na mke wanaomtegemea.


Chanzo: Habari Leo

WATALII 17 WAPORWA NA MAJAMBAZI

Kundi la watu wanaoaminika ni majambazi wakiwa na bunduki wamevamia Hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge iliyopo wilayani Hai na kuwapora watalii fedha na vitu vingine.

Majambazi hao walipora Sh5.4 milioni, Dola 3,200 za Marekani sawa na Sh5 milioni na Pauni za Uingereza 110 sawa na Sh300,000.


Pia walipora kamera moja yenye thamani ya Sh1.5 milioni, kamera ya video yenye thamani ya Dola 3,000 sawa na Sh4.8 milioni na kamera nyingine sita za kisasa.

Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz zilisema watalii 17 kutoka mataifa mbalimbali waliporwa huku watalii wanne wakijeruhiwa katika tukio hilo.

"Ni kweli hilo tukio lipo na tumeanzisha msako mkali wa kuwatafuta watu hao pamoja na vitu walivyoiba na tunaomba yeyote mwenye taarifa sahihi za majambazi hao watusaidie," ma Boaz.


Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:30 alfajiri baada ya majambazi hao kufanikiwa kuingia katika hoteli hiyo na kuwakusanya watalii wote waliokuwa wamelala na kuwaweka katika hema moja.

Baada ya kuwakusanya katika tenti hilo, majambazi walirudi katika mahema ambayo watalii hao walikuwa wamefikia na kuanza kupora kila kitu zikiwamo saa na simu za mkononi.

Wakati majambazi hao wakiendeleana uporaji, walijitokeza watalii wanne ambao walikuwa wanawahi ndege Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kutibua harakati hizo.


"Hao watalii waliokuwa wanakwenda KIA wao walikuwa wamelala vyumbani kwa hiyo walipopanda kwenye gari na lilipowashwa tu wale majambazi wakataharuki," ilidokezwa.

Chanzo kimoja katika hoteli hiyo kimedokeza kuwa, baada ya gari hilo kuwashwa, majambazi hao waliokuwa na bunduki na mapanga waliliendea gari hilo na kuvunja kioo cha gari hilo.


Baada ya kuvunja kioo hicho, majambazi hao walianza kuwapora watalii hao lakini sauti za kuvunjika kwa kioo cha gari ndiko kunakodaiwa "kuwashtua" walinzi wa hoteli hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo, Novatus Makunga aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili watu hao waweze kukamatwa.

SERIKALI YAIFUNGIA HOSPITALI YA IMTU

Serikali imeifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), baada ya kuifanyia ukaguzi na kubaini kasoro kadhaa za uendeshaji wake.


Ukaguzi huo ulifanywa jana na jopo la wataalamu kutoka Manispaa ya Kinondoni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baada ya IMTU kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ukaguzi huo ulifanywa jana na jopo la wataalamu kutoka Manispaa ya Kinondoni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baada ya IMTU kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Hospitali hiyo imefungiwa wakati Kamati ya Watu 15, iliyoundwa na Serikali ikiendelea kuchunguza kashfa hiyo.


Hata hivyo, wakati taarifa za kufungiwa zikitolewa habari za ndani zinaonyesha kuwa hapakuwa na mgonjwa yeyote hospitalini hapo, ikielezwa kuwa wagonjwa wote waliondoka baada ya kuibuka kwa kashfa ya viungo IMTU ikihusishwa.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Bunini Kamba alisema kuwa wameamua kuifungia hospitali hiyo kwa muda usiojulikana, baada ya kukuta upungufu mbalimbali katika maeneo ya kutolea huduma, jambo linalohatarisha usalama wa wagonjwa.

"Maabara tumekuta dawa ambazo muda wake wa kutumika umepita na hazikuwa katika mpangilio maalumu. Wodini hakuna usimamizi maalumu, hasa kwa wagonjwa wenye majeraha," alisema Dk Bunini.


Aliongeza: "Hakuna wauguzi wa kutosha na mashine ya kuchoma taka ngumu haifanyi kazi vilivyo. Tumeona kuwa hospitali hii haistahili kuendelea kutoa huduma kwa jamii."

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Yasin Mgonda alisema: "Tumesikia uamuzi huo uliotolewa baada ya kufanyika ukaguzi. Tutajirekebisha na tutakapokamilisha tutawaita kuja kutukagua tena."

Alisema kuwa pamoja na sababu nyingine, hospitali yake imefungiwa baada ya kubainika kuwa bomba la maabara limeharibika na halitoi maji.


Nyingine ni kutojaza vitabu vya wagonjwa kwa mujibu wa taratibu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, pia duka lake la dawa kuwa halijasajiliwa lakini akasema sababuhiyo imewashangaza kwani wanachojua wao duka hilo limesajiliwa.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia aliliambia gazeti hili kwamba anaipongeza Serikali kwa uamuzi huo akisema utanusuru maisha ya wananchi waliokuwa wakipata huduma hospitalini hapo.

"Tunaipongeza Serikali, ila tunaiomba iwatafutie wanafunzi wachuo hicho maeneo mengine ya kujifunzia," alisema Dk Saidia.

Juzi, Dk Saidia alisema kuwa wote waliohusika na kashfa ya utupaji mabaki ya viungo vya binadamu wanastahili kuchukuliwa hatua kali kwa sababu kitendo hicho kimekiuka sheria, taratibu, haki za binadamu, maadili ya ufundishaji na taaluma ya udaktari.


"Kama ni taasisi ya utafiti imepoteza sifa ya kufanya utafiti nakama ni ya mafunzo basi imepoteza sifa ya kutoa mafunzo ya tiba.
Kama ni hospitali itakuwa imepoteza sifa za kutoa tiba kwa binadamu," alisema Dk Saidia.

Naye spika wa serikali ya wanafunziwa chuo hicho (IMTUSO), William Mapunga alisema kuwa kufungiwa kwa hospitali hiyo kutawaathiri, kwani watakosa sehemu ya kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo, akiiomba Serikali kuliangalia suala hilo kwa mapana.


Chanzo: Mwananchi

MABAKI YA NDEGE YA ALGERIA YAONEKANA

Mabaki ya ndege iliyopotea ikiwa na watu 116 njiani kutoka Burkanafaso kwenda Algers yamepatikana nchini Mali.

Maafisa wa Jeshi wa Burkina faso wamesema ndege hiyo iliyokuwa chini ya shirika la ndege la Algeria imeanguka karibia kilomita 50 kutoka mpaka wa Burkanafaso.


Waongoza ndege walipoteza mawasilino na ndege hiyo muda mfupi baada ya kupata taarifa kutoka kwa Rubani kuwa alikuwa kwenye eneo lenye hali mbaya ya hewa.

Utafutaji wa ndege hiyo umeanzia katika eneo la Gao mpaka Tessalit. Kumekuwepo na hali mbaya ya hewa kwa zaidi ya saa 24. Waziri wa mambo ya nje wa ufaransa, Laurent Fabius amesema inaonekana ndege ilihamishwa mwelekeo kwa sababu ya hali mbaya ya hewa.

„Walikuwa wameelekezwa kubadili njia ya kawaida kutoka na mabadiliko ya hali ya hewa.

Ndege ilikuwa ikipaa juu ya eneo la Malian. Pamoja na juhudi kubwa , mapaka sasa hakuna dalili za kupatika na kwa ndege hiyo.


Pengine ndege imeangua"Ameongeza kuwa waziri wa ulinzi wa ufaransa alikuwa akisaidia katika utafutaji wa ndege hiyo. "Waziri wa ulinzi wameviruhusu vyombo vyao kwenda kwenye eneo kuitafuta ndege. Majeshi ya Algeria na Umoja wa mataifa wanafanya hivyo pia. Ndege mbili za jeshi la ufaransa zilizopiga kambi Niyame hivi sasa na tangu asubuhi zimekua zikiitafuta ndege hiyo.

Majeshi yetu katika eneo hilo ikiwamo vifaa vya matibabu vyote viko tayari

"Hapo awali, waziri mkuu wa Algeria Abdelmalek Sellal alitoa ufafanuzi wa tukio la kuanguka kwa ndege hiyo."


Usiku wa jana kama saa 9 ndege ya Hispania iliyokodiwa na Shirika la Ndege la Algeria ilikuwa katika safari yake kati ya Ouagadougou na Algiers.

Ilipoteza mawasiliano na Rada muda huo wa saa tisa usiku dakika 10 tu baada ya kupaa.

Mawasiliano ya mwisho ilikuwa na mnara wa kuongozea ndege ulioko Niger na ndege ilikuwa juu ya Gao, kama kilomita 500 kutoka kwenye mpaka wa Algeria. Kulikuwa na abiria 119 wakiwamo wafanyakazi wake.

Utafutaji bado unaendelea na tunawasilianana mamlaka zinazohusika. Waliokuwa kwenye ndege ni raia wa Algeria pamoja na mataifa mengine"Mamlaka zinazohusika nchini Burkina Faso ambako ndiko ndege ilitokea wameamua kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wanafamilia wa wale waliokuwa katika ndege. Baadhi ya ndugu wamefika katika uwanja wa ndege wa Ouagadougou kufuatilia taarifa kuhusu ndugu zao.


Baadhi walikuwa na malalamiko "Tuwanataka watuambie kama ndege hiyo imeanguka, kuna walionusurika, au wote wamekufa. Hayo ndio tunayotaka kujua. Tupo kwenye wakati mgumu. Watatu miongoni mwetu, tulitaka kusafiri na dada yetu lakini tuliamua kuahirisha safari katika dakika za mwisho. Hata hivyo dada yetu yeye aliondoka usiku jana." Mwaume mwingine aliyekuwepo kwenye uwanjahuo wa ndege alisema.

ISIS YAAGIZA WANAWAKE WAKEKETWE

ISIS yaagiza wanawake wote kuanzia umri wa miaka 11-46 kukeketwa.


Umoja wa Mataifa umeelezea ghadhabu kutokana na Fatwa iliyotolewa na Kundi la wapiganaji wa Kiislamu wa ISIS ya kuwataka wanawake wote waliozidi umri wa miaka 11 kukeketwa.
Afisa wa shirika la umoja wa mataifa nchini Iraq ,Jacqueline Badcock ameonya kuwa agizo hilo la kidini ama Fatwa itawaathiri zaidi ya wanawake milioni nne kati ya umri wa miaka 11-46.
Kundi hilo la wapiganaji wa Kiislamu ndilo linaongoza mashambulizi katika maeneo ya Kaskazini mwa Iraq na wao ndio wanaotawala mji wa Mosul.
Kundi hilo linalosheheni wapiganaji wa dhehebu la Sunni ndilo linaloendeleza wimbi la mashambulizi katika taifa hilo linalotishia kusambaratika katika ya maeneo yanayotawaliwa na madhehebu.
Ukeketaji sio kawaida nchini Iraq.
Mapema juma hili, Isisi iliwalazimisha Wakriso katika mji wa Mosul kuondoka na kuandika herufi N kwenye nyumba zao, hatua ambayo imetambuliwa kama kutaifisha mali za Wakristo katika eneo hilo.
Kulingana na amri hiyo mpya iliyotolewa chini ya Sharia, , wanawake wote kati ya umri wa miaka 11 na 46 wanapaswa kukeketwa.
ISIS yaagiza wanawake wote kuanzia umri wa miaka 11-46 kukeketwa.


Bi Badcock alisema kuwa utamaduni huo ni jambo geni sana nchini Iraq na ni swala linalopaswa kujadiliwa.
Alisema hayo alipokuwa akiwahutubia waandishi wa habari kupitia simu ya video katika mji mkuu wa Mkoa wa Kurdi wa Ibril.
Zoezi hilo la kuwapasha tohara wanawake limeenea sana katika mataifa mengi ya Afrika mashariki ya kati na jamii kadhaa barani Asia.
Baraza la Umoja wa mataifa lilipitisha mswada mnamo mwaka wa 2012 ya kuharamisha tamaduni hiyo ya upashwaji tohara kwa wanawake.
Isis ilitwaa mji wa Mosul mnamo mwezi wa Juni miongoni mwa miji mingine midogo midogo kuelekea mji mkuu wa Baghdad.

AJALI YA NDEGE YAUA ZAIDI YA WATU 40





Ndege ya Abiria ya Kampuni ya Trans Asia ya Taiwan imedondoka wakati ikijaribu kutua kwa dharura na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40.
Waziri wa usafiri wa Taiwan Yeh Kuang-Shih amesema watu 47 wamefariki na 11 kujeruhiwa katika ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 54 na wafanyakazi wa ndege wanne.

ATR 72 iliondoka Kaohsiung lakini ikapoteza mawasiliano baada ya mwendo wa saa moja ndipo ikaanguka na na kunawaka moto katika kijiji cha xixi kisiwani Penghu.
Meneja Mkuu wa TransAsia Hsu Yi-Tsung huku akilia, ameomba msamaha kwa ajali hiyo na akaahidi kuongeza juhudi za uokoaji na pia kuwasafirisha ndugu wa waliopoteza maisha kwenda kwenye eneo la tukio.

Siku za hivi karibuni Taiwan imepigwa na upepo mkali uliombatana na Mvua zilizoletwa na kimbunga Matmo, hata hivyo wanaosimamia anga katika eneo hilo wamesema hali ya hewa iliyokuwepo muda huo haikuwa inazidi kiwango kinachoweza kuzuia ndege kutua.

Habari za kuanguka kwa ndege hii kunakuja wakati visanduku viwili vya kutunzia kumbukumbu ya ndege ya malaysia iliyoangua nchini Ukraine tarehe 17 mwezi huu vikiwa vimefika mikononi mwa wataalamu wa masuala ya anga ili kuchunguza ni ni kitu gani kiliisibu ndege hiyo.

ALIYEBADILI DINI SUDAN KUSINI AKUTANA NA PAPA

Aliyebadili dini Sudan akutana na Papa Francis 


Mwanamke raia wa Sudan aliyesamehewa adhabu ya kifo baada ya kubadili dini amesafirishwa hadi nchini Italia baada ya kuwa kwenye ubalozi wa Marekani mjini Khartoum kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Meriam Yahia Ibrahim Ishag na familia yake waliondoka na ndege ya serikali ya Italia wakiongozana na Waziri wa nchini Italia Lapo Pistelli.
Baba wa Meriam ni muislamu na kwa Misingi ya sheria ya dini hiyo nchini Sudan Meriam pia ni muislamu na hawezi kubadili dini.
Meriam mwenyewe alilelewa na mama yake ambaye ni mkristo na kusema kuwa hajawahi kuwa muislamu.
Aliyebadili dini Sudan akutana na Papa Francis 


Pistelli Naibu waziri wa mambo ya nje wa Italia, aliweka picha yake na Meriam kwenye ukurasa wake wa facebook akisema kuwa wanaelekea kutua mjini Roma.
Mume wa Meriam Daniel Wani, ni mkristo,ana asili ya Sudani kusini na ana uraia wa Marekani.
Mtoto wa Meriam, Maya alizaliwa gerezani mwezi May, muda mfupi baada ya kuhukumiwa kunyongwa hatua iliyosababisha ghadhabu dunia nzima.
Aliachwa huru mwezi Juni baada ya kuwepo kwa mashinikizo.

NDEGE YA ALGERIA YATOWEKA NA WATU 116

Ndege ya Air Algerie imetoweka ikiwa na abiria 116


Shirika la ndege la Algeria , Air Algerie, limesema kuwa limepoteza mawasiliano na moja ya ndege zake ilipokuwa ikitoka mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou.
Afisa huyo anasema kuwa ndege hiyoya Air Algerie ilikuwa imepaa dakika 50 katika anga ya Sahara mara ya mwisho mawasiliano yao.
Ndege hiyo iliokuwa inaeelekea mji mkuu wa Algiers, ilikuwa na watu mia na kumi na wahudumu sita .
Oparesheni ya dharura ya kuitafuta ndege hiyo ieanzishwa,
Ndege hiyo nambari AH 5017 inamilikiwa na shirika la ndege la kihispania la Swiftair.
Mwandishi wa BBC Alex Duval Smith aliyeko katika mji mkuu wa Mali Bamako anasema kuwa kuna habari kuwa ndege hiyo huenda ilianguka katika eneo la janga la sahara kati ya
mji wa Gao and Tessalit .
Mwandishi huyo wa BBC ananukuu ripoti kutoka kwa wanajeshi wa kulinda amani walioko huko Mali na duru za shirika la habari la AFP.
Brigadia mkuu wa majeshi ya kulinda amani nchini Mali Koko Essien, amesema kuwa maeneo hayo ya jangwani yana idadi ndogo sana ya wakaazi kwa hivyo ni vigumu kupata habari kutoka huko na inawabidi kutafuta ilikoanguka ndege hiyo.
Ndege ya Air Algerie imetoweka ikiwa na abiria 116


Aidha Brig Essien anasema kuwa eneo hilo linamilikiwa na wapiganaji waasi .
Wamiliki wa ndege hiyo Swiftair wamesema kuwa ndege hiyo aina ya MD83 ilikuwa imeomba kubadili uelekeo wake kutokana na hali mbaya ya anga na ukungu mkubwa karibu na mpaka wa Algiers.
Ndege namba AH 5017 husafiri kupitia njia ya Ouagadougou-Algiers mara nne kwa wiki,AFP imeripoti.
Raia wa Algeria ni miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya Ndege hiyo,Gazeti moja la Algeria limeripoti.
Mwezi Februari ndege ya kijeshi ya Algeria ilianguka na kuuwa watu 77 waliokuwemo.
Tukio hili la hivi punde Linaloongeza wasiwasi kuwa njia inayotumiwa na misafara ya ndege ziendazo sehemu hiyo inapitia eneo lenye utata la anga ya Mali.

KIJANA ANG'OLEWA MENO 232

Madaktari nchini India wametumia saa 7 kufanikisha upasuaji wa kinywa cha kijana Ashik Gavai mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa akipata maumivu ndani ya kinywani.

Dr Sunanda Dhiware, mkuu wa Kitengo cha tiba ya meno katika hospitali ya JJ mjini Mumbai ameiambia BBC kuwa wamefanikiwa kuyang'oa meno 232 kinywani mwa Ashik aliyeletwa hospitalini hapo akiwa amevimba taya huku akilalamika kwa maumivu makali.

Madaktari wamesema wamelazimika kutumia nyundo na tindo kuyatoa meno hayo na wakadai kwamba hilo ni tukio la ajabu na linaingia katika rekodi ya dunia.
Hata hivyo Upasuaji huo umehusisha jopo la madaktari wanne.

Dr Dhiware anasema katika uzoefu wake wa miaka 30 ya udaktari wa kinywa na meno hajawahi kukutana na tukio lanamna hiyo.

Ameongeza pia kuwa kulingana na vitabu vilivyopo vinasema hali kamahiyo inaweza kujitokeza katika taya la juu na meno yaliyowahi kung'olewa katika hali hiyo yalikuwa 37 lakini cha kushangaza ni kuwa tukiola Ashik Gavai limetokea katika taya ya chini na ameng'olewa meno 232 idadi ambayo ni kubwa huku akisalia na 28 kwa matumizi yake ya kawaida wakati kitaalamu mtu mzima anapaswa kuwa na meno 32.

Baba mzazi wa kijana Ashik, Suresh Gavai amenukuliwa akisema mtoto wake alikuwa akilalamika kwa miezi kadhaa juu ya maumivu na kwamba walidhani inaweza kuwa ni matatizo ya saratani na ndipo wakamleta Mumbai




MBUNGE MWANAMUZIKI AUAWA KWA KUPIGWA RISASI

Mwanamuziki mashuhuri ambaye pia mbunge katika bunge la Somalia Saado Ali Warsame ameuawa kwa kupigwa risasi.


Msemaji wa kundi la wanamgambo wa kiislamu al-Shabab Abdulaziz Abu Musab aliiambia BBC kuwa mbunge huyo aliauawa kutokana na siasa zake wala sio muziki.

Mwandishi wa bbc mjini Mogadishi Mohammed Moalimu anasema kuwa mbunge huyo ni wa nne kuawa mwaka huu.


Bi Warsame alipata umaarufuwakati wa uongozi wa rais Siad Barre ambaye alipinduliwa mwaka 1991 kupitia nyimbo zake zilizokuwa zikiiushutumu uongozi wake.

Mbunge huyo aliishi kwa kipindi kirefu nchini Marekani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kabla ya kurejea nyumbani mwaka 2012 ili kuwakilisha ukoo wake kwenye bunge jipya nchini Somalia.

Mapema mwezi huu mbunge mwengine Ahmed Mohamud Hayd aliuawa baada ya kutoka hotelini ambapo katika tukio hilo, mlinzi wake pia aliuawa na katibu wa Bunge pia alijeruhiwa.


Kundi la Al-Shabab, ambalo lina uhusiano na al-Qaeda, limeapa kuendelea na mashambulizi zaidi katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Wanamgambo hao walipoteza ngome yao mjini Mogadishu na kuchukuliwa na Vikosi vya Umoja wa Afrika mwaka 2011,lakini wameendelea kutekeleza mashambulizi ya mabomu namauaji mjini humo.


Msemaji wa kundi hilo Abdulaziz Abu Musab amesema kuwa kundi lake limetekeleza mauaji kama ilivyopangwa na kuwa wataendelea kuwafuatilia Wabunge wengine ikiwa hawataachana na Bunge.

Al-Shabab imekua ikipigania kuunda taifa la kiislamu nchini Somalia.

MKE WA ASKARI AKUTWA AMEKUFA CHUMBANI KWA DEREVA BODABODA

Jeshi la Polisi linamshikilia dereva mmoja wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya mke wa askari polisi kukutwa amekufa chumbani kwa dereva huyo.

Tukio hilo ambalo limezua gumzo kubwa wilayani humo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika eneo la New Mwanga wilayani humo na mtuhumiwa akidaiwa kukutwa akiwa amelewa chakari.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.


"Hilo tukio lina ukweli na bahati mbaya sana mumewe ndiyo kwanza amehamishiwa Geita na alikuwa akaripoti halafu aje kuchukua familia yake," alisema Ndemanga.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, alisema hadi sasa haijafahamika nini kilitokea na kwamba hilo ni moja kati ya mambo ambayo polisi inachunguza.


"Hayo yote kwamba ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo kijana, nini sababu za kifo yatajulikana kadiri upelelezi unavyoendelea," alisema.

Imeelezwa kuwa jana ilikuwa siku ya askari huyo kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.


"Mpaka sasa hivi haijajulikana nini hasa kilitokea huko chumbani na ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo dereva," alisema mmoja wa watu waliokuwapo katika eneo la tukio ambaye hata hivyo, hakutaka kutaja jina lake na kuongeza kuwa jana saa sita mchana, mwili wa mwanamke huyo ulichukuliwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi.


Taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na mikwaruzo shingoni hali inayotia shaka kuwa huenda alinyongwa.

Habari nyingine zinadai kuwa siku ya tukio, mwanamke huyo alikuwa ameaga kuwa anakwenda kanisani lakini baadaye simu yake ilipopigwa ilikuwa ikipokewa na mwanamume.


Ilidaiwa kuwa mume wa marehemu alipojaribu kupiga simuya mkewe, ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyeonekana kuwa ni mlevi wakupindukia hali iliyomtia wasiwasi na kuamua kuwapigia simu marafiki zake wa karibu ili wamsaidie kumtafuta ndipo walipopata taarifa kuwa ulikuwapo uhusiano kati ya shemeji yao na dereva huyo wa bodaboda. Ilidaiwa kuwa marafiki hao walikwenda moja kwa moja nyumbani kwa dereva huyo wa bodaboda ambako walimkuta akiwa amelewa na walipoingia ndani walimkuta shemeji yao akiwa ameshafariki dunia."


Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.

ANYONGA KICHANGA NA KUTUPA KISIMANI

POLISI mkoani hapa inamshikilia msichana wa miaka 18, aliyetajwa kwa jina la Rhoda Idetemya kwa tuhuma ya kumyonga mtoto wake wa miezi miwili.


Ilidaiwa kuwa, Idetemya baada ya kumnyonga mtoto huyo aliyetajwa kwa jina moja la Elizabeth, mwili aliutumbukiza katika kisima cha maji ya kunywa katika Kijiji na Kataya Nyasubi wilayani Kahama.


Ilielezwa kuwa mwili wa mtoto huyo uligundulika katika kisima hicho saa moja jioni wakati mkazi wa eneo hilo Ada Patrick (25) alipokuwa akichota maji.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilona alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliozuka kati ya msichana huyo na baba wa mtoto kukataa kutoa fedha za matumizi ya mtoto.

Chanzo:Habari Leo

KAMBI YA JESHI YAVAMIWA DRC

Kumetokea ufyatulianaji mkali wa risasi katika kambi ya kijeshi katika mji mkuu wa Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa zinasema kuwa raia wameondolewa katika eneo hilo na haijafahamika makabiliano hayo yaliyotokea katika kambi ya wanajeshi wakumlinda rais yametokana nanini.


Wadadisi wa mambo wanahisi kwamba kisa hiki huenda kikazusha utata tena kati ya Congo Kinshasa na Congo Brazzaville kwa vile shambulio lilitokea karibu na mpaka kati ya nchi hizo mbili.


Taarifa kutoka kwa serikali zinasema kuwa wavamizi walijaribu kupenyeza katika kambi ya kijeshi ya Camp Tshatshi na makabiliano yalizuka kwa zaidi ya dakika 30 hivi.

Jamhuri hiyo ya Kidemokrasia ya Congo imesakamwa na vita kwa kipindi kirefu sasa nahata rais aliyepo madarakani kwa sasa Joseph Kabila alichukua mamlaka baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila mwaka wa , 2001.

Duru zinasema kuwa wavamizi takriban 20 walijaribu kuingia ndani ya kambi hiyo lakini shambulizi likazimwa.


Raiya walihamishwa kutoka maeneo yaliyoko karibu na uwanja wa ndege ulifungwa wakati wa shambulizi hilo.

Serikali bado haijamtaja nani aliyeishambulia.


Hii sio mara ya kwanza kwa Camp Tshatshi kushambuliwa mwaka uliyopita kami hiyo ilishambuliwa tena na wakati huo wafuasi wa dini ya ya kikristo ya dhehebu linaloongozwa na Paul Joseph Mukungubila walilaumiwa.

GENGE LA ULIPUAJI MABOMU LANASWA ARUSHA

JESHI la Polisi jijini Arusha limewakamata watu 16 akiwemo Imam wa Msikiti wa Al Quba uliopo mkoani Arusha, Jafar Lema na mfanyabiashara 1 wote wakihusishwa na matukio ya ulipuaji wa mabomu jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai nchini (DCI), Issaya Mungulu, katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Arusha leo, Jumanne Julai 22, 2014 imedaiwa kuwa Julai 21, 2014 saa 20.00 usiku katika maeneo ya Sombetini, Jeshi hilo limewakamata Yusufu Ally (30) na mkewe Sumaiya Juma (19) wakiwa nyumbani kwao baada ya kupekuliwa walikutwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono Saba (7), risasi sita za bunduki aina ya shortgun, mapanga mawili, unga wa baruti unaokadiriwa kufika nusu kilo na bisibisi moja.

Mungulu amenukuliwa akisema kuwa Yusufu ni miongini mwa watuhumiwa waliokuwa wanatafutwa kwa ulipuaji wa mabomu maeneo yote jijini Arusha na kuwa mahojiano juu ya mtuhumiwa bado yanaendelea dhidi yake.
Aidha, amesema uchunguzi wa shauri hilo pamoja na matukio mengine ya milipuko yanaendelea ikiwa ni pamoja na kuwahoji watuhumiwa walioko mikononi mwa polisi na kuwakamata watakaobainika kuhusika na matukio hayo.


Mtuhumiwa mwingine wa milipuko nchini asakwa na Polisi

Hata hivyo, Jeshi hilo limesema linamtafuta, Yahya Hella (33) mkazi wa Mianzini mkoani humo, mwenyeji wa Chemchemu, Kondoa–Dodoma kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya ulipuaji mabomu nchini.

"Zawadi nono itatolewa kwa yeyote atakaye toa taarifa zitakazowezesha ukamatwaji wa mhalifu huyu na pia nipende kuwashukuru sana wananchi kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa jeshi letu hapa nchini"alisema Mungulu.


Watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani

Amesema kufuatia tukio la mlipuko wa bomu Julai 7, 2014 saa 22.15 usiku katika mgahawa wa VAMA, eneo la Uzunguni Jijini Arusha, ambapo watu wanane walijeruhiwa vibaya, Jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 25 kwa uchunguzi na kuwa kati yao watu sita watafikishwa Mahakamani mapema iwezakanavyo.


Amewataja watuhumiwa watakaofikishwa Mahakamani kwa tukio hilo kuwa ni pamoja na Shaaban Mmasa (26) ambaye ni mlinzi aliyekuwa zamu siku hiyo kwenye mgahawa huo, Athuman Mmasa (38) na Mohamed Nuru (30), wote walinzi katika Mgahawa wa Chinese uliopo eneo la Gymkhana jirani na eneo la tukio.


Wengine ni Sheikh Jaffar Lema (38) ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Olturmet katika wilaya ya Arumeru, pia alikuwa Imam wa Msikiti wa AL-QUBA mjini Arusha ambaye ametambuliwa kama mmoja wa viongozi walioratibu matukio ya milipuko ya mabomu maeneo balimbali nchini, Abdul Salim (31), wakala wa Mabasi Stendi Arusha, na Said Temba (42), mfanyabiashara wa Arusha.

Kwa mujibu wa Mtandao wa JamiiForums, inadaiwa kuwa kuna vijana wamekuwa wakisafirishwa kwenda Somalia kujifunza ugaidi na Alshabab lakini wananchi wanalilalamikia Jeshi la Polisi kwa kutochukua hatua mapema.


Chanzo: FikraPevu

OBAMA MATATANI, TANZANIA YALAUMIWA

SERIKALI ya Rais wa Marekani, Barrack Obama imeingia lawamani kutokana na kufumbia macho mapigano yanayofanywa nchini Palestina na mamia ya watu wakiangamia, huku wengine wengi wakikosa makazi.

Pia, Serikali ya Tanzania imelaumiwa kukaa kimya katika suala hilo, tofuti na enzi za Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alionesha msimamo usioyumba katika kupigania haki za Wapalestina.

Akizungumza Dar es Salaam jana,Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Nasri Jaish alisema kinachoendelea Palestina kwa sasa ni mauaji ya halaiki au kimbari(genocide), lakini anashangwa na ukimya wa jumuia ya kimataifa."

Mauaji yanayoendelea Palestina kwa sasa hukuna namna nyingine ya kuyaelezea zaidi ya kusema niya kimbari,kwa kipindi kifupi watu 400 wameuawa,300 kujeruhiwa na nyumba za ibada zimevunjwa.

"Jumuia ya kimataifa, akiwemo Rais Obama anasubiri nini kitokee Palestina ndipo wazungumze, kimsingi inasikitisha. Jumuia ya kimataifa ni lazima ivunje ukimya na kuiambia Israel unyama wanaofanya kwa Wapalestina umetosha,"alisema Balozi Jaish.

Kwa upande wake, Profesa Sheriff Rwizi alisema Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kusemea watu wanao kandamizwa, wakiwemo Palestina, lakini anashangazwa na ukimya uliopo hivi sasa.

Akimwelezea Mwalimu Nyerere kuhusu msimamo wake kwa Palestina wakati huo, Profesa Rwizi alifafanua kuwa Mwalimu alisema: "Israel ni lazima iachie maeneo iliyonyakua kutoka kwa Palestina, hakuna anayeweza kuangalia unyonyaji wa aina hiyo ukiendelea," huku akimnukuu Nelson Mandela aliyewahi kusema;

"Ubaguzi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu,Israel imewaondoa mamilioni ya watu katika makazi yao, huu ni ukandamizaji mkubwa ambao hauvumiliki."

Kwa sababu hiyo, alihoji iko wapinguvu ya Tanzania leo katika kuwatetea waPalestina.

WATU NANE WASHIKILIWA NA POLISI WAHUSIKA WA UTUPWAJI MABAKI YA BINADAMU

JESHI la Polisi Kanda ya Dar es Salaam linawashikilia na kuwahoji watu wanane kwa kutupa viungo vya binadamu katika bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaan Suleiman Kova amesema hayo leo Ofisi kwake wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Amesema kuwa watu hao wakimemo madaktari wa International Medical and Technological University (IMTU) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukiri kuhusika na tukio la utupaji wa viungo vya binadamu katika eneo hilo.

Kamishna Kova amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji na kufanya uchunguzikuona kama wahusika wamefanya kosa linalohitaji kuchukuliwa hatua za kisheria au hawana kosa.

Ameongeza kuwa kufuatia tukio hilo tayari Jeshi la Polisi Kanda Maalum limeshafungua jarada la uchunguzi kubaini ikiwa wahusika wametenda kosa linalohitaji kufikishwa kwenye vyombo vya sharia kwa hatua zaidi.

Kamishna huyo amesema kuwa katika kutekeleza jambo hilo tayari jopo la wachunguzi likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jaffar Mohamed linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha watu hao kutupa viungo hivyo katika eneo hilo na idadi ya watu kulingana na viungo vilivyotupwa.

Aidha Kamishna Kova amewasihi wananchi wasiwe na wasiwasi kwani viungo vilivyookotwa havina uhusianona mauaji ya watu wengi na wala havihusiki na masuala ya ushirikina.

Amewaahidi wananchi kutoa taarifa kamili mara tu upepelezi utakapokamilika.

Viungo vya binadamu vikiwemo mikono, miguu, vichwa , mapafu na mioyo viligundulika jana (21.7.2014) jioni vikiwa vimehifadhiwa katika mifuko ya plastiki 85 na kutupa katika bonde la MbweniMpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni.

Mara baada ya kugunduliwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni walivichukua na kuvipeleka katika Hospitali ya Taifa kwa uchunguzi zaidi.

MAFUTA BEI CHINI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza mchakato wa kutafuta namna ya kupunguza gharama za uingizaji wa mafuta nchini. Hatua hiyo itawezesha pia bei ya nishati hiyo nchini kushuka.


Chini ya mchakato huo, Ewura inataka kushusha gharama za uagizaji wa mafuta, kwa kuchagiza ushindani wa upatikanaji wa mitaji ya fedha za uagizaji nishati hiyo.

Inataka katika ushindanishaji wa watoaji wa fedha ambao ni benki, hatimaye kuwe na ulinganifu wa upatikanaji fedha hizo miongoni mwa kampuni za mafuta.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema jijini Dar es Salaam jana, baada ya kufanikiwa katika utaratibu wa uingizaji mafuta wa pamoja, sasa wameamua kukutana na wadau kujadili namna ya kushusha zaidi gharama za nishati hiyo muhimu.

Mkutano huo wa wadau ulikutanisha washiriki mbalimbali, ikiwemo Benki Kuu (BoT), kampuniza mafuta, benki za biashara.

Ngamlagosi alisema uingizaji wa pamoja wa mafuta, umesaidia kuokoa muda na gharama kubwa za fedha zilizokuwa zikilipwa kutokana na meli kukaa muda mrefu. Mjadala huo umelenga mambo mawili makuu, yatakayowezesha kushuka kwa nishati hiyo.


Ushindani wa benki

Mkurugenzi huyo mkuu wa Ewura alisema kwanza wanaangalia namna ya kuweka ushindani wa benki katika ulipaji wa huduma za mikopo ya kampuni, ambazo zinaingia mkataba kwa ajili ya ununuzi wa mafuta.

"Kwa mfano, kwa sasa ni asilimia moja ambayo inalipwa na mlaji, lakini bado tunataka tuangalie iweze kushuka zaidi ya hapa. Kwa mfano nchi ya Msumbiji, kampuni zinalipa kati ya asilimia 0.3 mpaka 0.4 kwa hiyo na sisi tufike huko," alisema Ngamlagosi.


Alisema jambo lingine ni kurekebisha barua za benki kwa ajili ya kuruhusu upakuaji wa mafuta. Alisema katika uagizaji wa pamoja wa mafuta, meli moja inakuwa na mafuta ya kampuni nne au tano na ikitokea mmoja akashindwa kuwasilisha barua husika, hukwamisha ushushaji wa mafuta.

"Hapa ikitokea mmoja akashindwa kuleta 'letter of credit' (barua) kutokana na kushindwa kuelewana na benki, anakwamisha mzigo wa watu wote, kwa hiyo hata hii tutaangalia namna ya kurekebisha," alisema.


Mafuta bei chini

Kwa mujibu wake, kwa sasa suala hili wamelileta kwa ajili ya majadiliano na kupata mawazo ya wadau wa sekta hiyo. Mpango huo utakapofanikiwa, utatoa unafuu kwa mtumiaji wa mwisho ambaye ni mlaji.


Aidha, utaratibu wa uingizaji wa mafuta kwa pamoja umebainika kupunguza gharama kubwa na hivyo kuwa nafuu kwa walaji na uchumi wa nchi. Taarifa ya mamlaka inasema utaratibu huo umeokoa takribani Sh bilioni 126 ambazo hutumika.

"Hata gharama zimepungua sana. Zamani meli moja ilikuwa inakaa karibu siku 40 hadi 60 na kwa siku zinakaa meli tano mpaka sita, ambazo zote ilikuwa lazima uzilipiedola za Marekani 20,000 kwa hiyo ilikuwa gharama kubwa sana," alisema.

JWTZ WAONYA JUU YA WANAOVAA SARE ZAKE

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeonya juu ya matumizi ya sare na vifaa vingine vya majeshi kwa watu wasiohusika.Limetangaza kuwa hatua kali za kisheria, zitachukuliwa dhidi ya watu hao.

Limehadharisha juu ya uvaaji, uingizaji nguo nchini ikiwemo mitumba, kwamba kama itatokea, zinafanana kwa aina yoyote ile na ikadhaniwa ni za jeshi hilo, mtu anayehusika atafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za majeshi zilizopo.

"Msisitizo uliwekwa hapa katika vifungu vya sheria ni kwamba sio lazima ukutwe na sare ambazo zinatumiwa na JWTZ. Hasha!. Hapa sheria inasema hata kama tu nguo hiyo itaelekea kufanana kwa namna yoyote ile na sare za JWTZ, ni kosa la kisheria kuitumia," ilisema taarifa ya Jeshi kwa vyombo vya habari.


Taarifa hiyo ilitolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano, Makao Makuu ya Jeshi, jijini Dar es Salaam, jana. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtu yeyote yule asiyena ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza nchini sare za jeshi, atakuwa ametenda kosa, hivyo atafikishwa mahakamani.

Tamko hilo la jeshi linasema kwa muda mrefu sasa katika miji mikubwa, hasa Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma na mikoa mingine, kumekuwa na ongezeko la matukio ya wizi na uhalifu wa kutumia silaha.


"Imeonekana kuwa wanaohusika navitendo hivyo, baadhi yao huonekana wamevaa sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na zimekuwa zikitumika katika matukio yenye sura ile ile," ilisema.

Taarifa hiyo ilisema, "Hivi karibuni vichwa vya habari vimetawala sana kwenye vyombo mbalimbali vya habari sehemu mbalimbali hapa nchini, mara utasikia 'Mwanajeshi feki mbaroni Tanga' au AliyejifanyaOfisa wa JWTZ akamatwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na mengine mengi."

Ilisema pia kumejitokeza mtindo wa baadhi ya wasanii hasa wanamuziki wa kufokafoka maarufu bongo fleva, kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare zajeshi, kama vile suruali, viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia.

Kulingana na taarifa hiyo, mitaani nako kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi, hasa vijana, wanaovaa sare za jeshi, ambao wakiulizwa wanakozitoa, hudai wamenunua kwenye mitumba au kwenye maduka ya nguo.


"Ukipita kwa wauza mitumba nao utakuta wanauza nguo za jeshi, ingawa wao hufanya biashara hiyo kwa kificho, kwani huziweka sare hizo kwa nyuma ndani kwenye maghala yao na kuziuza kwa kifichona usiri mkubwa kwani wanafahamu kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi kuuza sare hizo, ingawa wapo baadhi yao ambao huziuza hadharani wakidai kuwa ni mitumba," ilisema.

Taarifa hiyo ilisema inawezekana kuwa kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji wa sare hizo, hawafahamu kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi, kukutwa na sare yoyote ile ya kijeshi, lakini kutokujua sheria, siyo utetezi mbele ya mahakama.

SHEHENA YA MABAKI YA BINADAMU YAKAMATWA BUNJU


Shehena yenye viungo vya binadamu vikiwa vimekaushwa na kuwekwa kwenye mifuko ya plastiki zaidi ya 85,imekutwa imetupwa katika dampo lisilo rasmi la Bunju"A"bonde la mto mpiji, mpakani mwa jiji la Dar-es-salaam na Bagamoyo mkoani Pwani,hali iliyozua taharuki,simanzi na mshangao kwa wakazi wa eneo hilo la Bunju.
Katika eneo hilo maarufu kama bonde la mto mpiji na kukumbana na umati wa watu wakienda kushuhudia tukio hilo ambalo wananchi hao walikuwa wakishangaa kutokea katika eneo lao,huku jeshi la polisi kituo cha polisi bunju na wale wa wazo hill,wakijaribu kuzuia umati wa watu wasisogelee katika eneo la tukio.

Nao mashuuda wa tukio hilo Bwana Ruta na Bwana Huseni wamesema kuwa mama mmoja aliyekuwa akiponda kokoto katika eneo hilo ambalo si halali kwa shuhguli za machimbo na dampo, aliona gari likija na kumwaga mifuko hiyo,ambapo mara baada ya kuondoka wamwagaji hao alikwenda kutafuta chohote kitu na ndipo alipokumbana na kadhia hiyo na kukimbia na kuomba msaada.

katika kituo kidogo cha polisi Bunju, jeshi la polisi chini ya kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni kamishan msaidizi wa polisi Camilius Wambura. Walilazimika kuongeza ulinzi ili kudhibiti wananchi hasa bodaboda waliokuwa wamefurika katika kituo hicho ili kujua hatma ya tukio hili mara baada ya kuwepo kwa tetesi za gari dogo maarufu kama kiyoliyoli kufikishwa kituoni hapo huku ndani ya gari hilo likitoa majimaji yaliyoashiria uwepo wa mizigo waliyotilia shaka.

Katika eneo la tukio wananchi wakishirikiana na askari wa jeshi la polisi walivalia kiraia, walichukua shehena hiyo na kwenda kuiihifadhi sehemu salama, ambapo licha ya zoezi hilo kufanyika karahisi kwa kuvalia gloves bila ya maski za puani, huku baabdhi ya wadadisi wa mambo wakisema huwenda zoezi hilo likawa na madhara kwa wahusika kwani viungo hivyo havikujulikana mara moja vilikaushwa kwa dawa gani.

kamandaa wa polisi mkoa wa kipolisi kinondoni Acp Camilius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa bado jeshi linaendelea na upelelezi ili kujua hiyo mifuko zaidi ya 85 yenye viungo vya binadamu vikiwa vimekaushwa kwa ustadi vimetoka wapi na pindi uchunguzi utakapo kamilika watatoa majibu.

WANAKIJIJI WAFANYA UHARIBIFU MALI KWA KUMTUHUMU UCHAWI MWANAFAMILIA

Wakazi wa kijiji cha Nguruka wilayani Uvinza mkoani Kigoma, wamechoma nyumba nne za familia moja yenye zaidi ya watu ishirini na kuteketeza vyakula na mali nyingine zenye zaidi ya shilingi milioni mia moja baada ya kumtuhumu mmoja wa wanafamilia kwa ushirikina.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mkoronga katika kijiji cha Nguruka Matei Charle ambaye alimuokoa mtuhumiwa wa uchawi aliyetambulika kwa jina la Siyajui Ahmad, amesema mama huyo alianza kushambuliwa akiwa katika msiba wa kijana Masoud Vyombo ambaye alifariki ghafla ambapo wakazi wa kijiji hicho waliomtuhumu kumuua kwa njia ya ushirikina walianza kumshambulia kabla ya kuokolewa ambapo mamia ya wananchi waliamua kuteketeza nyumba yake pamoja na nyumba tatu za kaka zake na wazazi wake, huku Siyajui Ahmad aliyetuhumiwa akieleza kuwa familia hiyo imepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni mia moja na kwamba alilazimika kutoroka ili kuokoa maisha yake.

Kamanda wa polisi mkoani Kigoma Frasser Kashai amesema jumala ya watu kumi na watano wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku kwa upande wake katibu mwenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Uvinza Majaliwa Zuberi akitoa wito kwa wananchi kutochukua sheria mkononi na akiitaka kamati ya maafa ya wilaya kuzisaidia familia nne zilizoathirika ambazo kwa sasa zinalala nje na hazina chakula, mavazi na mahitaji mengine ya msingi.

MAPIGANO YAENDELEA UWANJA WA NDEGE TRIPOLI

Mapigano yamezuka tena kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Libya, siku mbili baada ya wapiganaji kukubaliana kusitisha mapambano.

Ripoti zinasema kuwa vifaru vinatumiwa katika mapambano makali katika uwanja wa ndege wa Tripoli, ambao umeshambuliwa kwa makombora na mizinga.

Uwanja huo ulianza kushambuliwa juma lilopita na ikalazimika kuufunga.

Wakuu wa Libya wameonya kuwa kazi ya kukarabati uwanja huo itachukua miezi na kugharimu mamilioni ya dola.

AL SHABAAB WASHAMBULIA TENA LAMU

Kundi la Al shabaab limekiri kutekeleza shambulizi katika basi moja la abiria katika pwani ya Kenya hapo jana usiku.

Shirika la msalaba mwekundu limesema kuwa watu saba walipigwa risasi na kufariki huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Shambulizi hilo lilitokea katika mji wa Witu katika Kaunty ya Lamu.

Watu kadhaa wameuawa katika Pwani ya Kenya katika kipindi cha miezi kadhaa iliopita.

Kundi la Alshabaab limekiri kutekeleza mauaji hayo.

Linasema kuwa linalipiza kisasi kuwepo kwa majeshi yaKenya nchini Somali.

Ghasia hizo zimeathiri pakubwa sekta ya utalii nchiniKenya.

409 WAKAMATWA KWA UJANGILI KATAVI

WATU 409 wanaosadikiwa kuwa majangili sugu wamekamatwa wakifanya ujangili katika Hifadhi yaTaifa ya Katavi wilayani Mlele mkoa wa Katavi katika kipindi kilichoanzia Juni 2013 hadi Juni mwaka huu.


Katika kipindi hicho, silaha kadhaa zimekamatwa ndani ya hifadhi hiyoya Taifa zikiwemo bunduki nzito aina ya SMG zipatazo tano, riffle G3 zipatazo nane pamoja na risasi zipatazo 357 za SMG.

Silaha nyingine zilizokamatwa katika kipindi hicho ni pamoja na bunduki aina ya shotgun zipatazo 21, bunduki zilizotengenezwa kienyeji "magobori" yapatayo 138.

Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Hifadhiya Taifa ya Katavi, Mhifadhi Davis Mushi wakati akitoa taarifa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mpanda (DDC) iliyoketi mjini hapa.


Alibainisha kuwa kuwepo kwa makazi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mlele na Mishamo wilayani Mpanda karibu na Hifadhi ya Taifa ya Katavi kumesababisha wakimbizi wa makazi hayo kujihusisha ujangili kama njia ya kupatia kipato chao.

Akifafanua alibainisha kuwa mtandao wa watu kupitia mkoa wa jirani wa Kigoma na wakibadilishana na majangili na meno ya tembo.

WAKAMATWA KWA WIZI WA KILO 40 ZA TANZANITE

WAFANYAKAZI saba wa kampuni yaTanzanite One, wakiwemo viongozi wakuu wa idara ya ulinzi ya kampuni hiyo wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za wizi wa madini aina ya tanzanite yenye uzito wa kilo 40 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 10.


Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki alisema wizi huo ulitokea majira yasaa 8 usiku juzi, ikielezwa wafanyakazi hao walishirikiana na wafanyakazi wa Shirika la Madini laTaifa (STAMICO) kupanga wizi huo.

Nsimeki alisema uchunguzi wa awali umebaini mpango mzima wa viashiria vya upangaji wizi huo umefanywa na wafanyakazi hao na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi ambao bado hawajakamatwa mpaka sasa, lakini polisi iko katika msako mkali dhidi yao.

Alisema kiutaratibu madini yote yanayotoka mgodini kwenda kwenda chumba maalumu cha kuhifadhi madini, husafirishwa na gari maalumu lisiloruhusu risasi kupenya.


Nsimeki alisema cha kushangaza siku ya tukio hilo, shehena hiyo ya madini ilisafirishwa kwa gari ya kawaida aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 256 APQ, mali ya kampuni hiyo hatua ambayo ilihisiwa wafanyakazi hao pamoja na viongozi wa idara ya ulinzi walikuwa wanajua kikamilifu kilichokuwa kikiendelea.

Kamanda huyo alisema mara baada ya madini kupakiwa kwenye gari hilo la kupangwa kuelekea katika chumba cha kuhifadhia madini, ghafla walisikia risasi zikilia na moja ya risasi iligonga mlango wa gari hiyo na nyingine kwenye chesisi ya gari.


Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya walinzi na dereva wa Kampuni ya Tanzanite One kuona hali hiyo nao walitimua mbio bila ya hata ya kujitetea pamoja na kwamba walinzi hao walikuwa na silaha za moto na za kisasa za ulinzi.

''Lakini cha kushangaza muda mfupiwalinzi hao walirejea katika gari nakukuta mifuko miwili ya kilo 15 na 25 imeshachukuliwa na majambazihao na kutoweka nayo,'' alisema.


Hata hivyo, mfuko mmoja wenye uzito wa kilo 25 umepatikana ndani ya gari ya kampuni hiyo, kwani majambazi walishindwa kubeba kwa kuwa ulikuwa mzito nakuchukuliwa na kuhifadhiwa katika ofisi za Tanzanite One.

Nsimeki aliwataja wanaoshikiliwa na polisi ni pamoja na viongozi wakuu wa idara ya ulinzi ambao ni George Odeku Kisambe (38), mkaziwa Arusha ambaye ni meneja wa kitengo cha kamera (CCTV) na pia ni mkuu wa idara ya ulinzi na Jonathan Nyange (52), mkazi wa Kilimanjaro na pia ni dereva wa gari hilo.


Wengine ni Hussein Ng'ombo (64), mkuu wa zamu siku hiyo, Sunday Nzogora (35) mkaguzi wa Madini, Rodney Ngowi (48), na Samwel Kajumu (29) ambao ni mafundi mitambo, wote wakazi wa Mkoa waKigoma na Erick Briygy (44) raia waAfrika Kusini ambaye ni mdhibiti wa madini wa Tanzanite One.

Hii ni mara ya pili kufanyika kwa wizi huo, kwani mara ya mwisho ilikuwa mwaka juzi ambapo watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walivamia chumba maalumu na kuiba shehena kubwa ya madini yenye thamani ya mabilioni na kutokomea nayo kusikojulikana.

UKAWA WABADILIKA

VIONGOZI wanaounda kile kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesema hawako tayari kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka kesho huku nchi ikiwa na Katiba ya zamani, hivyo keshokutwa wanatarajiwa kuingia katika mazungumzo kunusuru mchakato mzima wa Katiba.

Wameeleza kuwa, kwa kutambua muda mfupi uliobaki kati ya mchakato wa Katiba kumalizika na Uchaguzi Mkuu, watafanya mazungumzo hayo kwa faida ya Taifa na wananchi waliojitokeza kwa wingi kuwasihi warejee katika Bunge Maalumu la Katiba linalotarajiwa kurejea kwa siku 60 kuanzia Agosti 5, mwaka huu.

Awamu ya kwanza ya Bunge hilo ilikutana kwa siku 70, lakini kutokana na wajumbe kusigana kwa mambo kadhaa, yakiwemo ya kiitikadi na kutoaminiana, liliahirishwa Aprili 25 mwaka huu ilikupitisha Bunge la Bajeti bila kuwepo na sura ya kukamilika karibuni.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mmoja wa viongozi wa umoja huo ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wana imani kuwa taifa linahitaji Katiba mpya hivyo watajadili katika mazungumzo hayo ya Jumatatu ili kuwawezesha kupatanjia mbadala iwapo mchakato huo utakwama.

Akifungua kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, Mbowe alisema kwa niaba ya uongozi wa Ukawa wanapongeza hatua ya taasisi, viongozi wa dini na watu mbalimbali kuwasihi kurudi katika Bunge la Katiba, na kwamba wako tayari kufanya mazungumzo kuhusukurejea bungeni.


Alisema hata kama kwenye mazungumzo hayo watakubaliana kurejea bungeni na wakiwa katika bunge hilo kutajitokeza maamuzi yakutaka kulivuruga bunge, hawatasitakuchukua hatua kama ya awali.

"Napenda kuwataarifu wananchi kuwa Ukawa tuko tayari kwa mazungumzo kwa nia ya kunusuru mchakato wa Katiba kuendelea kama walivyotusihi watu mbalimbali, lakini tutaenda katika mazungumzo hayo Jumatatu kwa kuhakikisha mchakato huo hautanajisiwa," alisema.


Alidai kuwa wao kama chama cha siasa wamepata habari za ndani zinazodai kuwepo kwa njama za kuvuruga mchakato huo ili kuendelea kutumika kwa Katiba ya zamani, jambo alilodai kuuliza dhamira hizo katika mazungumzo hayo.

"Sisi hatuko tayari kuona uchaguzi ujao unafanyika kwa kutumia Katibaya zamani na tume ya uchaguzi iliyopo, hivyo tutahakikisha tunakwamua hali hii ili mchakato uendelee," alisema Mbowe na kuongeza kuwa, watu mbalimbali wamekuwa wakiwasihi Ukawa kurejea bungeni bila kuzungumza kwa nini waliamua kutoka nje ya bunge na kwanini mchakato huo unatishia kukwama.


Alisema viongozi wa Ukawa wamejadiliana na kufikia maamuzi kuwa hawakatai mazungumzo, bali wanachopinga ni kurudi Bungeni kabla sababu iliyowafanya watoke haijafanyiwa kazi huku akieleza kuwa mwenye mamlaka ya kuokoa mchakato huo ni Rais Jakaya Kikwete.

"Hatuwezi kuwa wanasiasa wa kuzirabali mazungumzo ni kitendo cha uungwana wa kawaida katika uongozi pale inapotokea kutoelewana kwa kuangalia tatizo nakufanyia kazi kwa ajili ya kunusuru mchakato na kurudi katika mchakato," alisema.


Alisema katika mkutano wa awali kujadili jinsi ya kunusuru mchakato huo walikubaliana kila chama kuweka bayana vikwazo vya mchakato ambapo chama tawala na Ukawa kila moja walitoa sababu zao.

Mbowe alisema baada ya kutoa taarifa zao watazijadili katika kikao hicho cha kamati kwa siku mbili, ikiwa ni pamoja na hali ya siasa nchini, mchakato mzima wa katiba pamoja na suala la uchaguzi wa serikali za mitaa na kisha kutoa taarifa kesho.


Naye, Mjumbe wa Kamati hiyo, Profesa Mwesiga Baregu alisema jambo la msingi ni Ukawa kurejea bungeni na kukubaliana katika bunge hilo kuongozwa na agenda zilizo chini ya sheria kwa kujadili kilichopo katika Rasimu ya pili na kujadili nje ya rasimu ni kuvunja sheria.

Alisema pia Ukawa wanatakiwa kuwa makini na wanaotaka warejee bungeni kwani siyo kila mmoja nia yake ni njema.

Chanzo: Habari leo

WANAKIJIJI MAKETE WATAKA BANGI ILUHUSIWE

Huku harakati za kutaka matumizi ya Bangi kuhalalishwa zikishika kasi katika sehemu mbali mbali duniani, Tanzania haijaachwa nyuma.

Wanakijiji katika wilaya ya Makete , mkoa wa Njombe Kusini Magharibi mwa Tanzania wanataka serikali iweke sheria ambayo itaweza kuhalalisha matumizi ya mmea huo.

Wanakijiji hao zamani walikuwa wakitumia mbegu za mmea huo kukaanga na chakula lakini siku hizi wanalazimika kuzitumia kwa usiri mkubwa wakihofia kukamatwa na polisi.

Mwenyeketi wa Halmashauri ya wilaya ya Makete Daniel Okoka amesema matumizi ya Bangi katika wilaya hiyo hayajaanza leo, tangu zamaniwatu kitamaduni walikuwa wakitumia Mbegu za Bangi kukaanga na chakula.

Na kama mmea huo ungekuwa na tahri kubwa kiafya, basi watu wengi wilayani humo wangekuwa vichaa.

Miti ya mimea hiyo pia ilikuwa ikitumiwa kutengeza kamba ambazo anasema zilikuwa za nguvu sana.

Lakini kwa sababu ya sheria kali, matumizi ya Bangi au Marijuana yanafanywa kichinichini katika wilaya hiyo.

NDEGE YATUA KATIKATI YA BARABARA

Shughuli ziliathirika leo wilayani Mityana baada ya ndege kutua kwa dharura katika barabara ya magari ya Mityana.

Ndege hiyo N604AR, iliyokuwa imewabeba wanajeshi wa Marekani, ilituakatika eneo la Kiwawu umbaliwa kilomita 22 kutoka wilaya ya Mityana.

Kwa mujibu wa mtandao wa Nation, kamishna wa wilaya Joel Walusimbi, alithibitisha tukio hilo akisema rubani wa ndege hiyo alilazimika kutua katikati ya barabara

Polisi walisema kuwa ndege hiyo ilikuwa inaelekea mjini Juba Sudan Kusini kutoka uwanja wa ndege wa Entebbe.

DUNIA YAMKUMBUKA MANDELA

Hii leo ni siku ya kimataifa ya kusherehekea maisha ya hayati Nelson Mandela.


Wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa wakifanya shughuli mbali mbali za kijamii kumkumbuka.

Moja ya shughuli hizo imekuakufanya usafi.

Waziri wa Mambo ya nchi za njee wa A-Kusini pamoja na kikosi cha mabalozi kadha wanaoishi A-Kusini wameweza kufanya usafi katika kituo kimoja cha magari ya abiria (Daladala) mjini Pretoria.


Huu ulikuwa wito wa Rais Jacob Zuma kwa raia wa afrika ya kusini kulisafisha taifa lao.

Lakini baadhi yao wamelalamika wakisema kuwa hiyo ni kazi ya serikali.


Ili kuadhimisha kuzaliwa kwake mamilioni ya watu pia wamejitolea kutumia dakika 67 za mda wao kufanya mambo mema ili kuadhimisha miaka 67 aliyotumia kama mwanaharakati wa kisiasa.

Vuguvu hilo lilianzia mjini Johanesburg na New York mnamo mwaka 2009 lakini sasa linasimamia mataifa 126.


Bwana Mandela, aliyefariki mwaka jana alisifika sana kwa kupigana vita dhidi ya utawala wa mzungu.

Aliishi grezani mwa miaka 27 kabla ya kuwa rais wa kwanza mzalendo nchini Afrika Kusini mwaka 1994.


Kabla ya kifo chake aliugua homa ya mapafu kwa mda mrefu, ugonjwa ambao mara kwa mara ulikuwa unazuka mwilini mwaka hata baada yamatibabu.

Mnamo siku ya Alhamisi, vitu vinavyosimulia maisha yake vilinadiwa kama kumbukumbu kwa maisha yake na kuchangisha pesa ili kusaidia shirika la kibindamu.

AMUUA MTOTO WA MIAKA TISA KISHA KULA UBONGO WAKE

MAUAJI ya kutisha yanaendelea kuuandama mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kijana Laurance Flavian (20), mkazi wa Marangu Mashariki kumuua Mwanafunzi wa darasa la Pili katika Shule ya Msingi Marangu Hills, Francis Fortunatus (9), kwa kumkata mapanga sehemu za kichwani na kula ubongo wake, kisha na yeye kujikata uume wake na kusababisha mauaji hayo.


Akizungumza Kamanda wa polisi mkoani humo, Robert Boaz, amesema tukio hilo limetokea leo Ijumaa Julai 18, 2014 saa7:15 asubuhi katika eneo la Marangu Pentekoste katika Wilaya ya Moshi mkoani humo.


Amesema mtoto huyo ambaye pia ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Marangu Hills alikutwa na mauti wakati akielekea shuleni na kuwa kijana huyo (Laurance Flaviani), alianza kumshambulia kwa kumkata na mapanga sehemu za kichwani nakutoa ubongo wake na kuula hali iliyomsababishia, kufariki dunia papo hapo.


Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda Boaz, kijana huyo baada ya kumuua mtoto huyo nayeye alijijeruhi kwa kuukata uume wake, na kukimbizwa katika Hospitali ya Kilema ambapo alikufa wakati akipatiwa matibabu kutokana na kutokwa na damu nyingi kaatika sehemu aliyojikata.

"Mtoto huyu akielekea shuleni asubuhi ghafla kijana huyo ambaye nay eye sasa ni marehemu, alianza kumshambulia kwa kumkata kwa panga kichwani bila sababu yeyote, hali iliyosababisha kifo cha mtoto huyo papo hapo"Kamanda Boaz.

Aidha, amesema chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana na kuwa taarifa za awali kuhusu tukio hilo kinasadikiwa kuwa kijana huyo alikuwa na ugonjwa wa akili na kwamba kabla ya kutenda tukio hilo alikuwa akifanya vurugu na kuvunja vioo vya nyumba yao za watu katika eneo hilo.


Mashuhuda wasimulia

Hata hivyo, taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kijana huyo baada ya kutekeleza mauaji hayo ambapo inadaiwa mtoto aliyemuua ni mtoto wa bosi wake wake na kwamba baada ya kuukata uume wake alianza kuula kama nyama choma huku akikata kipande kimoja baada ya kingine.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Tetrula Kimario, amesema kijana huyo ambaye alikuwa akifanya kazi ya kutengeneza Sanamu za mapambo katika kiwanda kilichopo Marangu Pentekoste, na kuwa Julai 17, 2014 alianza kubadilika kwa kufanya vitu visivyoeleweka ambapo tajiri yake ambaye ni Baba wa mtoto aliyeuawa alimchukua na kumrudisha nyumbani kwao karibu na alipokuwa anaishi mwanzoni.


Amesema, ilipofika leo asubuhi mtoto wa bosi wake alitoka kwenda shule, ndipo kijana huyo alipomkata kichwa na kisha kuanza kula ubongo wake, ambapo watu walifikia katika eneo la tukio waliamua kumpiga kwa mawe hadi polisi walipofika katika eneo la tukio.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, mkoa huo umekumbwa na matukio ya mauaji na unyanyasaji wa watoto waliochini ya umri wa miaka kumi na nane (18).

NDEGE YA MALAYSIA YADAIWA ILISHAMBULIWA


Kuanguka kwa ndege ya Malaysia si ajali,bali shambulio la kigaidi yasema Ukraine


Maafisa nchini Ukraine wanasema kuwa ndege ya abiria iliyoanguka nchini humo ilidunguliwa katika eneo la mashariki mwa taifa hilo ambako waasi wanaoiunga mkono Urusi wamekuwa wakipigana na vikosi vya serikali.
Wanasema abiria wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo ya shirika la Malaysia iliyokuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kuelekea Kualar Lumpur wameufariki.
Wengi wa abiria hao walikuwa ni raia wa Uholanzi.
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alitaja tukio hilo kama kitendo cha ugaidi.
Maafisa wa Ukraine walichapisha kile walichotaja kuwa mawasiliano ya simu yaliyonaswa kati ya waasi wakiwaeleza maafisa wa Urusi kwamba ni wao ndio waliohusika katika kuindungua ndege hiyo.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Ukraine, Pavlo Klimkin, amesema kuwa serikali ina ushahidi wa kutosha kwamba ndege hiyo ilidunguliwa.
Takriban Abiria 300 wa mataifa mbalimbali wamefariki baada kuanguka kwa ndege hiyo.


' Tulinasa pia mawasiliano ya simu kati ya magaidi hao wakizungumzia kundunguliwa kwa ndege hiyo.
Kwa sasa tunatafsiri sauti zao na kisha tutaziweka kwenye mtandao wa internet ili kuthibitisha hilo."
Hata hivyo sauti hizo zilizonaswa bado hazijathibitishwa na upande uliohuru na waasi hao wamekanusha kuhusika wakisema kuwa ni wanajeshi wa serikali ndio walioidungua ndege hiyo.
Kadhalika marekani imesema kuwa inaamini ndege hiyo ililipuliwa angani na wala halikuwa tukio la ajali.

Makamu wa rais Joe Biden hata hivyo amesisitiza kuwa Marekani bado inatafuta maelezo.
''Ndege ya Malaysia iliyokuwa ikitoka Ulaya magharibi kuelekea Kuala Lumpur, yaelekea ilipokuwa ikivuka karibu na mpaka kati ya Ukraine na Urusi, nasema yaelekea kwa sababu hatuna taarifa za kina, nataka kuwa makini na kile ninachosema yaelekea ilidunguliwa, ilidunguliwa na wala sio ajali. Ililipuliwa kutoka angani. Tunaona ripoti kwamba huenda raia wa Marekani walikuwa kwenye ndege hiyo na bila shaka huo ndio wasiwasi wetu wa kwanza.''
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema kuwa Ukraine inapaswa kuwajibika katika tukio la udunguaji wa ndege hiyo.

Msemaji wa serikali ya Urusi amesema kuwa mkasa huo haungetokea ikiwa Kiev haingeimarisha harakati zake za kijeshi mashariki mwa Ukraine.

MSHUKIWA WA UGAIDI KENYA AKAMATWA TANZANIA

Mmoja wa watuhumiwa wa matukio ya ugaidi nchini Kenya, Jihad Gaibon Swaleh, amefikishwa mahakamani nchini Tanzania.

Mshukiwa huyo amesomewa mashtaka ya kufadhili vitendovya kigaidi nchini Kenya.


Pamoja naye watuhumiwa wengine 16 ambao wanadaiwa kuendesha vitendo vya kigaidi nchini Tanzania pia wamefikishwa mahakamani hii leo wakikabiliwa na tuhuma za kula njama ya kutenda makosa ya kigaidi nchini Tanzania.

Washtakiwa wote 17 wamerejeshwa rumande baada ya kusomewa mashtaka ya vitendo vya kigadi nchini Tanzania pamoja na nchi jirani ya Kenya.


Upande wa mashtaka ukiongozwa na mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa serikali mwandamizi Prosper Mwangamila ulidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dares Salaam, kuwa kwa kutumia mtandao wa facebook aliweza kushawishi watu wengine kuwasiliana kwa lengo la kutafuta vifaa vya kulipua mabomu nchini Kenya na kusababisha majerahi, hofu na Vifo.


Jihand Gaibon Swaleh ambaye amesomewa mashtaka mawili hakuruhusiwa kukiri wala kukana mashitaka yanayomkabili kutokana na kwamba mashitaka hayo yanaangukia katika makosa ya ugaidi ambayo kwa mujibuwa sheria nchini Tanzania mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kuendesha kesi za namna hiyo.

Katika kesi ya awali kutajwa mahakamani hapo washtakiwa wengine 16 walisomewa mashtaka mawili ikiwemo kula njama kutenda kosa pamoja na kushawishi wenzao kushiriki katika vitendo vya kigaidi katika sehemu mbali mbali nchini Tanzania.


Ni makosa ambayo wanadaiwa kutenda kati ya Januari mwaka 2013 na Juni 2014 katika maeneo tofauti Tanzania.

Katika kesi zote mbili dhidi ya washtakiwa hao Upande wa mashtaka uliiambia mahakama iliyokuwa chini yahakimu mfawidhi wa mahakama hiyo bi Hellen Riwa kuwa upelelezi bado unaendelea na hivyo kuiomba mahakama kuahirisha kesi hizo hadi mwishoni mwa mwezi huu waJulai.


Awali mapema asubuhi msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania Bi Advera John Bulimba aliwealeza waandishi wa habari kuhusu tuhuma dhidi ya washtakiwa hao.

Hii ni mara ya kwanza kwa kundi kubwa la watuhumiwa kufikishwa mahakamani kwa pamoja wakikabiliwa na tuhuma za makosa ya kigaidi huku mtandao wa kijamii wa facebook nao ukitajwa kuhusika katika kutawanya taarifa za kuwezesha kutenda makosa hayo.

UFAULU KIDATO CHA 6 JUU

UFAULU katika mtihani wa Kidato cha Sita mwaka jana, umeongezekakwa asilimia 8.13 huku shule za mikoani zisizo na majina makubwa zikichomoza katika orodha ya kumibora.Matokeo hayo yalitangazwa jana naBaraza la Mitihani Tanzania (Necta),huku yakionesha baadhi ya shule kongwe kama vile Tambaza ya jijiniDar es Salaam, zikiwa zimeshika mkia.

Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema katika mtihani huo uliofanyika kati ya Mei5 na 21, mwaka jana, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 8.13 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana.

Jumla ya watahiniwa 38,905 sawa na asilimia 95.98 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu. Mwaka jana wanafunzi waliofaulu walikuwani 44,366 sawa na asilimia 87.85.

Kaimu Katibu Mtendaji alisema wanafunzi waliofaulu, wasichana ni 12,080 sawa na asilimia 97.66 wakati wavulana ni 26,825 sawa na asilimia 95.25.

Shule Bora

Katika matokeo hayo, shule zilizofanya vizuri ni Igowole (Iringa), Feza Boys (Dar es Salaam),Kisimiri (Arusha), Iwawa (Njombe), Kibaha (Pwani), Marian Girls (Pwani) Nangwa (Manyara), Utawa (Mbeya), Kibondo (Kigoma) na Kawawa (Iringa).Ufaulu wa shule hizo umepangwa kwa kutumia kigezo cha wastani wapointi (Grade Point Average – GPA)na mchanganuo kwa kuzingatia idadi ya watahiniwa wasiopungua 30.

Kumi za mwisho

Kwa upande wa shule 10 za mwisho, pamoja na Tambaza, Dk Msonde alizitaja nyingine kuwa ni Ben Bella (Unguja), Fidel Castro (Pemba), Muheza High School (Tanga), Mazizini (Unguja), Mtwara Technical (Mtwara), Iyunga Technical (Mbeya), Al-Falaah Muslim (Unguja), Kaliua (Tabora) naOsward Mang'ombe (Mara).Wanafunzi BoraAkizungumzia walivyopatikana wanafunzi waliofanya vizuri zaidi, Kaimu Katibu Mtendaji huyo wa Necta, alisema waliangalia wastani wa GPA kwenye masomo ya tahasusi pamoja na wastani wa alama za jumla walizopata.Wanafunzi hao waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kitaifa na shule zao kwenye mabano ni Isaack Shayo (St. Joseph Cathedral),Doris Noah (Marian Girls), Innocent Yusufu (Feza Boys), Placidl Pius (Moshi), Benni Shayo (Ilboru), Abubakar Juma (Mzumbe),Mwaminimungu Christopher (Tabora Wavulana), Chigulu Japhaly (Mzumbe), Hussein Parpia (Al-Muntazir Islamic Seminary) na Ramadhani Ally Msangi (Feza Boys).

Kwa upande wa wasichana 10 bora kwa masomo ya sayansi kitaifa, watano wametoka Shule ya Marian.Nao ni Doris Noah, Monica Mtei, Wema Kibanga, Deborah Mlawa na Doreen Kashushura.

Wengine ni Frida Mbilinyi, Gloria Kweka (Msalato), Aisha Mnjovu, Mulhat Said (Feza) na Heavenlight Munis (St Mary Goreth). Wavulana 10 bora kwa masomo ya Sayansi kitaifa na shule zao kwenye mabano ni Isaack Shayo (St Joseph Cathedral), Innocent Yusuf, Ramadhan Msangi (Feza), Placid Pius (Moshi), Benini Shayo (Ilboru),Abubakar Juma (Mzumbe), Mwaminimungu Christopher (Tabora Boys), Chigulu Japhaly (Mzumbe), Hussein Parpia (Al Muntazir Islamic Seminary) na Lusekelo Kihesya (Mpwapwa).

10 bora

Biashara Watahiniwa 10 bora kwa masomo ya Biashara ni Jovina Leonidas (Nganza), Nestory Makendi (Kibaha), Imma Anyandwile (Umbwe), Thersia Marwa na Grace Chelele (Loyola), Betria Rugila (Baobab), Jaqueline Kalinga (Weruweru), Tajiel Kitojo (Arusha), Shiriya Ramaiya (ShaabanRobert) na Mwanaidi Mwazema (Weruweru).

Lugha, Sanaa

Watahiniwa kumi bora wa masomoya Lugha na Sanaa ni Lisa Mimbi (St. Mary Goreth), Rosalyna Tandau(Marian Girls), Joseph Ngobya (St. Joseph Cathedral), Aneth Mtenga na Idda Lawenja (Marian Girls), Edna Mwankenja( Kisimiri), Catherine Kiiza ( St. Mary Mazinde Juu), Nancy Adonswai (Mwika), Mohamed Salmin (Mwanza) na Idrisa Hamisi (Mwembetogwa).

Ubora wa ufaulu

Msonde alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 30,225 sawa na asilimia 85.73 wamefaulu katika madaraja I - III wakiwemo wasichana 9,954 sawa na asilimia 90.59 na wavulana 20,271 sawa na asilimia 83.53.

Daraja kwa Kwanza ni wanafunzi 3,773, wavulana 2,232 na wasichana 1,541, Daraja la Pili ni wanafunzi 9,631ikiwa wavulana ni 6,179 na wasichana 3,452.Daraja la Tatu ni wanafunzi 16,821 ikiwa wavulana ni 11,860 na wasichana 4,961, Daraja la IV: wanafunzi 4,420 ikiwa ni wavulana 3,474 na wasichana 946 na Daraja 0: wanafunzi 612, wavulana wakiwani 524 na wasichana 88.

Ufaulu Kiswahili

Msonde alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo yote 14 ya msingi umepanda ikilinganishwa na mwaka 2013. Ufaulu wa juu kabisa ni ule wa somo la Kiswahili ambao ni asilimia 99.88 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hilo wamefaulu.Alisema ufaulu katika masomo ya Sayansi (Physics, Chemistry, Biology na Advanced Mathematics)umeendelea kuimarika kwa kulinganisha na ufaulu wa masomohayo mwaka 2013.

Gredi za ufauluAlisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni wanafunzi 34,645 sawa na asilimia 98.26 ya waliofanya mtihani, wasichana wakiwa ni 10,900 ambayo ni asilimia 99.2 na wavulana 23,45 sawa na asilimia 97.84.

Mwaka 2013 watahiniwa 40,242 sawa a asilimia 93.92 ya watahiniwa wa shule walifauu mtihani huo. Mtahiniwa anahesabiwa kuwa amefaulu somo kwa kupata angalau gredi D (alama 30) katika somo husika.Hivyo, kiwango cha juu cha ufaulu katika somo ni gredi A na cha chinikatika somo ni Gredi D. "Ufaulu katika gredi A, B+, B na C utakuwa ni Principal Pass," alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Necta.Kulingana na mpangilio huo, Daraja la Kwanza ni poiti 3-7, la Pili8-9, Tatu 10-13 na Daraja la Nne mtahiniwa atakuwa amefaulu kwa kuwa na angalau D mbili au principal pass moja.Aliyepata Sifuri ni aliyepata ufaulu chini ya D mbili. Uzito wa alama katika Gredi; A=1, B+= 2, B=3, C=4, D=5, E=6 na F=7.

Watahiniwa wa Kujitegemea Alisema watahiniwa wa Kujitegemea waliofaulu ni 4,260 sawa na asilimia 80.73 ya watahiniwa 5,277 waliofanya mtihani.Mwaka 2013 watahiniwa wa kujitegemea 4,124 sawa na asilimia 53.87 walifaulu mtihani huo. Msonde alisema Baraza limezuia matokeo ya watahiniwa 150 wa shule ambao hawajalipa ada ya mtihani hadi watakapolipa, watahiniwa tisa waliopata matatizo ya kiafya."Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa katika Mtihani wa Kidato cha Sita Mei, 2015.

Alisema watahiniwa 29 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote. Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya Mtihani wa Kidato cha Sita Mei, 2015.

Msonde alisema Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa wawiliwaliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani. Matokeo Ualimu Katika hatua nyingine, matokeo ya walimu waliofanya mtihani mwaka 2014 yanaonesha watahiniwa katika ngazi ya Cheti, Stashahada na Stashahada ya Ualimu Ufundi, hakuna mwanafunzi aliyepata alama za juu.Dk Msonde alisema watahiniwa 4,161 sawa na asilimia 85.71 ya watahiniwa 4,899 waliofanya mtihani wa Stashahada ya Ualimu mwaka 2014 wamefaulu.Kati ya watahiniwa hao, wasichana ni 1,401 sawa na asilimia 83.64 na wavulana 2,760 sawa na asilimia 86.79.Alisema katika hao waliofaulu, hakuna aliyepata daraja la juu (distiction). Waliopata daraja la credit ni watano, pass 4,156, wanaorudia mtihani ni 658 na waliofeli ni 36.Akizungumzia matokeo ya mtihani wa Stashahada ya Ualimu Ufundi, Msonde alisema "watahiniwa wote watatu waliofanya Mtihani wa Stashahada ya Ualimu Ufundi wameshindwa baadhi ya masomo, hivyo watarudia masomo waliyoshindwa katika Mtihani wa Mei 2015.

Bofya hapa Kuangalia matokeo http://www.necta.go.tz/matokeo2014/ACSEE.htm

WEZI WA CHUMA WAIBA RELI

Sehemu ya njia ya reli iliyoibwa


Wezi wa chuma nchini Afrika Kusini wameiba karibu kilomita kumi za chuma kwenye njia ya reli na kusababisha uharibifu wa thamani ya dola milioni 2.3.
Sehemu kubwa ya chuma ya reli imeibwa katika muda wa miezi michache iliyopita. Njia hiyo ya reli hutumiwa na magari ya moshi kutoka mjini Johannesburg kwenda mjini Nigel. Taarifa hii ni kwa mujibu wa jarida la The Star.
Watu watano wamefikishwa mahakamani baada ya kukamatwa na walinzi ambao hushika doria katika sehemu hiyo wakiibaa chuma hiyo.
"ni wataalamu wa kuiba hao. Hakuna dalili ya wao kukosea hata kidogo,'' asema Thumbu Mahlangu,mwanakamati ya usafiri.
Msemaji wa usafiri wa reli Mike Asefovitz anakubaliana na hilo.
''Hawa wezi sio watu wadogo. Chuma hizi huwa ni nzito na kuweza kuzing'oa unahitaji mashine kubwa.''

Chuma hizo zina thamani ya dola 120,000 katika soko la vyuma kuu kuu.
Wizi huo umesababisha mabehewa mapya 34 kuegeshwa tu katika kiwanda kwani hazina pa kutumiwa. Kiwanda hicho sasa kinahofia watu zaidi ya 700 huenda wakapoteza kazi zao.
Nchini Afrika Kusini wizi wa vyuma ni tatizo kubwa sana kiasi cha kuleta hasara ya mamilioni ya dola kwa uchumi wa nchi.

JELA KWA KUMTUMIA OBAMA BARUA YENYE SUMU

Richardson ameigiza katika vipindi vya 'The Vampire Diaries' na 'The Walking Dead.


Muigizaji mwanamke nchini Marekani aliyemtumia Rais Barack Obama barua iliyokuwa na sumu ya Ricin amefungwa jela kwa miaka 18.
Shannon Richardson, mwenye umri wa miaka 36, kutoka Texas, pia alimtumia meya wa New York Michael Bloomburg barua nyingine iliyokuwa na sumu hiyo hiyo.
Alidai kuwa mumewe waliyeachana naye ndiye alituma barua hizo katika njama ya kumlimbikizia madai hayo.
"sikuwa na nia ya kumdhuru mtu, '' Shannon aliambia mahakama.
Alikiri kosa la kumiliki na kutengeza sumu hiyo mwezi Disemba.

Jaji alimpa hukumu kubwa zaidi ikilinganishwa na kosa lake na pia kutakiwa kulipa faini ya dola 367,000.
Richardson, mama mwenye watoto sita, ameigiza katika vipindi kama 'The Vampire Diaries' na 'The Walking Dead.'
Viongozi wa mashitaka wanasema kuwa mwanamke huyo aliagiza bidhaa za kutengeza sumu hiyo kupitia kwa mtandao kisha akatuma barua tatu zilizokuwa zimepakwa sumu hiyo.
Shannon mwenye watoto sita aliomba mahakama kumhurumia kwa kumpa adhabu ndogo


Kulingana na viongozi wa mashitaka, moja ya barua alizomtumia Obama , ilikuwa na maandihsi haya: "kilicho ndani ya barua hii, hakiwezi kulinganishwa na mipango yangu kwako bwana Rais. ''
Barua nyingine iliyopokewa na meya Bloomberg, anayeunga mkono kudhibitiwa kwa bunduki, ilisema, '' mpige risasi mtu yeyote atayekuja kuchukua bunduki za mtu aliyetuma barua hii.''
Barua ya tatu iliyokuwa na kemikali hiyo ya sumu, ilifunguliwa na bwana Mark Glaze, mkurugenzi mkuu wa idara inayofadhiliwa na Meya ya kupambana na silaha haramu.
Richardson katika kumtaka jaji kumhurumia, aliomba msamaha akisema, '' mimi sio mtu mbaya. Sina nia ya kumdhuru mtu yeyote.

Aliomba msamaha na huruma na kusema tayari anahisi ameadhibiwa vya kutosha kwa kunyang'anywa watoto wake sita

ISRAEL NA HAMAS WAKUBALIANA KUSITISHA MASHAMBULIZI KWA MUDA

Vuguvugu la kupigania Uhuru wa Palestina, Hamas, na Israel zimekubali kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza kwa muda wa saa tano baadaye hivi leo baada ya siku tano za mapigano makali.


Baada ya ombi la umoja wa mataifa jeshi la Israel limesema kuwa litasitisha mashambulizi kati ya saa nneasubuhi hadi saa tisa kwa saaza Gaza, ili kuwaruhusu wakaazi kupata chakula na huduma muhimu.

Msemaji wa Hamas Sami AbuZukhri amethibitisha kuwa vuguvugu hilo kadhalika litasitisha mashambulizi ya roketi dhidi ya Israel wakati huo.


Msemaji wa shirika la umoja wa mataifa linalowasaidia wakimbizi wa Palestina Christopher Gunnes amesema kuwa ni matumainiyake kwamba usitishaji huo wa mapigano utatoa fursa ya kusuluhisha matatizo yanayoikabili gaza.

Hapo jana jumatano jazba zilizidi pale watoto wanne wa kipalestina wote kutoka familia moja waliuwawa katika shambulizi la mizinga kutoka Israel wakati wakicheza kwenye ufuo wa bahari huko Gaza.


Israel imesema ilikuwa ikiwalenga wapiganaji wa Hamas na kwamba vifo hivyo ni matokeo ya mkasa mkubwa wa mapigano hayo.

Naye rais wa Marekani Barrack Obama amesisitiza kuwa Israel ina haki ya kujilinda.

WANASAYANSI WAELEZA FAIDA ZA 'USHUZI'

Wanasayansi katika chuo kikuu cha Exeter, nchini Uingereza, wanasema kuwa wamegundua harufu mbaya kama vile ya kujamba japo inachukiza kwa pua, ina manufaa makubwa kwa afya ya binadamu


Wanasayansi hao wanasema kuwa harufu hiyo mbaya inaweza kuwa kinga dhidi ya magonjwa ya moyo na akili na hata Saratani, Gesi au harufu mbaya ambayo hutokana na chakula kinachosagwa tumboni mwako inaweza kulinda baadhi ya viungo vya mwili wako.

Ndio! athari ni kile ambacho unakidhania: Eti watu wanauchukulia utafiti huu kumaanisha kuwa harufu mbaya inayotokana na mtu kujamba inaweza kuzuia magonjwa fulani mwilini kama vile saratani.


Utafiti huo uliochapishwa katika mtandao wa chuo kikuu cha Exter uligundua kuwa gesi hiyo inayojulikana kama Hydrogen Sulfide ambayo pia hupatikana katika Mayai yaliyooza, inaweza kuwa muhimu katika kutibu baadhi ya magonjwa.

"Ingawa gesi ya hydrogen sulfide inajulikana kuwa na harufu mbaya na hupatikana katika Mayai yaliyooza pamoja na harufu ya mtu kujamba, hutengenezwa mwilini na inaweza kuwa kana tiba kwa magonjwa fulani," alisema daktari Mark Wood, profesa wachuo hicho cha Exeter.


Hata hivyo gesi hiyo ina athari mbaya ikiwa katika viwango vikubwa , kwa mujibu wa utafiti huo

Watafiti wanasema licha ya harufu hiyo mbaya ya kujamba kuchukiza, ina uwezo mkubwa wa kupunguza uwezekenano wa mtu kupatwa na magonjwa kama vile, saratani, kiharusi, mshtuko wa moyo na kuumwa na mifupa.

ASKARI WA JWTZ AFARIKI MAZOEZINI MLIMA KILIMANJARO

Ofisa mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) amefariki dunia na mwingine amesagika mguu baada ya mawe kuporomoka wakati wakipanda Mlima Kilimanjaro katika mazoezi.


Wanajeshi hao ni miongoni mwa maofisa 263 wa JWTZ waliopanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika kwa makundi kuanzia Julai 12, mwaka huu kupitia njia ya Rongai iliyopo wilayani Hai.

Habari za uhakika zilizopatikana jana zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 10:00 alfajiri katika urefu wa mita 5,000 kutoka usawa wa bahari wakati maofisa hao wakitoka eneo la Hans Meyer wakikaribia kilele cha Gilmans.


Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Erastus Lufungulo alilithibitisha kutokea kwa maafa hayo na kueleza kuwa mawe hayo yaliporomoka kutoka juu ya Hans Meyer na kushuka hadi eneo la Jamaica.


Aliyefariki dunia katika ajali hiyo wametajwa kuwa ni Cadet MT 104948 Malata Thomas Kitene (26) baada ya kupata majeraha ya kichwa na Cadet MT 105896 Gabriel Makenge (32) ambaye amevunjika na kusagika mguu wa kushoto.


"Baada ya kupata taarifa za tukio hilo, kikosi chetu cha uokoaji kilikwenda eneo la tukio na kushiriki kazi ya uokoaji, lakini taarifa zaidi kuhusu ziara ya maofisa hao mnaweza kupata kwa wasemaji wa JWTZ," alisema.

Hata hivyo, msemaji wa JWTZ, MejaErick Komba hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.


Majeruhi pamoja na maiti ya ofisa hao waliteremshwa kutoka kileleni jana saa 4:00 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mjini Moshi.

Taarifa zaidi zilisema maofisa hao walipanda mlima huo ikiwa ni utaratibu wa kila mwaka kwa ajili ya mazoezi ya ukakamavu.