MWANAJESHI ALIYEUAWA NA M23 AAGWA.

JESHI la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ),
limeleezea namna
mwanajeshi wake, Meja
Khatibu Shaaban Mshindo,
alivyouawa baada ya
kuangukiwa na bomu,
wakati akiwa katika jukumu
la ulinzi wa amani nchini
Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC).

Pamoja na hayo,
Watanzania wametakiwa
kuimarisha mshikamano
na kuachana na makundi
yenye nia ya kuleta
mgawanyiko, hasa katika
kipindi hiki kigumu
ambacho Tanzania
imepoteza askari wake
waliopewa dhamana ya
kitaifa ya ulinzi wa amani
katika nchi zenye migogoro
Afrika.

Akitoa salamu za
rambirambi wakati askari
huyo wa kikosi cha Mizinga
namba 83 KJ kilichopo
Kibaha akiagwa rasmi
kijeshi Dar es Salaam jana,
Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi, Jenerali Davis
Mwamnyange, alisema
askari huyo pamoja na
askari watano wa
Tanzania, waliangukiwa na
bomu hilo na kujeruhiwa
vibaya.

“Waliangukiwa na bomu
Agosti 28, mwaka huu
huko Goma DRC eneo
walilokuwa wakifanyia
kazi… Meja Mshindo
aliumia vibaya na kukutwa
na mauti njiani akipelekwa
hospitalini,” alisema
Jenerali Mwamunyange.
Alisema katika tukio hilo,
askari wengine watano wa
Tanzania walijeruhiwa
vibaya na wanaendelea
vizuri na matibabu nchini
humo na hali zao
zinaendelea vizuri.

Akimzungumzia Meja
Mshindo, Jenerali
Mwamunyange alisema
katika uhai wake alikuwa
mchapakazi, muaminifu,
hodari na mtiifu na kifo
chake kimetokea wakati
jeshi linamhitaji.

“Kifo chake kimeacha
pengo ndani ya JWTZ na
itachukua muda mrefu
kuziba pengo hili.” Waziri
wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, alisema
kifo cha askari huyo ni
msiba wa kitaifa na
kumtaja Meja Mshindo
kuwa shujaa aliyekutwa na
mauti wakati akitekeleza
kazi aliyotumwa na nchi
yake.

Alisema kifo hicho pamoja
na vifo vya askari wengine
saba wa JWTZ vilivyotokea
Darfur mwaka huu, ni
chachu kwa Tanzania
kuendeleza jitihada za
kusaidia nchi zenye
migogoro na kuhamasisha
amani Afrika.

“Serikali inapata
matumaini namna
Watanzania walivyosimama
pamoja na kuunga mkono
jeshi letu katika kipindi
hiki kigumu. Ingekuwa nchi
nyingine, haya yaliyotokea
yangeleta mgawanyiko
mkubwa miongoni mwa
raia, lakini kwa hapa kwetu
hali imekuwa tofauti,”
alisema Membe.

Aliwataka wachache wenye
mawazo ya kutumia
matukio hayo kuwagawa
Watanzania, waache mara
moja nia yao hiyo, kwa
kuwa moja ya kazi ambayo
Tanzania inayo, ni pamoja
na nia yake ya
kuhamasisha na kutangaza
amani Afrika na dunia kwa
ujumla.

“Jamani wajibu wetu ni
kuhakikisha haya maeneo
yenye migogoro yanakuwa
na amani, kule DRC hali ni
mbaya, watu wanakufa kila
kukicha na akinamama na
watoto wanabakwa na
kudhalilishwa, sasa sisi
kama taifa ni vyema
kujitokeza na kusaidia
wenzetu,” alisisitiza.

Meja mshindo, alizikwa
jana nyumbani kwao Fujoni
Zanzibar na ameacha mke
mmoja, Hawa Mnimbo na
watoto watatu ambao ni
Shaaban, Abuu na Samir
Mshindo