UNHCR - TANZANIA HAIJAWAFUKUZA WAKIMBIZI

Shirika la Umoja wa Mataifa
la Kuhudumia Wakimbizi,
UNHCR, ofisi ya Tanzania
limekanusha taarifa katika
baadhi ya vyombo vya
habari kwamba, Tanzania
imewarejesha nyumbani
kwa nguvu, wakimbizi
25,000 wa Burundi mwezi
mmoja uliopita.
)
Vilevile serikali ya Tanzania
imesema, taarifa hiyo ni ya
uzushi ambayo haina ukweli
wowote na yenye nia ya
kuichafulia jina nchi ya
Tanzania ambayo kwa muda
mrefu imekuwa kimbilio na
makaazi ya wakimbizi wengi
kutoka nchi mbalimbali
hasa za Ukanda wa Maziwa
Makuu.

Akizungumza na BBC,
Mwakilishi Mkazi wa UNHCR
nchini Tanzania , Bi. Joyce
Mends Cole, amesema,
amewasiliana na mwakilishi
wa shirika hilo nchini
Burundi ambaye
amethibitisha kwamba
hakuna wakimbizi wa nchi
hiyo waliorejeshwa kutoka
Tanzania.

Bi. Joyce amebainisha kuwa,
tatizo lililopo ni
kuchanganywa kwa maneno
"Wakimbizi" na "Wahamiaji
Haramu".

Amefafanua kwamba, katika
operesheni inayoendelea
kwa sasa nchini Tanzania,
ya kuwasaka wahamiaji
haramu huenda baadhi ya
wakimbizi waliosalia
wamekamatwa kimakosa.

Hata hivyo Waziri wa
Mambo ya Ndani wa
Tanzania Dk. Emmanuel
Nchimbi, alimuhakikishia
kuwa operesheni hiyo
inafanyika kwa umakini
mkubwa na kwa kuzingatia
mikataba ya kimataifa ya
haki za uhamiaji.

Katika hatua nyingine,
serikali ya Tanzania kupitia
Msemaji wa Wizara ya
Mambo ya Ndani, Bw. Isaack
Nantanga, imesema hakuna
mkimbizi yeyote
aliyerejeshwa Burundi kwa
hiari wala kwa nguvu katika
kipindi kilichotajwa.

Bw. Nantanga amebainisha
kuwa, wakimbizi wote
264,000 ambao Tanzania
imewapatia "Hifadhi ya
Ukimbizi" wapo na
wanaendelea kuishi kwenye
kambi na makazi ya
wakimbizi yaliyopo katika
mikoa ya Tabora, Kigoma,
Katavi na Tanga.

Wakimbizi hao wanatoka
katika nchi za Burundi,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, DRC, na Somalia.

Hadi Septemba nne mwaka
huu, zaidi ya "Wahamiaji
Haramu" 27,000
wamerejeshwa makwao kwa
hiari ambao walikuwa
wakiishi nchini Tanzania
kinyume cha sheria katika
mikoa ya Rukwa, Kigoma na
Kagera