NDUGU WAKWARUZANA KUGOMBEA MWILI WA MAREHEMU HUKO ITENKA

NDUGU wamefarakana
wakigombea mwili wa
marehemu, Philipo
Sigare (32) aliyekuwa
Ofisa Mtendaji wa Kijiji
cha Itenka. Hali hiyo
imesababisha msiba
kuwekwa sehemu mbili
tofauti kwa wakati
mmoja mjini Mpanda
Mkoa wa Katavi. Ofisa
huyo alifariki
Septemba 9 , mwaka
huu.

Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Katavi,
Dhahiri Kidavashari
alisema ilibidi aingilie
kati, kunusuru mzozo
huo katika chumba cha
kuhifadhia maiti,
ambako kila upande
ulitaka uchukue mwili.

Mzozo huo ulivuta
hisia za wakazi mjini
Mpanda baada ya
pande zinazopingana
kwenda katika chumba
cha kuhifadhia maiti
katika Hospitali ya
Wilaya mjini Mpanda,
ambako mwili
umehifadhiwa,
wakitaka kuuchukua
kwenda kuuzika.

“Nimewaasa
wanafamilia hao kama
watashindwa
kuelewana, basi
waende mahakamani
ambako ufumbuzi wa
mgogoro huo
utapatikana,” alisema
Kamanda Kidavashari.

Baadhi ya ndugu
walidai maziko
yameshindikana,
kutokana na mzozo
huo na kwamba baadhi
yao wanajipanga
kupeleka shauri hilo
mahakamani ili haki
iweze kutendeka.

“Pande mbili zilikutana
hapo hospitalini na
kuanza kutupiana
maneno makali ya
kashfa, wakidai kuwa
ndugu wa upande wa
Thobias wanataka
kuchukua msiba ili
waweze kula pesa za
rambirambi,” alisema
mmoja wa mashuhuda.

Chanzo cha mzozo huo
inadaiwa ni kutokana
na baadhi ya ndugu
kutaka maziko yasubiri
kaka mkubwa wa
marehemu, Mathias
Sigareti ambaye ni
Mwalimu wa Shule ya
Msingi kijijini Kasanga
atakapowasili huku
wengine wakipinga.

Miongoni mwa ndugu
waliopinga hilo, ni
Thobias Kizimzuri
aliyeamua kuweka
msiba nyumbani kwake
katika Mtaa wa
Makanyagio mjini
Mpanda, akidai yeye
ndiye aliyekuwa
akimhudumia mgonjwa
wakati wote alipokuwa
amelazwa hospitalini
kwa matibabu.

Wakati huo huo dada
yake Thobias, aitwaye
Magreti Francis
alipinga uamuzi wa
kaka yake, pia akaamua
msiba uwe nyumbani
kwake Mtaa wa
Majengo.

Kutokana na
mkanganyiko huo,
waombolezaji
walijikuta
wakigawanyika katika
nyumba hizo huku kila
upande ukifanya
maandalizi ya maziko.

Hata baada ya kaka
mkubwa aliyekuwa
akisubiriwa kuwasili,
iliamriwa msiba ubaki
kwa dada yao Magreth,
Mtaa wa Majengo,
lakini uamuzi huo
ulipingwa.

Kila upande uliendelea
na taratibu za
kuchimba kaburi katika
maeneo tofauti kwenye
makaburi ya Mwangaza
mjini Mpanda, kabla ya
kwenda chumba cha
maiti kuchukua mwili.

Hali hiyo ilisababisha
mzozo mkali ambao
Kamanda wa Polisi
akiwa na kundi la
askari, walifika na
kuingilia kati.