RAIS KIKWETE AMALIZA ZIARA YAKE JIJINI MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Jakaya Kikwete ameitaka mikoa nchini kuwa na mipango ya uanzishwaji viwanda jambo ambalo litasaidia kuinua maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo.

Kauli hiyo ya Rais ameitoa katika majumuisho ya ziara yake ya siku sita mkoani Mwanza baada ya kutembelea wilaya zote na kujionea shughuli mbalimbali za maendeleo.

Mwanza unatajwa kuwa mkoa wa pili Tanzania katika kuchangia pato la Taifa kwa mwaka ambapo unachangia zaidi ya asilimia 12 ukitanguliwa na Dar es Salaam.

Rais anashangaa kuona mkoa huu hauna mipango ya kuongeza viwanda kutokana na ukweli kuwa wakazi wa mijini wanategemea ajira katika kuendesha maisha yao.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa ni maarufukwa kulima zao la Pamba licha ya zao hili nchini kushuka thamani katika soko la kimataifa hivi karibuni.

Mfumo wa kilimo cha Mkataba unasuasua, Rais anawanyooshea kidole baadhi ya wanunuzi kwa kuwa kikwazo katika kuboresha kilimo hicho kwa kiasi kikubwa.

Katika maelezo yake Mheshimiwa Rais anahimiza kilimo cha matunda, mboga mboga na Maua kwenye ukanda huu wa ziwa hatua itakayowezesha kuwa na masoko katika nchi za Ulaya.

Katika ziara yake mkoani Mwanza Rais Kikwete amezindua na kuwekamawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya nishati ya umeme, maji, afya na kilimo.