MTANZANIA MWINGINE ADAKWA DUBAI

Kwa wiki iliyopita, tuilipekenyua maeneo yote muhimu na kukumbana na mambo mapya kuhusu habari za‘unga’huku taarifa zikionesha kuwa, hali katika viwanja vye ndege duniani kote ni tete. Tuhuma za Watanzania kukamatwa au kufariki kutokana na madawa ya kulevya bado zinaendelea kuongezeka. Kwenye hii thread kuna tuhuma tatu zinazowahusu Watanzania, mmoja inadaiwa amefariki baada ya mzigo kupasukia tumboni na wengine wawili wanadaiwa kukamatwa kwenye nchi za watu wakiwa na mzigo.
Mtanzania afia Dubai akiwa na unga tumboni
Habari zilizotufikia juzi zinadai kwamba Mtanzania aliyejulikana kwa jina moja la Chambuso amefariki dunia katika Jiji la Dubai, Falme za Kiarabu kutokana na unga aliokuwa ameubeba tumboni kuyeyuka kabla ya kufika kwenye kituo husika. Habari za uhakika kutoka chanzo chetu jijini Dar zinasema kuwa marehemu Chambuso alikuwa na‘mlinzi’wake ndani ya Ndege ya Emirate huku akiwa hamjui.
Ikazidi kudaiwa kuwa, baada ya kushuka jijini Dubai, hali ya Chambuso ilianza kubadilika akilalamikia zaidi maumivu ya tumbo, ndipo‘mlinzi’huyo alipombeba na kumpeleka hospitali (haikutajwa jina).“Baada ya kufariki dunia, jamaa (mlinzi) alijiweka mbele akitaka kufanya maarifa kwa madaktari ili tumbo la jamaa lipasuliwe atoe mzigo. Akashtukiwa, akakimbia na mpaka sasa maiti hiyo iko chini ya ulinzi wa serikali,”kilisema chanzo hicho.
Mtanzania aliyekamatwa na unga China
Tukiachana na kifo cha Chambuso huko Dubai, Septemba 2, mwaka huu zilitufikia taarifa kwamba, mchumba wa mwigizaji Pendo Mushi‘Pendo wa Maisha Plus’aliyejulikana kwa jina moja la Tasha amedakwa na unga nchini China. Kwa mujibu wa taarifa hizo, Tasha alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing nchini humo akiwa na unga aina ya heroin (kiasi na thamani hakikutajwa).
Ili kupata uhakika wa madai hayo, juzi Ijumaa Wikienda lilimtafuta Pendo kwa njia ya simu ya mkononi na kumuuliza kuhusu madai hayo ambapo alikiri.“Yeah, ishu ni kweli. Mimi nilizipata hizo taarifa kutoka kule nikawaambia ndugu zake. Kwa mujibu wa mtu wake aliyekuwa naye kule (China) jamaa (Tasha) ameshapandishwa kortini,”alisema Pendo huku akisema uchumba wake na Tasha ulishakufa.
Msanii wa Bongo Movie adaiwa kufungwa Brazil
Wiki mbili sasa, mapaparazi wetu wamekuwa wakifuatilia kwa undani kuhusu kusambaa kwa madai kwamba, staa wa filamu za Kibongo, Aisha Bui eti kafungwa miaka 5 jela katika gereza moja nchini Brazil baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya kwenye kibegi. Kwa mujibu wa madai ya habari hizo, eti Aisha alidakwa kwenye uwanja wa ndege wa jijini Brasilia akirejea Bongo kupitia Dubai.
Septemba 2 na 5, mwaka huu, waandishi wetu walifika nyumbani kwa baba wa Aisha, Kigamboni, Dar kutaka kujua ukweli. Septemba 2, mtu aliyekutwa nyumbani hapo alisema Aisha yupo Brazil lakini hakuna mawasiliano naye na alikwenda siku chache kabla ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Julai mwaka huu. Septemba 5, hakukutwa mtu ila majirani walielekeza eneo analopatikana mzee huyo ambapo ni ufukweni. Hata hivyo, sehemu hiyo hakupatikana na waandiishi waliacha namba zao za simu.
Jioni, mzee Bui alizipata namba zilizoachwa, na saa 9:00 usiku wa kuamkia Septemba 6 alimpigia simu mwandishi wetu na kumvurumishia matusi huku akisema akome kumfuatafuata akidai yeye hana mawasiliano na binti yake tangu mwaka 2007. Mzee huyo alikwenda mbele zaidi kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu (SMS) kwenye simu ya paparazi akitumia lugha ya Kiarabu ambapo kwa mujibu wa wataalam wa lugha hiyo ni dua ya kumwombea mabaya mwandishi huyo.
Mnaigeria aliyekamatwa na unga alitahadharishwa na wenyeji wake magomeni asipitie JNIA.
Anthonie Ojo, raia wa Nigeria aliyekamatwa Septemba 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar (JNIA), akijaribu kusafirisha kete 99 za unga na ndege ya Shirika la Ethiopian Airways alinaswa. Mwanamke huyo aliyevalia baibui akidai anakwenda kuhiji Maka, anadaiwa aliununua mzigo huo Magomeni-Mapipa jijini Dar. Aliziweka kete hizo kwenye makopo yaliyokuwa na poda ya Johnson.
Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, wenyeji waliomuuzia unga mwanamke huyo walimtahadharisha kuhusu hali ya ulinzi iliyopo sasa JNIA hasa baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kushikia bango udhibiti wa unga lakini mtuhumiwa huyo alidaiwa kusema atapita kwa anavyojua yeye.
Nzowa azungumzia
Ili kwenda mbele zaidi, mapaparazi wetu walikwenda ofisini kwa Kamanda wa Kikosi Maalum cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa ili kutaka kujua kama amesikia lolote kuhusu Aisha Bui. Alisema:"Eee, kuna habari kama hiyo lakini si rasmi kwangu, bado nafuatilia Brazil ikiwa tayari nitawajulisha tu."Tulimtafuta Aisha kwenye mitandao, hasa Facebook, Instagram na Twitter bila mafanikio. Tumemwachia ujumbe kwa kuamini kwamba akirudi hewani ataukuta na kujibu lakini wapi!