WANAFUNZI WALIPULIWA NA BOMU

Taarifa kwa mujibu wa
ITV — Wanafunzi wawili
wa kidato cha kwanza
katika shule ya
sekondari Matombo
katika wilaya ya
Morogoro
wamejeruhiwa, baada ya
kulipukiwa na kitu
kinachosadikiwa kuwa ni
bomu, wakati wakitoka
shuleni.
Wanafunzi hao
waliojeruhiwa katika
sehemu mbalimbali za
miili yao ni Luciani
Juma (14) na Anthonia
Charles (15), wakazi wa
kijiji cha Konde, Tarafa
ya Matombo wilayani
Morogoro, ambapo
Luciani aliyelazwa katika
hospitali ya rufaa ya
mkoa wa Morogoro kwa
matibabu, ameiambia
ITV kuwa walikumbwa
na tukio hilo wakati
wakitokea shuleni,
ambapo njiani
walikutana na kitu
mfano wa balbu ya tochi
ambacho hata asubuhi
wakati wa kwenda shule
walikiona na kukipuuza,
ndipo mmoja
wawanafunzi alikirushia
ganda la muwa aliokuwa
akila, na kililipuka na
kutoa mshindo mkubwa.
Daktari anayemtibu
Lucien katika wadi
namba moja ya hospitali
ya rufaa ya mkoa wa
Morogoro, aliyejulikana
kwa jina moja Dk.
Francis amesema
majeruhi huyo
anaendelea vizuri, na
amepata majeraha katika
sehemu mbalimbali za
mwili wake ikiwemo
sehemu za siri, kwenye
paja na sehemu ya
nyonga na kwamba
katika maeneo hayo
walifanikiwa kutoa vitu
mfano wa chuma.
Kaimu kamanda wa
polisi mkoa wa Morogoro
John Laswai,
amethibitisha
kujeruhiwa kwa
wanafunzi hao, ambapo
majeruhi Anthonia
ametibiwa na
kuruhusiwa na kwamba
polisi wanaendelea na
uchunguzi zaidi kubaini
kitu kilichowajeruhi
wanafunzi hao, ambacho
kilitoa mshindo mkubwa
na mtawanyiko wa
vyuma, kama kilikuwa
ni bomu ama
vinginevyo.