UN YAIKOSOA TANZANIA KWA KUWARUDISHA MAKWAO WAHAMIAJI

Umoja wa Mataifa umesema
kuwa takriban wahamiaji
haramu elfu 25 kutoka
Burundi wameondoshwa
Tanzania kwa nguvu katika
mwezi mmoja uliopita.

Afisa wa shirika la Umoja
wa Mataifa la kuwahudumia
wakimbizi UNHCR amesema
malori yanayowasafirisha
warundi yamekuwa yakivuka
mpaka kila siku , huku
wahamiaji haramu wengi
wakikosa mahitaji muhimu
kama vile maji na chakula
Katika wiki za hivi karibuni,
Tanzania imekuwa
ikiwarejesha makwao kwa
nguvu wale walioelezwa
wahamiaji haramu kutoka
Burundi, Rwanda na
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya
Congo.

Kwa miaka mingi Tanzania
iliwahifadhi mamilioni ya
wakimbizi waliokuwa
wakiyakimbia mapigano
katika nchi jirani.

Takriban watu milioni moja
walitoroka kutoka Burundi
na kuingia Tanzania wakati
wa mgogoro wa wenyewe
kwa wenyewe wakati vita
vilipozuka mwaka 1993.

Wengi walirejea kwa hiari
wakati amani ilipopatikana
mwaka 2006.

Nchi hiyo imekuwa makao
kwa mamilioni ya wakimbizi
katika kipindi cha zaidi ya
miaka kumi iliyopita
kutokana na migogoro
katika eneo la maziwa
makuu.

Maafisa wa Tanzania sasa
wameanza kutekeleza amri
ya kuwaondoa kwa nguvu
wale wanaodaiwa kuwa
wahamiaji haramu kutoka
Burundi, Rwanda, na
Jamuhuri ya kidemokrasia
ya Congo.

Shughuli hii imetokea
wakati mmoja na mgogoro
wa kidiplomasia kati ya
Tanzania na Rwanda
ambayo imekuwa ikikanusha
madai ya kuchochea vurugu
katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.

Mgogoro ndani ya Jamhuri
ya kidemokrasia ya Congo
nao unaendelea kuchochea
idadi ya wakimbizi
wanaotoroka vita na kuingia
katika nchi jirani.