CHADEMA YAMSHITAKI BALOZI WA CHINA NCHINI.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemshtaki Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youging kwa Umoja wa Mataifa (UN) kwa kujihusisha na siasa katuika majukwaa nchini kitendo ambacho ni hatari katika uhusiano wa diplomasia kati ya Tanzania na China.

Pia kimemshtaki kwa Serikali ya China na ya Tanzania kikidai kitendo cha balozi huyo ni kukiuka Mkataba wa Kidiplomasia wa Vienna (Vienna Convention of Diplomatic Reletions of 1964 ibara ya 41 (1-3) ambao unasimamia sheria za nchi wanachama w Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chadema, Ezekiel Wenje alisema kitendo cha Balozi wa China, Dk. Youging kujihusisha na siasa za uenezi katika Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kosa kubwa kimataifa na amepoteza sifa za kushikilia nafasi hiyo.

Wenje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) na Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alisema balozi huyo amevunja sheria za Mkataba wa Vienna ambao unasimamia sheria za nchi wanachama wa UN.

Alisema kifungu alichovunja kinakataza Balozi yeyote kujihusisha na shughuli nyingine ambazo haziendani na majukumu ya uwakilishi wa nchi na nchi.

Wenje alisema balozi huyo anapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kama inavyoelekezwa katika mkataba wa Vienna kwamba ikiwa balozi atakiuka mkataba huo atakosa sifa na ataondolewa kinga aliyonayo na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Alisema: "Jambo hili katika macho ya diplomasia, limevunja misingi na taratibu za ushirikiano wa kimataifa, wenye nia njema kwa wananchi wa pande mbili, baina ya nchi na nchi na katika ngazi ya serikali.

"Kwanza ni taswira ya dharau ya hali ya juu ambayo Balozi wa China ameamua kuwaonyesha Watanzania, hatuamini kwamba amepungukiwa na uwezo kiasi gani lakini anapaswa kukumbushwa aweze kuheshimu mipaka ya majukumu na wajibu wa diplomasia kwa nafsi ya balozi anapokuwa nchi ya ugenini.

"Balozi huyu anapaswa kukumbushwa kuwa uhusiano wa vyama, kwa maana ya Chama cha Kikomunisti cha China na CCM hata kama ungekuwa mzuri kiasi gani hauna mwingiliano na uhusiano wa Serikali ya Tanznaia na China.


"Hatutaki kuamini kuwa serikali ya China imemtuma Balozi Youquing kuja nchini kufanya kazi za ukatibu mwenezi wa CCM, tumesikitishwa heshima aliyopewa na Watu wa China ameidharau na amevuka mstari ambao hakuna mwanadiplomasia yeyote makini anayeheshimu uhusiano baina ya nchi na nchi angejaribu kufanya hivyo.

"Mstari aliouvuka balozi huyu umefafanuliwa wazi katika Mkataba wa Vienna Convention wa 1961 hasa katika kifungu cha 41(1) na 3, katika masuala yanayohusu uhusiano na kinga za mabalozi, kwamba ni marufuku kwa mwanadiplomasia yeyote kuingilia siasa za ndani za nchi mwenyeji wake.

"Chadema tunachukua hatua dhidi ya balozi huyo kujihusisha na chama cha siasa kwa kuvaa kofia ya CCM na kuelezea mambo ambayo hayakupaswa kusemwa kwenye majukwaa ya siasa.

"Kwanza tunaandika barua tatu, moja itakwenda Serikali ya China, ya pili itakwenda UN na nyingine itakwenda Serikali ya CCM ambayo ndiyo imempeleka huko mikoani.

"Barua hizo zitakuwa zinataka kueleza msimamo wa tukio hilo la balozi wa China nchini kujihusisha na siasa za majukwaani na kuvaa nguo za CCM, tunataka kujua hatua gani zitakazochukuliwa haraka kabla ya Chadema hatujapendekeza hatua za kuchukua.


"Hii ni hatari kwa balozi huyo kujiingiza kwenye siasa kitendo kinachosababisha kuhatarisha uhusiano uliopo kati ya wawekezaji wa China nchini kwa sababu wananchi wanaweza kutafsiri vibaya.

"Kwa mfano kuna maeneo ni ngome za Chadema na pale kuna wawekezaji wa China wanaweza kukataa kutoa ushirikiano wakidai ni wapo mlengwa wa CCM, pia ni hatari chama kingine kitapokuja kushika dola hakutakuwa na uhusiano mzuri.

"Tutaambatanisha ushahidi wa kutosha katika barua hizo ikiwa ni pamoja na picha za mnato na video, maneno aliyotamka kwenye mkutano, picha inayoonyesha akiwa amveaa sare za CCM na jinsi anavyocheza".

Picha zilizonyeshwa kwa waandishi wa habari zilionyesha Balozi Youging akiwa katika mikutano mbalimbali ya CCM maeneo ya Kishapu, Shinyanga na Kahama.

Katika picha hizo balozi huyo alionekana amevaa sare za CCM, akihutubia na kuendesha baiskeli akiwa na viongozi wa chama hicho akiwamo Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.


Kwa mara ya kwanza balozi huyo aliibukia katika mkutano waCCM uliofanyika Shinyanga huku akishangiliwa na wananchi alipojaribu kuzungumza kisukuma.

CCM yazungumza
Wakati huohuo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimesikitishwa na hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumshutumu Balozi wa China, Dk. . Lu Youqing kwa kuhudhuria mikutano ya CCM.)

Kimewataka watanzania kupuuza madai ya Chadema kikisema hayana msingi kwa maendeleo ya taifa na watu wake.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu.


Alisema ni wazi Chadema kinataka kutumia matatizo ya wananchi kuyageuza agenda ya siasa.

Chadema haina budi itambue kuwa chama tawala cha China (CPC) kimekuwa na urafiki wa muda mrefu na CCM ikizingatia Balozi Dk. Lu pia ni kiongozi wa chama hicho.


Nape alisema hatua ya Balozi huyo kuhudhuria mkutano huo ni mafanikio ya ziara ya iliyofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana China mapema mwaka huu.

"Balozi Dk. Lu amekuja kuleta ukombozi kwa watanzania hasa wa Kanda ya Ziwa kwa kuleta wawekezaji katika Mkoa wa Shinyanga kwa kujenga viwanda wa nyuzi, pamba, nyama, maji na ngozi ambako ajira zaidi ya 1000 zitapatikana.


"Watanzania wapuuze madai haya kwani si dhambi kwa Balozi wa China kuhudhuria mkutano wa CCM…urafiki wetu hakuanza leo ni wa muda mrefu katika historia ya nchi hizi mbili tangu na baada ya Uhuru,"alisema Nape.

Nape alisema CCM imepitaka kila eneo la yakiwamo majimbo yanayoongozwa na wapinzani na kubaini kuwapo changamoto nyingi.

Aliitaka Chadema kwenda kutatua haraka matatizo hayo badala ya kufanya mikutano Dar es Salaam pekee.


Wiki iliyopita akiwa mjini Shinyanga Balozi Dk. Lu Youqing, alihudhuria mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema kuwa hakuna chama imara kama hicho.