MASHAHIDI WANNE WAJITOA KESI YA KENYA HUKO ICC

Kiongozi wa mashtaka katika
mahakama ya kimataifa ya
jinai ICC, Fatou Bensouda,
amepata pigo jengine baada
ya mashahidi wengine
wanne kujiondoa katika kesi
dhidi ya Naibu Rais wa
Kenya William Ruto na
mshtakiwa mwenzake
Joshua Arap Sang.


Hili limetokesa siku moja tu
kabla ya Bensouda kuanza
kuwasilisha mashahidi
mbele ya mahakama siku ya
Jumanne kesi dhidi ya Ruto
itakapoanza tena.

Mashahidi hao
wanajumuisha manusura wa
moto ulioteketeza kanisa la
Kiambaa mkoa wa Rift
Valley na kusababisha vifo
vya watu 35 wakati wa
ghasia za baada ya
uchaguzi mkuu nchini Kenya
mwaka 2007-2008
Bwana Ruto anatuhumiwa
kwa kuchochea ghasia ili
kujinufaisha kisiasa wakati
Sang akidaiwa kumsaidia
Ruto kuafikia malengo yake
kwa kutumia kituo cha Redio
alichokuwa anafanyia kazi
wakati wa ghasia hizo.


Hii sio mara ya kwanza kwa
mashahidi kujiondoa katika
kesi dhidi ya washukiwa
hawa. Wiki mbili zilizopita
mashahidi wengine wawili
walijitokeza nchini Kenya
wakidai kuwa
wanalazimishwa na upande
wa Mashtaka kutoa ushahidi
wa uongo dhidi ya wawili
hao.

Wadadisi wanasema kuwa
kujiondoa kwa mashahidi
katika kesi hii bila shaka
kutaathiri uwezo wa
kiongozi wa Mashtaka Fatou
Bensouda lakini amewahi
kusikika akisema kuwa kwa
mashahidi kujiondoa katika
kesi yake dhidi ya Ruto na
Sang sio hoja.


Kesi dhidi ya Ruto
iliakhirishwa wiki jana
baada ya upande wa
mashtaka kusema kuwa
hawajakuwa tayari
kuwasilisha mashahidi wao
na hivyo kupewa muda na
mahakama hadi siku ya
Jumanne wiki hii.