JESHI LA POLISI LAPATA KASHIFA

Jeshi la Polisi limeingia
katika kashfa nzito baada
ya mkuu wake, Inspekta
Jenerali Said Mwema,
kuibiwa upanga wa
dhahabu ambao ni mali
ya Shirikisho la Wakuu wa
Majeshi ya Polisi wa nchi
za Kusini mwa Afrika
(SARPCCO).

Upanga huo wenye uzito
wa takriban kilo tatu na
wenye thamani ya zaidi ya
fedha za Tanzania Sh600
milioni, ni kielelezo kwa
nchi inayokabidhiwa
uongozi wa SARPCCO.

Mwaka jana Tanzania
ilikuwa mwenyekiti wa
SARPCCO, ambapo upanga
huo ulikabidhiwa kwa IGP
Mwema na Jenerali
Magwashi Victoria ‘Riah’
Phiyega, ambaye ni
Kamishna wa Taifa wa
Polisi wa Afrika Kusini
aliyekuwa amemaliza
muda wake kwa wakati
huo.

Hilo ni tukio la pili la wizi
la mali zinazohusu ofisi ya
IGP, ambapo mwaka jana
ndani ya ofisi hiyo
kuliibwa kompyuta ndogo
(laptop), ikiwa na taarifa
muhimu za kipolisi. Hadi
sasa hakuna taarifa za
kupatikana kwa kompyuta
hiyo.

IGP Mwema alikabidhiwa
upanga huo Septemba 5,
2012, katika mkutano saba
wa SARPCCO uliofanyika
Zanzibar na kuhudhuriwa
na wakuu wa majeshi ya
Polisi kutoka nchi 13,
pamoja na mashirika ya
kimataifa.

Upanga huo ambao
unakwenda sambamba na
bendera ya SARPCCO, ni
moja ya vielelezo vya nchi
iliyochaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa shirikisho
hilo, ambaye moja kwa
moja anakuwa ni Mkuu
wa Jeshi la Polisi katika
nchi husika.

Kwa mujibu wa taratibu
za SARPCCO, vielelezo
hivyo hutakiwa kuwekwa
ofisini kwa kiongozi
husika, ikiwa ni alama ya
kila mgeni atakayeingia
ofisini hapo kutambua
uwepo wa wadhifa huo wa
kimataifa.

Uchunguzi wa gazeti hili
ulibaini kuwa IGP
aligundua kutoweka kwa
upanga huo wiki iliyopita,
wakati akijiandaa kwenda
kuukabidhi kwa
mwenyekiti mpya wa
SARPCCO, ambaye ni IGP
wa Namibia.

Taarifa za ndani ya jeshi
hilo zilibaini kuwa, IGP
alilazimika kuondoka bila
upanga huo alipokwenda
Namibia wiki iliyopita
kuhudhuria mkutano wa
nane wa SARPCCO,
uliofanyika Jumapili
iliyopita mjini Windhoek.

Kwa mujibu wa
uchunguzi, IGP Mwema
alikabidhi upanga
unaofanana na huo ambao
siyo wa dhahabu,
alioazimwa kutoka kwa
Mkuu wa Jeshi la Polisi la
Namibia, Inspekta Jenerali,
Luteni Jenerali Sebastian
Ndeitunga, na
kukabidhiwa kama ishara
ya kukabidhiwa uenyekiti
wa SARPCCO kwa kipindi
cha mwaka mmoja.

Uchunguzi ulibaini kuwa
IGP Mwema alitoa ahadi
ya kurejesha upanga halisi
ndani ya kipindi cha
mwezi mmoja, au Serikali
ya Tanzania italazimika
kutengeneza mwingine
kulipa uliopotea.

Uchunguzi wa gazeti hili
unaonyesha kuwa kashfa
hiyo ametupiwa Mkuu wa
Polisi Zanzibar, Kamishna
Mussa Ali Mussa pamoja
na dereva wake, ikidaiwa
kuwa upanga huo baada
ya kupokewa na IGP
Mwema, Septemba mwaka
jana uliwekwa kwenye
gari la kamishna huyo.

Kamishna Mussa ndiye
alikuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya
Mkutano wa Saba, na pia
ofisa mwenyeji kwa
wajumbe wa mkutano huo
uliofanyika Zanzibar.

Hata hivyo, taarifa zingine
zilidai kuwa IGP Mwema
naye analaumiwa kwa
kutofuatilia kwa karibu
zana za kazi, kwani baada
ya kuupokea alitakiwa
kuhakikisha unakuwepo
ofisini kwake kama alama
ya uenyekiti wake.

Gazeti hili lilipowasiliana
kwa njia ya simu na Mkuu
wa Polisi Zanzibar,
Kamishna Mussa Ali
Mussa kuhusu madai hayo
alisema, kitara (upanga)
hicho ni kweli kimepotea,
lakini yeye hahusiki kwa
kuwa kila kitu kina
utaratibu wake.

“Ni kweli kitara
kilikabidhiwa kwa afande
IGP na mimi nilishuhudia
kikikabidhiwa, na ni kweli
kitara hakijulikani kiliko,
lakini mimi sihusiki na
kupotea kwake. Ni kweli
mimi nilikuwa ofisa
mwenyeji wa mkutano
huo, lakini siku hiyo
zilitolewa zawadi nyingi,
watu walipewa mikoba,
kwa hiyo mtu akipoteza
mkoba wake niulizwe
mimi?” alihoji Kamishna
Mussa.

Alisema kila kitu kina
utaratibu wake na
kwamba taarifa kwamba
yeye amehojiwa kutokana
na upotevu wa kitara
hicho au kuna kamati
imeundwa, hazina ukweli.

“Sijawahi kuona kamati
hiyo. Kamati hiyo kwanza
imeundwa na nani na
inatoka wapi? Hayo
maneno yanatengenezwa
na watu wa nje,” alisema
Kamishna Mussa.

Alisema kinachofanyika
hivi sasa ni kukitafuta ili
kiweze kurejeshwa
kunakohusika.

Taarifa zingine zilidai hata
bendera ya mezani ya
mwenyekiti wa SARPCCO,
aliyokabidhiwa sambamba
na upanga huo nayo kuna
hatihati ilipotea.

Msemaji wa Jeshi la Polisi
nchini, Advera Senso
alipotakiwa kuzungumzia
suala hilo alisema aulizwe
kamishina wa polisi
Zanzibar.

“Suala hilo muulize
Kamishina wa Zanzibar
ndiye anayejua,” alisema
Senso.

Uchunguzi unaonyesha
kuwa maofisa katika ofisi
ya IGP na ile ya Kamishna
wa Polisi Zanzibar,
wamehojiwa akiwamo
Kamishna Mussa, na
kwamba upelelezi mkubwa
umekuwa ukiendelea
ndani ya jeshi hilo.

Hata hivyo, juhudi za
gazeti hili za kutaka
kufahamu uamuzi wa
SARPCCO katika ofisi yake
ya uratibu iliyopo kwenye
ofisi za Makao Makuu ya
Kanda ya Polisi wa
Kimataifa (INTERPOL),
Harare, Zimbabwe,
hazikuzaa matunda baada
ya baruapepe iliyotumwa
kwa ofisa mratibu wa
SARPCCO ambaye pia ni
mkuu wa ofisi ya Kanda
ya INTERPOL, C. Simfukwe
kutopata majibu.

SARPCCO ilianzishwa
mwaka 1995, Victoria Falls,
Zimbabwe, lakini kisheria
ilitambulika rasmi mwaka
2006 na lengo lake kuu ni
kupambana na uhalifu wa
kuvuka mipaka.

Uenyekiti wake ni mwaka
mmoja, ambapo kwa sasa
mwenyekiti ni Mkuu wa
Jeshi la Polisi la Namibia
Inspekta Jenerali, Luteni
Jenerali Sebastian
Ndeitunga, aliyepokea
wadhifa huo kutoka kwa
IGP Mwema.


Source:Mwananchi