KANDA YA VIDEO YA SHEIKHE PONDA AKIHAMASISHA UASI YADAKWA.

SERIKALI imenasa kanda za video
zinazomuonyesha Kiongozi wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa
Ponda, akitoa mahubiri yanayowahamasisha
waumini wa dini ya Kiislamu kuanzisha uasi
dhidi ya serikali.
Tukio la kunaswa kwa kanda hizo limekuja
ikiwa ni siku chache baada ya Jeshi la Polisi
Zanzibar kutangaza kumsaka Sheikh Ponda
kwa tuhuma za uchochezi, akingali anatumikia
kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Dar es
Salaam kumkuta na hatia ya kosa la uchochezi.

Katika kanda hizo ambazo MTANZANIA
Jumapili imefanikiwa kuziona, Sheikh Ponda,
amerekodiwa akiwa katika Msikiti wa
Mbuyuni, Zanzibar, alikohudhuria Mhadhara
wa Dini ya Kiislamu, akiwataka waumini wa
dini hiyo kuchukua hatua za kuikomboa
Zanzibar kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani, kutoka kwenye
mikono ya utawala wa makafiri.

Huku akiitikiwa kwa neno Takbir kutoka
washiriki wa mhadhara huo, Sheikh Ponda
anasikika akisema Zanzibar ni nchi ya Kiislamu,
hivyo Waislamu wana wajibu kwa kuikomboa
kutoka mikononi mwa vibaraka wanaoiongoza,
aliodai kuwa wananyonya uchumi wake na
kuutoroshea nje ya visiwa hivyo.

Moja ya kanda hizo iliyorekodiwa kwa muda
wa saa moja na dakika ishirini na nne, ambayo
Sheikh Ponda alitumia muda mwingi kusisitiza
umuhimu wa Waislamu kuikomboa Zanzibar
kutoka mikononi mwa aliowaita makafiri,
anasikika akisema:
"Mna wajibu wa kuikomboa Zanzibar na si
mnaweka vibaraka, wanateuliwa huko halafu
wanakuja hapa kuwaongozeni, fedha zote
zinachukuliwa hapa na kupelekwa kule kwa
sababu tumepoteza nchi, tumepoteza hadhi.

"Makafiri wanatakiwa kuyaheshimu mambo
matakatifu ya Kiislamu na kuyajua, kama
hawataheshimu Mwenyezi Mungu alisema
lazima mlipize kisasi katika mambo
matakatifu. Mungu alisema ni lazima mlipize
kisasi mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu.
Mambo matakatifu yamewekewa kisasi.

"Miongoni mwa mambo matakatifu
yaliyowekewa kisasi ni haki na uadilifu
pamoja na dini ya Kiislamu,
unapozungumzia dini ni pamoja na masheikh,
hawa ni watu watakatifu, watu wenye hadhi, ni
watu wakubwa na watakatifu kuliko baba
mtakatifu kama wanavyosema wao."
Sheikh Ponda pia anasikika akieleza kuwa
Waislamu wamedhalilishwa kwa muda mrefu,
hivyo wana wajibu wa kuikomboa Zanzibar
kwa kuwa hata Mtume Mohammad aliongoza
jeshi akakomboa nchi ya Maka kipindi cha
Mwezi Ramadhani.

Alieleza kushangazwa na uteuzi wa Rais wa
Zanzibar kufanyikia Dodoma na hata uamuzi
wa kumuondoa madarakani kuchukulia
mkoani humo na kutoa mwito wa jambo hilo
kusitishwa.

Katika hili anasikika akisisitiza kuwa; "Hakuna
mtu ambaye haelewi kwamba Zanzibar ipo
mikononi mwa watu wasio stahiki, Zanzibar
ni nchi ya Waislamu. Sisi Waislamu wa
Zanzibar tuna mazingatio makubwa kuliko
watu wengine kipindi hiki cha Mwezi
Ramadhani kwa sababu mafundisho
tunayoyapata katika maisha ya Mtume
Mohammad ni sawa na mazingira ya sasa,
hivyo tunatakiwa kuyatekeleza. Zanzibar si
nchi ya watu, bali ni ya Waislamu.

Katika mahuburi yake kwenye mhadhara huo,
Sheikh Ponda anakisika akieleza kuwa
Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umezaa
ufisadi visiwani humo na kurejea kauli aliyodai
kutolewa na Mtume iliyokuwa ikiwaonya
Wazanzibari kutoruhusu uwepo wa Muungano.
"Tangu lini bia, ukahaba ukawa hitajio la
Wazanzibari na hii ndiyo 'product'
iliyotokana na Muungano na Mapinduzi.
Maovu ambayo hamkuyapata kuyaona ni kauli
ya Mtume, alisema mkiruhusu muungano
ufisadi unatokea. Leo hii mnaona nchi ya
Zanzibar mambo ambayo si hitajio la
Wazanzibari, mmeingiza watawala waovu
katika ardhi hii.

"Zanzibar ina watu wenye akili kubwa, wenye
uwezo na ina wasomi wa fani zote na ni watu
wa kuigwa duniani kote…. hivi sasa
Mwislamu anapokwenda mahakamani
anayesikiliza shauri ni kafiri. Mwislamu
anapofunguliwa kesi, sheria hazifuatwi kwa
maana kwamba kuna utaratibu wa dhamana,
lakini hautolewi, jambo ambalo linaonyesha
wazi kuwakandamiza Waislamu.
"Leo hii viongozi wetu wanatiwa jela bila
sababu, kosa lao ni pale wanapotetea
Uislamu. Wako gerezani, tutapataje sifa ya
Ramadhani tusipowatoa hawa ndugu zetu
walioko gerezani na Mungu anasema mambo
matakatifu yanalipiziwa kisasi.

"Kila siku viongozi wa Kiislamu wanauawa,
Sheikh Hamis ameuawa anatoka msikitini,
kafa na hakuna maelezo kwa sababu kwa
mujibu wa sheria, lazima kuwe na maelekezo
na mahakama iseme. Yote hayo hakuna
maelezo yoyote utadhani kafa paka, kapigwa
risasi kafa hakuna maelezo yoyote ya serikali.
"Ndugu zangu hali ni mbaya sana, watu
wanapanga mikakati kwa ajili yenu ninyi.
Msifikirie kuwa jamii haiwezi kutoweka.
'Tujenga utayari kwa ajili ya kupigania dini ya
Mwenyezi Mungu, hilo ni jambo la msingi.

Ukimya wenu ni tatizo kubwa sana, hivi ndivyo
wanavyotaka wafike mahala wakamate
mashekh wawaweke ndani, halafu mkae kimya,
hili jambo ni kubwa na ni la dini, mnatakiwa
msimame kidete kwa ajili ya jambo hili.
"Suala la kisasi lina uhusiano na uhai,
mtapata uhai mzuri katika kulipiza kisasi
ninyi Waislamu."
Akizungumzia kukamatwa kwake hapo awali,
alisema ulikuwa ni mkakati uliopangwa
Dodoma, baada ya kusikilizwa kwa malalamiko
ya waumini wa dini ya Kikristo.

Mbali na hayo, kauli nyingine zinazoelezwa na
baadhi ya watu walioona na kusikiliza kanda
hizo kuwa zina kila dalili ya kuhatarisha amani
nchini, ni ile anayosikika akisema; "Sisi
viongozi ndio tunatoa maagizo tuingie
barabarani hata kama serikali imepiga
marufuku. Kama wataleta jeshi sisi tunakuwa
'front.'
"Kama wewe unaogopa polisi itakapofika
Jihad utatoka, hawa ni watu kama wewe,
anavyokupiga kirungu hakuna sababu ya
kumwogopa binadamu mwenzako, hizo ni
hatua za kujenga nafsi na utayari.

"Kipindi cha uchaguzi mkitumie vizuri,
muwatoe hawa madarakani, watoeni
wakatae halafu kimbembe kianze pale,
mnatoa kauli ya moja kwa moja. Waambieni
kuwa ninyi na sisi ni moto na baruti.
"Kwa upande wa Katiba, kuna suala la
kupiga kura, hakikisheni kura yenu
izingatie maslahi yenu.

Kule Bara
tulipendekeza mahakama ya kadhi
imetupwa na sasa hivi kazi zile ambazo
zinatakiwa kufanywa na mahakama ya
kadhi zinafanywa na mahakama ya
mwanzo."

--
Posted By Blogger to Michael M. Mazalla at 8/04/2013 02:46:00 PM