kumekuwapo na mjadala
kuhusiana na hatua ya klabu ya
Yanga kupinga udhamini wa Ligi
Kuu ya Tanzania unaotarajiwa
kufanywa na Azam Media.
Tumeona ni vema tukatoa
msimamo wetu wa pamoja
kuhusiana na hatua hiyo ya
wenzetu kwa lengo la kuweka
rekodi sawa.
Tunataraji hatua hii ya vilabu hivi
13 itafunga mjadala huu na
tungependa wana habari, kama
mtaamua kuuendeleza, basi
muundeleze katika mrengo
ambao wadau, yaani sisi vilabu
vinavyoshiriki mashindano hayo,
zimeamua kuufuata.
Tunapenda kukumbusha kwamba
kwa muda mrefu, kilio cha vilabu
vya Ligi Kuu ya Tanzania vilikuwa
ni ukosefu wa wadhamini na kwa
bahati nzuri kuna dalili kwamba
Mungu ameanza kukisikia kilio
hicho msimu huu.
Kwa faida ya umma, tungependa
kutoa takwimu za nchi jirani
zinazotuzunguka. Kenya, kila
klabu hupata Sh milioni saba za
Kenya (sawa na Sh milioni 125 za
Kitanzania) kwa mwaka –fedha
ambazo zimeifanya ligi ya Kenya
kuwa na uwiano na ushindani wa
kweli (fedha hizo ni mjumuisho wa
gharama za matangazo ya
televisheni na udhamini wa bia ya
Tusker).
Tanzania leo tunajivunia kuwazidi
Kenya kutokana na udhamini wa
Azam ambapo kwa mwaka huu,
kila klabu itapata zaidi ya Sh
milioni 170 (Jumla kutoka milioni
100 za Azam na milioni 70 za
Vodacom).
Hatuna sababu ya kutaja viwango
vya udhamini kwa nchi nyingine
jirani kama Uganda, Burundi,
Rwanda, Zambia nk kwa vile zote
zina udhamini wa chini kuliko
Kenya.
SuperSport, ambao wanaliliwa na
baadhi yetu, udhamini wao kwa
ligi ya Uganda ni dola 350,000
ambazo ni pungufu kulinganisha
na dola milioni moja zilizotolewa
na Azam Media hapa nchini.
Ni imani yetu kwamba udhamini
huu utaifanya ligi ya Tanzania
kuwa bora kuliko zote za Afrika
Mashariki. Hili litasaidia
kutengeneza timu bora ya Taifa ya
Tanzania.
Tungependa kutoa ufafanuzi wa
masuala machache ambayo
yaliongelewa na wenzetu wa
Yanga kama sababu za kupinga
udhamini huu.
BODI YA TPL
Kwa mujibu wa Katiba za FIFA, CAF
na TFF, Haki za Televisheni zipo
chini ya FA ya nchi husika. TFF
iliamua kukasimu shughuli ya
majadiliano kwa Kamati ya Ligi
ambayo ilishirikisha vilabu vyote
14, ikiwamo Yanga na wawakilishi
wake walihudhuria mchakato
mzima hadi mwisho.
Hoja ya Yanga kuwa bodi haina
nguvu/Mamlaka kisheria kwa
kuwa ni ya mpito inakosa mashiko
kwa sababu kimsingi ni TFF ndiyo
iliyoingia mkataba kwa sababu
ndiyo iliyopewa mrejesho na
Kamati ya Ligi kwamba mchakato
umekwenda sawasawa.
Hoja ya kuwa Bodi ya TPL iliyoko
sasa hivi haina mjumbe hata
mmoja aliyeteuliwa kutoka
YANGA.
Hili si kweli hata kidogo.
Mmoja wa wajumbe wa TPL ni Seif
Ahmed almaarufu Seif Magari;
ambaye vyeo vyake ndani ya
Yanga vinajulikana.
Kama alikuwa hahudhurii vikao
vya TPL, hilo ni suala la Wanayanga
wenyewe kumuhoji kwanini
alikuwa hahudhurii hivyo na hivyo
kuinyima klabu yake ushiriki
katika mijadala muhimu kwa
maslahi ya soka hapa nchini.
Ifahamike pia kwamba TPL
haikuhodhi mchakato huu bali
ilitoa fursa kwa vilabu vyote vya
Ligi Kuu kushiriki ambapo Yanga
ilikuwa ikiwakilishwa na Makamu
Mwenyekiti wake, Clement Sanga
na Katibu Mkuu, Lawrance
Mwalusako.
Hii maana yake ni kwamba hoja
kuwa Yanga haikushirikishwa ni
mfu.
Yanga walitumia neno UTARATIBU
WA DUNIA NZIMA wakisema eti
hakuna mahala duniani ambapo
kampuni yenye klabu inayocheza
ligi husika kupewa mkataba wa
udhamini au urushwaji wa
matangazo.
Inaonekana Yanga hawakufanya
utafiti kwani ligi ya Afrika ya
kusini ina timu inayoitwa Super
Sports United na inarushwa na
kituo cha TV cha Supersports.
Pia majirani zetu Kenya wana timu
inayoitwa Tusker FC huku ligi hiyo
ikidhaminiwa na bia ya Tusker.
Tunawashauri Yanga kuwa ni vema
kufanya utafiti kabla ya kuibuka
na hoja za namna hii ili kuepuka
kuwapotosha wanachama wao.
Yanga pia katika hoja zao
wamepinga utaratibu wa
kugawana mapato sawa.
Hoja hii ni
ya msingi na majadiliano yetu
yalilitazama hili kwa kina lakini
tukaona kwa mazingira ya
Tanzania na uchanga wa ligi
yenyewe kwa sasa ni heri
kugawana sawa ili pesa kwa usawa
ili itoke kwa wakati na kusaidia
vilabu kujiendesha. Yanga
wanakosea wanaposema eti wao
wanastahili kupewa zaidi kwa
sababu ni klabu kubwa na yenye
mashabiki wengi kwa kuwa sababu
hii haitumiki sehemu yoyote
duniani.
Tuchukulie mfano wa nchi ya
England ambako ingawa Liverpool
ina washabiki wengi kuliko
Manchester City na Chelsea,
imezidiwa kwenye mapato ya
televisheni na timu hizo.
Hii ni sababu kinachoamu mapato
mwisho wa siku ni kiasi cha mechi
za timu ambazo zimeonyeshwa na
televisheni kwenye msimu husika
na nafasi ya timu kwenye
msimamo wa ligi.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba
nchini England, malipo haya
hufanyika baada ya msimu
kumalizika na hapo ndipo watu
hukaa chini na kupigiana hesabu
za nini kilipatikana. Sasa ukitumia
mfumo huu, ina maada timu
zitalazimika kusubiri ligi iishe ili
kuangalia msimamo ya ligi kisha
kugawana mapato. Sote tunajua
jinsi timu zinavyoteseka kwa
kukosa nauli, posho, mishahara,
pesa za kambi nk.
Kwa mazingira yetu ya Tanzania
kwa sasa, mfumo kama huu
haufai. Hii ni kwa sababu timu
zinahitaji fedha kuanzia kwenye
maandalizi ya mechi ya kwanza na
hazikopesheki fedha kwenye
mabenki.
Tanzania inachohitaji kwa sasa ni
ligi yenye ushindani tofauti na
sasa ambapo ushindani uko kwa
timu chache zenye uwezo wa
kifedha.
Tukizijengea uwezo timu zote taifa
litakuwa na ligi nzuri na hatimaye
timu nzuri ya taifa. Pia itawezesha
wadhamini wengi zaidi kuingia
kwenye mpira na hivyo timu
nyingi zaidi kufaidika.
Tukifikia huko, tunaweza kukaa
chini na kutazama mfumo wa
kugawana mapato utakaokuwa
bora zaidi wakati huo.
Mambo ya Kuzingatia.Tangu ligi
ianze hapa nchini takribani miaka
50 iliyopita, hakuna timu iliyowahi
kulalamikia mfumo wa kugawana
mapato sawa kwa kila mechi
ambao umekuwa ukitumika.
Mfano mapato ya mlangoni
tumekuwa tukigawana sawa na
Yanga haijawahi kulalamika, Pesa
za udhamini wa Vodacom tangia
ilipokuwa ikidhaminiwa na TBL
hadi leo hii tumekuwa tukigawana
sawa na Yanga haijawahi
kulalamika kutaka kupata zaidi
kwa kuwa eti ina mashabiki wengi,
pia hata pesa za haki ya matangazo
ya Televisheni zilizowahi kutolewa
huko nyuma nailiyokuwa ikiitwa
GTV, na Star TV kwa nyakati tofauti
pesa ziligawiwa sawa kwa kila
timu.
Hii ni kwa sababu kikanuni, timu
zote zinazoshiriki kwenye ligi ni
sawa na zote zinaweza kuwa
bingwa au kushuka daraja.
Ni mdudu gani huyu aliyeingia
kwenye soka ya Tanzania na
kuanza kuleta siasa za kubaguana?
Baba wa Taifa alipata kutuasa
kwamba dhambi ya ubaguzi ni
sawa na kula nyama ya mtu.
Ikianza, haitaishia kwenye ligi
pekee na itakwenda hadi mahali
tusipotaka.
MGOGORO WA MASLAHI
Yanga imekuwa ikilalamikia
uwepo wa kiongozi mwandamizi
wa makampuni ya Bakhresa
kwenye bodi ya Ligi na kusema
inaleta mgongano wa maslahi.
Sisi vilabu tunaamini kwamba
uwepo wa kiongozi huyu ndiyo
umesaidia makampuni yake
kuwekeza fedha kwenye mpira.
Na mifano ipo hai tukianzia na
michuano ya Vijana ya Uhai Cup,
ujenzi wa kituo cha michezo cha
Chamazi ambacho kinatumiwa na
timu nyingi za Tanzania.
Na sasa tunafaidika na udhamini
huu mnono ambao haujapata
kutokea katika historia ya
Tanzania.
Tungependa viongozi wengi zaidi
wa makampuni yanayoheshimika
hapa nchini wakijitokeza kuongoza
mpira badala ya kuanza
kuwapinga.
Kwa mfano, tungependa kuona
mkurugenzi wa benki ya CRDB
akiwa kiongozi wa Ashanti, bosi wa
Barrick akiongoza Mbeya City na
Mkurugenzi wa Tanga Cement
akiongoza Coastal Union.
Hivi ndivyo namna mpira
unavyoweza kuvutia wawekezaji.
Ndiyo maana tulifurahi wakati
Yusuf Manji, alipoomba uongozi
Yanga.
Bado tunataraji kwamba naye
atajitosa kuingiza fedha zake
kwenye ligi ya Tanzania (mpira)
kama alivyofanya Bakhresa
ambaye pamoja na kutumia fedha
zake Azam FC, bado ameamua
kusaidia na timu nyingine kwa
ujumla.
Tunapenda kumuahidi Yusuf Manji
kwamba iwapo naye atataka
kudhamini Ligi Kuu iwe kibiashara
au kiufadhili, sisi tutamuunga
mkono na hatutajali suala la
mgongano wa maslahi.
UPOTEVU WA MAPATO
Wenzetu Yanga wamedai kwamba
kwa kuonyesha mechi kwenye
televisheni, mapato yake ya
mlangoni yatapungua.
Hili pia halikufanyiwa utafiti wa
kutosha. Katika siku za karibuni,
mechi zilizoingiza mapato
makubwa zaidi ya milangoni ni zile
ambazo zilionyeshwa Live kwenye
televisheni za ndani na nje ya
nchi.
Mifano ni mechi za watani wa jadi
msimu uliopita zilizoonyeshwa
Live na SuperSport na mechi za
Kombe la Kagame zilizoonyeshwa
wakati huo.
Hata mechi ya Taifa Stars na Ivory
Coast iliyoonyeshwa Live pia,
ilijaza uwanja. Ulaya ambako
karibu kila familia inamiliki
televisheni na umeme wa
uhakika, bado watu wanajaa
katika viwanja vya soka.
Mpira kuonyeshwa kwenye
televisheni unaufanya utangazike
zaidi na watu watake kuona. Kuna
faida nyingi za mpira kuonyeshwa
kwenye televisheni kuliko hasara
moja ya kufikirika ambayo Yanga
wanaiona.
Ingekuwa vema iwapo Yanga
wangetoa takwimu za kuonyesha
ni kwa namna gani mechi
kuonyeshwa kwenye televisheni
kuliwahi kupunguza mapato ya
milangoni.
Kwa faida ya umma, mpira kuwa
kwenye televisheni kuna faida
zifuatazo; jezi kuongezeka
thamani na hivyo kuvutia
makampuni makubwa kutaka
kudhamini klabu wakitumia fursa
ya kutangaza bidhaa zao,
matangazo ya viwanjani (touchline
fence) kuwa na thamani zaidi
ambapo kwa sasa vilabu havipati
chochote, kuchochea michezo ya
kubahatisha, kutabiri matokeo na
kupata habari kupitia simu za
mkononi na hivyo vilabu vitaanza
kutengeneza fedha za kutosha.
Ulaya wamesonga mbele kutokana
na televisheni. Anayekataa mpira
kuonyeshwa kwenye televisheni
ni sawa na mtu anayegoma
kutumia mfumo wa digitali katika
ulimwengu wa leo.
UWAZI KWENYE MCHAKATO WA
KUUZWA KWA HAKI ZA
MATANGAZO
Yanga wameandika kwenye taarifa
yao rasmi eti hakukuwa na uwazi
kwenye mchakato wa kuipata
kampuni ya kurusha matangazo ya
Televisheni.
Sote tunajua kuwa vituo vya
televisheni vilivyopo nchini kama
Star TV ambayo iliwahi kurusha
mechi kadhaa msimu uliopita
vilikuwa vikijua kuwa kuna nafasi
hiyo na TFF mara kadhaa
wamekuwa wakitangaza hilo
kupitia idara ya Habari ya TFF.
TFF kwa mfano walikwenda mbali
kwa kuialika Supersports kuja
kuonesha mechi bure kwa
kilichokuwa kikiitwa Super Week
ili kuwashawishi waje kuwekeza
na mara ya mwisho ni Yanga hawa
hawa walioongoza harakati za
kuikataa Supersports kuonesha
mechi bure wakisema kuwa kama
ni kuwavutia inatosha.
Katika mazingira kama haya
tunastaajabishwa na ukigeugeu wa
Yanga leo kusema eti tenda
haikuwekwa wazi. Sote tunajua
kuwa ni Super Sports pekee
tuliokuwa tukiwategemea na
kuwashawishi ambao
hawakuonesha kuhitaji kuja
kuwekeza. Kwa nini leo tuikatae
Azam TV?
Yanga wanaposema eti TFF/Kamati
ya Ligi imeipa haki za matangazo
kampuni ambayo haina ofisi wala
kituo cha televisheni kilicho
hewani kwa sasa wanasahau kuwa
huko nyuma TFF iliwahi kuwapa
haki za matangazo GTV ambao
hawakuwa na ofisi wala kitu cha
TV na baada ya miezi michache
walifungua ofisi zao na kuleta
vingamuzi na kuaza kurusha mechi
zetu. Vilabu vilifaidi udhamini ule
kabla ya ile kampuni kufilisika.
Kwa hiyo hii si mara ya kwanza
kwa jambo hili kufanyika na kama
Azam TV hawataonesha mechi za
ligi hiyo sisi kama vilabu
haituhusu kwani ni hasara yao.
Tunachowaomba Azam Media sisi
kama vilabu ni kuhakikisha
wanatulipa pesa zetu kwa haraka
ili zitusaidie kwenye
maandalizi,Tunawaomba Yanga
wasichafue hali ya hewa kwa kuwa
wao hawana shida ya Pesa.
Sisi Umoja wa Vilabu 13
vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania
tunapinga, kwa nguvu zote, madai
ya Yanga kwamba
hatukushirikishwa kama vilabu
kwenye mchakato huu.
Mfumo wa ugawanyaji wa mapato
tuliouchagua, tuliuchagua
wenyewe bila kushurutishwa na
yeyote na tunadhani ndiyo mfumo
unaotufaa kwa sasa hadi hapo ligi
yetu itakapokuwa na nguvu maana
kwa sasa inaruhusiwa klabu
kupata fedha mwanzoni kulingana
na hali halisi ya vilabu vyetu.
Tunawashauri wenzetu wa Yanga
waanze kuamini kwenye kitu
kinachoitwa Uwajibikaji wa Pamoja
(Collective Responsibility). Mambo
yanayoamuliwa kwenye vikao
hayapaswi kupingwa nje ya vikao.
Kama hoja ililetwa kwenye vikao
na ikazidiwa nguvu na hoja
nyingine, hakuna sababu ya
kuikataa kwa sababu tu
hukubaliani nayo. Mfumo wa
kidemokrasia una kanuni moja
kuu; Wengi Wape
Imetolewa na
Vilabu 13 vya Ligi Kuu ya Tanzania
Simba SC, Azam FC, Ashanti
United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting
Stars, Mgambo JKT, JKT Oljoro,
Rhino Rangers, Mbeya City,
Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar,
Coastal Union na Kagera Sugar.
Chanzo:Shaffihdauda.com