WASOMI WAMUUNGA RAIS KIKWETE MSIMAMO JUU YA RWANDA NA RAIS KAGAME

WASOMI na baadhi ya
wanasiasa wazalendo nchini
wameunga mkono msimamo wa
Tanzania uliotolewa na Rais Jakaya
Kikwete kuhusiana na chokochoko
zinazoanzishwa na Rwanda na
wamemtaka Rais wa nchi hiyo,
Paul Kagame, kukaa meza ya
mazungumzo na waasi wa nchi
hiyo walioko Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
kwani amani haiwezi kutafutwa
kwa njia ya mtutu wa bunduki.


Akizungumza na MAJIRA kwa njia
ya simu jana Mhadhiri wa Chuo
cha St. Agustino, katika kitivo cha
sayansi ya siasa, Prof. Mwesiga
Baregu, alisema ushauri alioutoa
Rais Kikwete kwa Rais Kagame ni
mzuri, hauwezi kuleta athari
zozote tofauti na kutumia mtutu
wa bunduki kukabili waasi.


"Mimi nikiwa kama mtaalam
wa kutatua migogoro suala la
mazungumzo ni njia moja
ambayo huwa inatumika mara
kwa mara na inasaidia kuleta
amani," alisema na kuongeza;

"Kutumia mtutu wa bunduki
haileti tija kwa mataifa yote
mawawili, hivyo ni busara
itumike njia ya mazungumzo."

Alitoa mwito kwa nchi jirani
kushirikiana kutatua mgogoro
uliopo kwa njia ya mazungumzo
baina ya Rwanda na DRC.


Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo
cha Elimu Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Dkt. Kitila
Mkumbo, alisema anakubaliana na
kauli ya Rais Kikwete na
anashangazwa na Rais Kagame ni
kwa nini anachukizwa kuambiwa
azungumze na waasi.


"Maana yake inaonekana hataki
kushauriwa...ushauri huo ni
kitu kizuri kinaweza kuleta
maelewano," alisema Dkt.
Mkumbo. Alisema Rais Kagame,
anaonekana kama dikteta
kutokana na kukataa kuambiwa
ukweli na viongozi wenzake.

Alisema kauli ya Rais Kikwete,
aliyoitoa kwenye hotuba yake ya
mwisho wa mwezi wa saba
hakugusia masuala ya vita na
anaamini kwamba kwa karne hii
sio mwafaka nchi kuingia kwenye
vita kwani nchi zina matatizo
mengi ambayo yanahitajika
kupatiwa ufumbuzi.

"Alichoongea Rais Kikwete, ni
msimamo unaotakiwa kuungwa
mkono na Watanzania kwani
yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na
hiyo ndiyo kauli ya nchi...hivyo
alichosema ni sawa," alisema
Dkt. Mkumbo.


Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri, Absalom Kibanda,
alisema ameridhishwa na kauli ya
Rais Kikwete, kwani ametumia
lugha sahihi katika kueleza hali
halisi, hivyo Watanzania wote
wanatakiwa kumuunga mkono.


Alisema kwa hali ilivyo ni lazima
Watanzania waungane katika
masuala kama hayo ili kuleta
mshikamano wa nchi.


Mwenyekiti wa Tanzania Labour
Party (TLP) Augustino Mrema,
alisema anamuunga mkono Rais
Kikwete, kwa kauli yake hiyo.


Alisema Rais Kagame ameanza
chokochoko dhidi ya Tanzania na
kwamba hivyo, ndivyo alivyoanza
hata Idd Amin. "Siungi mkono
vita vitokee, lakini kama
atatuchokoza basi tuwe wa
mwisho kujibu mapigo," alisema
Mrema.


Aliyekuwa Mhadhiri UDSM, Dkt.
Azaveri Lweitama, amezitaka nchi
za Afrika Mashariki kukaa chini ili
kuangalia jinsi ya kutatua mgogoro
huo.


Alisema kuipiga Rwanda ni kazi
ndogo sana, lakini hauwezi
kumaliza tatizo kwa kutumia
bunduki na badala yake ni vyema
nchi hizo zikaangalia namna ya
kumaliza mgogoro.

"Unajua mnaweza kuingia
katika vita mkamuondoa Rias
wa Rwanda, lakini bado
mkatengeneza matatizo mengine
kwa rais ajaye," alisema.


Alisema Kongo kuna waasi wa
Rwanda na hata Rwanda pia kuna
waasi wa kutoka Kongo, hivyo ni
lazima kutafuta njia nzuri ya
kutatua tatizo hilo.

Kwa upande mwingine, Dkt.
Lweitama, alivitaka vyombo vya
habari kutopotosha taarifa
zinazozungumzia vita vikitokea
hakuna mtu atakayebaki salama.


"Vyombo vya habari vijitahidi
kuandika habari zisizo za
uchochoezi, kwani hata ninyi
pia ni Watanzania, naamini vita
ikitokea hakuna mhariri wala
mwandishi atakayebaki
salama," alisema.


Alisema vyombo vya habari pia
vina nafasi ya kukaa chini na
kutafakari namna ya kumaliza
mgogoro kwa kuwa vina nafasi
kubwa kwa mustakabali wa taifa.

Uhusiano wa Tanzania na Rwanda
unaelekea kupata mtikisiko baada
ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa
Serikali ya Rwanda kuzungumza
na mahasimu wao.


Rais Kikwete alitoa ushauri huo
kwa nia njema kwa kuwa bado
anaamini kuwa kama jambo
linaweza kumalizwa kwa njia ya
mazungumzo njia hiyo ni vyema
itumike.

Ushauri ule aliutoa pia kwa
Serikali ya Kongo na kwa Serikali
ya Uganda. ambapo katika
mkutano ule Rais Yoweri
Museveni wa Uganda aliunga
mkono kauli hiyo.


Tangu atoe ushauri huo viongozi
wa Rwanga wamekuwa wakitoa
kauli za kejeli dhidi ya Tanzania na
Rais Jakaya Kikwete. Katika
hotuba yake Rais Kikwete, alisema
uhusiano wa Tanzania na Rwanda
unapitia katika kipindi kigumu

Credits: MAJIRA.