WATANZANIA 247 WASHIKIRIWA KWA KUHUSIKA NA DAWA ZA KULEVYA

WATANZANIA 247
wamekamatwa katika
nchi mbalimbali
duniani na
wanashikiliwa kwa
tuhuma za kukutwa
wakisafirisha dawa za
kulevya. Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera na Uratibu,
William Lukuvi, alisema
hayo jana alipokuwa
akijibu swali la mbunge
wa Viti Maalumu,
Catherine Magige
(CCM).

Katika swali hilo,
Magige aliitaka Serikali
ieleze ukubwa wa
biashara ya dawa za
kulevya nchini na ukoje
na kuhoji kama haioni
kuna tatizo katika
ukaguzi wa abiria na
mizigo kwenye viwanja
vya ndege wanakopita
watuhumiwa.
Mbunge huyo pia
aliitaka Serikali, ieleze
imefanya juhudi gani
za kukabiliana na hali
ya upitishwaji wa dawa
hizo.
Akijibu swali hilo,
Lukuvi alisema ukubwa
wa biashara hiyo
nchini, unadhihirishwa
na idadi hiyo ya
watuhumiwa
Watanzania
wanaoshikiliwa nje ya
nchi kuanzia 2008 hadi
Julai 2013.
Mbali na Watanzania
hao nje ya nchi, Lukuvi
alisema nchini kuna
wageni wapatao 31
wanaoshikiliwa
mahabusu katika
magereza ya Keko na
Ukonga.
Baada ya kutoa
ufafanuzi huo, Mbunge
wa Karatu, Mchungaji
Israel Natse
(Chadema), aliomba
kuuliza swali la
nyongeza ambapo
aliitaka Serikali kutaja
kwa majina wahusika
katika biashara ya
dawa za kulevya.
Akijibu swali hilo,
Lukuvi alisema kazi ya
Serikali si kutaja
majina, bali kuyapokea
na kuyafanyia
uchunguzi na mwisho
kuchukua hatua za
kisheria.

"Si kazi ya Serikali
kutaja wahusika
bungeni, lakini
tunachofanya kwa
ambao wanatajwa ni
kuwapeleka katika
vyombo husika na
kuendelea na
uchunguzi na
wakithibitika ndipo
wanatajwa na
kuchukuliwa hatua.
"Tukisema tuwataje,
hata humu ndani
wabunge wote
watakwisha maana
wako kwengi
wanaotajatajwa. Hata
gazeti la Jamhuri
limetaja maana
wenzetu wanao
ushahidi nao, na wale
wasioridhika wanaweza
kwenda kushitaki.
Hivyo walio na majina
na vielelezo watuletee
ili tuwashughulikie.
Baadhi ya wabunge
walionekana kuguna na
kuzomea pale Lukuvi
alipokuwa akitoa
ufafanuzi wa suala
hilo, jambo
lililomfanya Spika Anne
Makinda, kukemea hali
ya zomeazomea ndani
ya Bunge.

Hivi karibuni, vita dhidi
ya dawa za kulevya,
imekuwa gumzo baada
ya Waziri wa Uchukuzi,
Dk Harrison
Mwakyembe kuapa
kuzuia uchochoro wa
kupitisha dawa hizo
katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere.
Kwa kuanzia, Dk
Mwakyembe alitaja
maofisa alioagiza
wafukuzwe kazi na
kufunguliwa mashitaka
ya jinai chini ya Sheria
ya Kuzuia Dawa za
Kulevya, kwa tuhuma
za kupitisha dawa za
kulevya katika uwanja
huo.
Maofisa hao ni pamoja
na Maofisa Usalama,
Yusufu Daniel Issa,
Jackson Manyonyi,
Juliana Thadei na
Mohamed Kalungwana.
Mbali na maofisa hao,
pia aliagiza Jeshi la
Polisi kumwondoa
mara moja katika
uwanja huo, askari
Polisi, Koplo Ernest na
kumchukulia hatua za
kinidhamu kwa
kushiriki kwake kwenye
njama za kupitisha
mabegi sita ya dawa za
kulevya, yaliyokamatwa
Afrika Kusini.

Pia alisema Polisi
inapaswa kumsaka
Nassoro Mangunga,
aliyekwepa vyombo vya
Dola vya Afrika Kusini
na kutoroka na mabegi
matatu ya dawa hizo.

Dk Mwakyembe alisema
mbeba mizigo katika
uwanja huo, Zahoro
Seleman, anapaswa
kufukuzwa kazi,
kukamatwa na
kufunguliwa mashitaka,
ili aunganishwe na
wenzake kujibu
mashitaka ya jinai.

Dk Mwakyembe pia
aliiagiza Idara ya
Usalama wa Taifa
kuendesha uchunguzi
wa kina kwa maofisa
wake waliokuwa zamu
siku ya tukio, kwa
kuchelewa kufikisha
mbwa wakati mwafaka
kukagua mabegi hayo
na kuliletea Taifa
fedheha kubwa.