WANYARWANDA WAAMBIWA WARUDI KWAO

Mamia ya wahamiaji haramu kutoka nchini
Rwanda wakiwa na ng'ombe zaidi 900
wameanza kuondoka nchini kurejea kwao
kutokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete
kuwataka waondoke Tanzania kabla ya siku
14.


Aidha, imeelezwa kuwa kumekuwapo
ongezeko la askari wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) mkoani Kagera hasa wilayani
Ngara hali inayozua hofu kwa baadhi ya
wananchi, huku ikiongeza msukumo kwa
wahamiaji haramu kuondoka.


Akiwa katika ziara mkoani Kagera, Rais
Kikwete alitoa agizo la kuwataka wote
waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria
waondoke mapema jambo lililotakiwa
kuanza kutekelezwa Julai 29 na kukamilika
Agosti 10 mwaka huu.


Alisema kuwa wahamiaji haramu na wale
wanaoendesha ama kuhusika na ujambazi,
uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa
mifugo waamue kuchukua hatua mwafaka za
kuondoka mapema kabla vyombo vya ulinzi na
usalama kuanza operesheni maalumu ya
kuwasaka.


Tayari idadi kubwa ya wafugaji wenye makundi
ya ng'ombe imeanza kuondoka kuelekea eneo
la mpakani la Rusumo kutoka ardhi ya
Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa agizo hilo la
Rais Kikwete.


Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia
ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine
Kanyasu alisema kwamba idadi kubwa ya
wafugaji waliokuwa wakiishi kinyume cha
sheria, imeitikia wito wa agizo la Rais na
kuanza kuondoka kwa hiyari yao.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na idadi
kubwa ya wahamiaji kuanza kuondoka, bado
wapo ambao hawajaondoka kutokana na kudai
kuwa na vibali walivyovipata kutoka Ofisi ya
Uhamiaji na kubainisha kwamba vibali hivyo
vitakaguliwa kwa umakini wakati wa
operesheni maalumu ili kujua uhalali wake.


"Jambo hili la wahamiaji haramu lilikuwa kero
kubwa, siyo tu kwa Wilaya ya Ngara, bali mkoa
mzima wa Kagera, lakini tunashukuru sasa
wameanza kuondoka, wamebaki hao wenye
vibali. Ni lazima vibali hivyo tutavikagua
maana vipo vilivyotolewa kinamna," alieleza
Kanyasu.


Alionya kwamba jukumu la kuwaondoa kwa
nguvu wahamiaji haramu pamoja na wafugaji
linasubiri muda wa mwisho ili kuanza
kutekelezwa kama Rais Kikwete alivyoagiza.


Hofu ya Wanajeshi kuongezeka

Akizungumzia suala la wanajeshi kudaiwa
kuongezeka wilayani Ngara, Kanyasu alisema
kwamba katika wilaya yake kuna kikosi cha
dharura kinachokaa katika moja ya kambi za
JWTZ kikikuwa na idadi kubwa ya askari lakini
wananchi hawakuwa na taarifa nacho ila
kutokana na sababu za kiusalama.


"Unajua kuna kelele za hapa na pale na
haya majibizano yanayotokea baina ya
Rwanda na Tanzania. Haya ni kama
yamewastua watu na kudhani kuwa askari
wetu wa Kikosi cha Dharura waliopo hapa
Ngara wameletwa maalumu kutokana na
tahadhari," alisema na kufafanua kuwa askari
hao wapo siku zote kwa ajili ya kulinda mipaka
ya Tanzania.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya aliwataka
wananchi kutulia na kutoa ushirikiano kwa
jeshi hilo.


Rais Kikwete aliagiza operesheni hiyo ya
kuwaondoa wahamiaji haramu ifanyike katika
Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati
mmoja ikisimamiwa na vyombo vya ulinzi na
usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa
na Uhamiaji akiwaonya wahalifu kuwa
hapatakuwa na mahali pa kukimbilia wala
kujificha.


Chanzo:Mwananchi