AFYA YA MANDELA YAANZA KUIMARIKA

Rais mstaafu nchini Afrika Kusini ,
Nelson Mandela aliyelazwa hospitalini
tangu tarehe nane mwezi Juni,
anaonyesha dalili za afya yake
kuimarika.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka
kwa serikali. Hata hivyo Mandela
mwenye umri wa miaka 95 angali hali
mahututi ambayo inadhibitiwa na
madaktari.

Rais Jacob Zuma amewataka watu
kuendelea kumuombea Mandela na
kuwashukuru wale waliotenda mema
kwa niaba ya Mandela.

Mandela ambaye ni rais wa kwanza
wa nchi hiyo kuchaguliwa
kidemokrasia, anatazamiwa na wengi
kama baba wa taifa.

Alifungwa jela miaka 27 baada ya
kuanzisha vita dhidi ya utawala wa
ubaguzi wa rangi.

Anajulikana na ukoo wake kwa jina
Madiba, na alichaguliwa kama rais wa
Afrika Kusini mwaka 1994 baada ya
wazungu kumaliza utawala wao na
kisha akaondoka mamlakani baada ya
miaka mitano ya kutawala nchi.

Katika taarifa yake, bwana Zuma alitoa
wito kwa wafanyabiashara kuunga
mkono mradi unaofadhiliwa na wakfu
wa Mandela kujenga hospitali ya
watoto.

"Madiba anapenda sana watoto, na
anawatakia afya nzuri.

Anatutaka
tuhakikishe kuwa wanaishi maisha
mazuri katika siku za baadaye,''
alisema Zuma.

Wakfu wa Mandela , ungependa
kujenga hospitali yenye uwezo wa
kuwashughulikia watoto 238 wa
kulazwa pamoja na kuwatibu watoto
kote nchini Afrika Kusini.