Kila Lazima Kulipia Tsh. 1000/ Kwa kila Laini

SERIKALI imesisitiza kuwa
itatoza Sh 1,000 kwa kila kadi
ya simu inayotumika lakini pia
inaangalia utaratibu wa
kufanya makato hayo kwa njia
ambayo haitamuumiza
mtumiaji wa simu.

Akizungumza jana jijini Dar es
salaam, Waziri wa Fedha,Dk
William Mgimwa alisema kuwa
kupitia tozo hizo wanatarajia
kukusanya Sh bilioni 160 kwa
mwaka.

"Kupitia wawakilishi wenu na
sisi serikali kuwa sikivu,
tulishauriwa na ikaonekana
kwamba kuna uwezekano wa
kupata chanzo kingine cha
mapato kupitia kadi za simu"
alisema.

Alisema katika mapendekezo
yaliyokuwa yametolewa
serikali ilishauriwa kutoza Sh
1,450 katika kila kadi ya simu
lakini baada ya kukaa na
kushauriana serikali iliona ni
vyema ikatoza Sh 1,000 ili kila
mwananchi aweze kumudu
gharama ambapo kwa mwaka
kila mmiliki wa kadi ya simu
atatozwa sh 12,000.

Alisema baadae serikali
ilipokea mapendekezo
mbalimbali ili kuangalia kama
hilo linaweza kutekelezeka na
walipita ngazi zote kabla
halijapelekwa katika kamati za
Bunge na kushauriwa kwamba
tozo hilo linaweza kufanyika
kwa lengo la kukuza uchumi
hasa maeneo ya vijijini.

"Tathmini zote zimefanyika
kikamilifu na baadae suala hilo
likafikishwa Bungeni ambapo
pia napo lilikubalika...
inawezekana watu
wanalalamika lakini ngazi zote
suala hilo lilipopita lilikubalika
na ikaonekana ni sawa
kutozwa sh 1,000 kwa kila
kadi ya simu" alisema.

Alisema kutokana na hilo kwa
kutwa nzima kadi ya simu
itatozwa Sh 33.35 au Sh 100
kwa siku tatu ambapo serikali
inaangalia utaratibu mzuri
ambao hautamuumiza
mtumiaji wa simu.

Dk Mgimwa alisema fedha hizo
zitakazokusanywa zitaongeza
upatikanaji wa maji vijijini,
umeme pamoja na kuboresha
miundombinu katika maeneo
ya vijijini.