MAJIRANI WAZUNGUMZIA KIWANDA CHA KUTENGENEZA SILAHA DAR

Mtuhumiwa aliyekamatwa na
polisi Julai 18 kwa tuhuma za kumiliki kiwanda
cha silaha nyumbani kwake maeneo ya Kawe
Mzimuni alifahamika na majirani zake kama
fundi funguo.


Juzi, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
ilitangaza kumshikilia mtu mmoja kwa tuhuma
za kumiliki kiwanda cha kutengeneza silaha
nyumbani kwake kinyume na sheria.


Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Ally
Mlege alisema taarifa za uwapo wa kiwanda
hicho walizipata baada ya kukamtwa kwa
watuhumiwa wanne wa ujambazi.


Wakizungumza kwa masharti ya kutokutaja
majina, majirani hao walisema kijana huyo
alikuwa akiishi katika nyumba ya familia pamoja
na wazazi na mkewe, na alizoeleka mtaani kwa
jina la Makufuli na watu wengi walijua
kutengeneza funguo ndio kazi yake iliyokuwa
ikimpatia kipato.


Walisema alikuwa ni kijana wa kawaida na
alikuwa akijumuika na vijana wengine wa
mtaani kama kawaida na hawakuwahi kufikiria
wala kuhisi alikuwa akijihusisha na biashara
yoyote haramu katika nyumba hiyo ikiwamo
kumiliki vifaa vya kutengenezea silaha kama
SMG na Shotgun, zaidi ya ile ya ufugaji wa
ngo'mbe inayofanywa na familia hiyo
Wakielezea kukamatwa kwake mmoja wa
majirani hao, alisema siku ya tukio majira ya saa
sita mchana waliona magari yakienda katika
nyumba hiyo inayotazamana na Shule ya Msingi
Kawe A na baadaye kuzuka purukushani
zilizodumu kwa takribani muda wa saa mbili.


Walisema baadaye mtuhumiwa pamoja na
mkewe walikamatwa kwa tuhuma hizo.
Walisema mtaa umekuwa kimya toka kutokee kwa tukio hilo kila mmoja akijaribu kutathimi ni kwa
namna gani mtuhumiwa huyo aliweza kufanya biashara hiyo kwa siri ikiwa nyumba hiyo iko katika eneo
la msongamano wa watu na pia karibu na uwanja ambao wanajeshi huwa wanafanyia mazoezi.


Jana nyumba aliyokuwa akiiishi mtuhumiwa ilionekana kuwa kimya huku mlango wa mbele ukiwa
umefungwa, na nje kukiwa na zizi la ng'ombe.


Nyumba za jirani watu walioneka nje wakifanya shughuli zao kama kawaida,lakini wengi wao wakiwa
makini kuongea.


Siku ya Jumanne Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam ilitangaza kumshikilia mtu mmoja kwa tuhuma
za kumiliki kiwanda cha kutengeneza silaha nyumbani kwake kinyume na sheria.


Kaimu kamanda wa polisi wa kanda Maalumu ya Dar es Salaam Ally Mlege alisema taarifa za kuwapo
kiwanda hicho walizipa baada ya kukamtwa kwa watuhumiwa wanne wa ujambazi.

Alisema majambazi hao walikamatwa baada ya
taarifa kutoka kwa wasamaria wema na katika
mahojiano walifanikiwa kupata taarifa za
kiwanda hicho.