ASKARI WANAFUNZI 117 WATIMULIWA

Wanafunzi 117 wa Polisi,
wamefukuzwa katika Chuo cha
Taaluma na Mafunzo ya Polisi
(MPA), kilichopo Manispaa ya
Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Waliotupiwa virago na kufutwa
kwenye kozi hiyo ni wale
waliopoteza sifa za kuendelea na
mafunzo ya kijeshi baada ya
kukutwa na makosa ya utovu wa
nidhamu, utoro na matatizo ya
kiafya.


Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP), Matanga Mbushi, ambaye ni
mkuu wa chuo hicho alisema
katika mahojiano maalumu
kwamba, waliotimuliwa chuoni ni
kati ya askari wanafunzi 3,189
waliokuwa wamesajiliwa kuanza
mafunzo ya kijeshi katika chuo
hicho, Oktoba 25 mwaka jana.


Kati yao askari 115 ni wale wa
Polisi na askari wawili wanatoka
katika Idara ya Uhamiaji iliyopo
chini ya Wizara ya Mambo ya
Ndani.


Kufukuzwa kwa wanafunzi hao ,
kuna akisi moja kwa moja jinsi
menejimenti ya chuo hicho
ilivyojipanga upya kupunguza
wimbi la baadhi ya askari walioko
kazini na ambao wanalipaka
matope jeshi hilo kutokana na
kupotoka kimaadili kwa kutaka
kujinufaisha kimaslahi.


Askari hao walikuwa waungane na
wenzao ambao wanatarajiwa
kuhitimu mafunzo ya awali ya
polisi na uhamiaji, Julai 26 mwaka
huu baada ya kupatiwa mafunzo
ya medani za kivita. Mgeni wa
heshima atakayeshuhudia kuagwa
kwa askari 3,092 ni Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.
Emmanuel Nchimbi.


Kamishna Mbushi alisema askari
hao pamoja na mambo mengine
wamepatiwa mafunzo maalumu ya
utunzaji wa amani ya nchi iliyopo,
Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (ICT), Haki za
Binadamu, Masuala ya mtambuka
(Cross cutting issues), Usimamizi
wa majanga na Usimamizi wa kazi
za Polisi.


Mafunzo mengine ni pamoja na
Polisi Jamii, Sheria ya ushahidi,
Sheria ya mwenendo wa makosa
ya jinai, Upelelezi wa makosa ya
jinai, Usalama barabarani na stadi
za kazi.


Taarifa za awali kutoka ndani ya
chuo hicho, zinaeleza kuwa
mahafali hayo ya Polisi
yatatanguliwa na medani za kivita
yatakayofanyika Julai 25 huko
katika Kijiji cha Kilele-Pori, Wilaya
ya Siha.


Credit: ipp media