KAGAME HUENDA AKATUPWA ICC

ONYO lililotolewa na Ikulu ya
Marekani dhidi ya Serikali ya
Rwanda, linalomtaka Rais wa nchi
hiyo, Paul Kagame, kuacha
kuwasaidia waasi wa kikundi cha
M23, lina kila dalili zinazomuweka
kwenye kundi la viongozi wa
Kiafrika ambao hatma yao baada
ya kuachia madaraka inazungukwa
na wingu la mashaka.


Rais wa Marekani, Barack Obama,
ambaye mapema wiki hii
alikaririwa na vyombo vya habari
mbalimbali duniani akimtaka Rais
Kagame kuacha kukisaidia kijeshi
kikundi cha waasi wa M23,
anaaminika kuitoa kauli hiyo
kama msimamo wa serikali yake
inayopinga watawala
wanaojihusisha na uhalifu wa
kivita.


Ingawa hadi sasa Rais Kagame
hajatajwa na Ikulu ya Marekani
kama mmoja wa viongozi wa
Afrika wanaotuhumiwa kwa
uhalifu wa kivita, onyo lililotolewa
na Rais Obama linadhihirisha
kuwepo kwa ushahidi
unaomhusisha na matukio ya aina
hiyo yaliyopata kuwagharimu
baadhi ya marais walionyooshewa
kidole na Marekani kwa aina hii
hii anayonyooshewa sasa Kagame.


Wadadisi na wafuatiliaji wa
mambo walioichambua kauli ya
Rais Obama, wanaeleza kuwa
aliitoa baada ya Marekani
kujiridhisha na ushahidi
ilioukusanya ukiihusisha Serikali
ya Rwanda kuwasaidia waasi wa
kundi la M23.


Wanaeleza kuwa Marekani baada
ya kubaini ushirika wa majeshi ya
Rwanda yaliyojipenyeza ndani ya
makundi ya waasi wanaopigana na
Serikali ya Kongo, huku
wakitekeleza vitendo vya kinyama
dhidi ya binadamu katika maeneo
ya mashariki mwa nchi hiyo yenye
utajiri mkubwa wa madini,
imeamua kumtosa Kagame,
ambaye amekuwa na uswahiba wa
muda mrefu na taifa hilo.


Katika tathimini yao kuhusu uzito
wa onyo la Rais Obama kwa Rais
Kagame, wanaeleza kuwa
hataweza kuepuka kitanzi cha
mashitaka katika Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita
(ICC).


Waasi wa kikundi cha M23, mbali
na kuendesha mapambano dhidi
ya majeshi ya Serikali ya Kongo,
jambo linalopingwa na jumuiya ya
kimataifa, pia wanatuhumiwa kwa
ubakaji na mauaji ya watu
wasiokuwa na hatia.


Tuhuma hizo pia zinaelekezwa
kwa majeshi ya Rwanda,
yanayodaiwa kushirikiana na
waasi hao na ndizo zinazomuweka
Rais Kagame katika hatari ya
kufikishwa mahakamani na hata
kuhukumiwa kama ilivyokuwa
kwa aliyekuwa Rais wa Liberia,
Charles Taylor, ambaye kwa sasa
anatumikia kifungo cha miaka 50
jela baada ya kupatikana na
makosa ya uhalifu wa kivita nchini
Sierra Leone ambako zaidi ya
watu 50,000 waliuawa katika vita
ya wenyewe kwa wenyewe na
wengine wengi wakiachwa na
ulemavu wa kudumu.


Kama inavyotokea kwa Rais
Kagame sasa, kwa Taylor pia
ilikuwa hivyo hivyo, pale
alipokuwa akionywa na jumuiya
za kimataifa na yeye kudharau
maonyo hayo.


Wakati wadadisi na wachambuzi
wa mambo wakiwa na mtizamo
huo kuhusu onyo la Serikali ya
Marekani dhidi ya Rais Kagame
kujiingiza kijeshi katika vita vya
ndani ya Kongo, ushahidi
uliokusanywa na taasisi za Umoja
ya Mataifa za kutoa misaada ya
kibinadamu unaonyesha kuwa
wanajeshi wa Rwanda
wanaopigana bega kwa bega na
waasi wa M23 wamekuwa
wakijihusisha na vitendo vya
kihalifu dhidi ya binadamu.


Ni ushahidi wa aina hiyo ndio
uliotumiwa na ICC, kumhukumu
Taylor, aliyekuwa akituhumiwa
kuvisaidia vikundi vya waasi vya
Revolutionary United Front (RUF)
na Armed Forces Revolutionary
Council (AFRC) kwa kuvigawia
silaha za kivita kwa muktadha wa
kupewa madini ya almasi.


Stephen Rapp, mchambuzi wa
sheria za makosa ya jinai wa
Marekani, katika mahojiano yake
na gazeti la The Guardian la nchini
Uingereza, alieleza kuwa uongozi
wa Serikali ya Rwanda una tuhuma
za kujibu katika Mahakama ya ICC,
kuhusu mapigano yanayoendelea
Mashariki mwa Kongo.


Kauli hiyo ya Rapp inaunga mkono
madai ya mara kwa mara ya
mashirika ya kimataifa
yanayojihusisha na utetezi wa haki
za binadamu ya Human Right
Watch, Save the Children, UNICEF
na UNHCR, ambayo kwa nyakati
tofauti yamekuwa yakidai kuwa na
ushahidi wa kutosha wa waasi wa
M23 kusaidiwa na Jeshi la Rwanda
kufanya mauaji ya raia wasiokuwa
na hatia katika miji mbalimbali ya
Mashariki mwa Kongo.


Inadaiwa pia kuwa upo ushahidi
unaoonyesha jinsi ambavyo waasi
wa M23 wamekuwa wakiwatumia
watoto wadogo katika vikosi vya
majeshi na ndio ambao
wamekuwa wakitangulizwa mstari
wa mbele katika uwanja wa
mapambano, hususan katika
matukio ya uhalifu wa kivita.


Tuhuma nyingine zinazoelekezewa
Serikali ya Kigali ni kufadhili kundi
la waasi la CNDP, lililokuwa chini
ya uongozi wa Jenerali Bosco
Ntaganda, ambaye amejisalimisha
kwenye Mahakama ya ICC
mapema mwaka huu.


Sehemu kubwa ya wapiganaji wa
kundi la Ntaganda sasa
wameungana na waasi wa kundi la
M23 na wamekuwa wakijiimarisha
kiulinzi katika maeneo yenye
utajiri mkubwa wa madini nchini
Kongo.


Source:Mtanzania