JAJI AJITOA KESI YA MAUAJI YA PADRI MUSHI HUKO ZANZ

Kesi ya mauaji ya Padri Evarist
Mushi imechukua sura mpya,
kufuatia Jaji wa Mahakama kuu ya
Zanzibar, Mkusa Isaac Sepetu
kujitoa baada ya upande wa
utetezi kuwasilisha ombi la
mshatikiwa Omar Mussa Makame
kutokuwa na imani naye.

Akisoma uamuzi baada ya
kupokea maombi ya upande wa
utetezi, ambayo yaliwasilishwa
Julai 2 mwaka huu, Jaji Mkusa
amesema kwamba uamuzi wa
mshtakiwa ni haki yake kwa
mujibu wa sheria lakini amesema
hakubaliani na hoja zilizotolewa
na Wakili Abdallah Juma
Mohamed.

Wakili Abdallah Juma Mohamed
aliwasilisha hoja tatu, akimtaka
Jaji Mkusa ajiondoe katika kesi
hiyo, kuutaka upande wa
waendesha mashtaka wapewe
muda maalum wa kukamilisha
upelelezi wa kesi hiyo na
kuwasilisha mahakamani ili kesi
hiyo iweze kusikilizwa kwa muda
muafaka.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Mkusa
amesema hoja zote
zilizowasilishwa hazina msingi
wowote, na
kinachoonekana kwa upande wa
utetezi unajaribu kuiburuza
mahakama ikiwemo kuchagua Jaji
wa kusikiliza kesi hiyo kwa vile
hoja za kumtaka kujiondoa
hazikuzingatia mashiko ya
kisheria.

Jaji Mkusa amesema suala la
mshtakiwa kunyimwa dhamana
lipo wazi kwa mujibu wa sheria
ambapo makosa ya mauaji hayana
dhamana lakini wakili wa utetezi
wamekuwa akiwasilisha ombi la
kutaka mteja wake aachiwe huru
kila wakati kesi inapotajwa wakati
jambo hilo limeshatolewa uamuzi
zaidi ya mara tatu.

Jaji Mkusa amesema baada ya
uamuzi wake wa kujitoa, jalada la
kesi hiyo litarudishwa kwa Jaji
Mkuu kwa ajili ya taratibu za
kupangiwa Jaji mwingine, na kesi
hiyo imeahirishwa hadi Agosti
mosi mwaka huu.

Mtuhumiwa Omar Mussa Makame
anakabiliwa na shtaka la kumuua
Padri Evarist Mushi mnamo
Febuari 17 mwaka huu katika eneo
la Beitrasi kwa kumpiga risasi
kinyume na kifungu cha 196 na
197 cha sheria namba 6 ya mwaka
2004 ya mwenendo wa makosa ya
jinai ya Zanzibar.