HOUSE BOY ATUPWA JELA MAISHA KWA KUMLAWITI MTOTO

Mahakama  ya Hakimu Mkazi ya
Wilaya ya Mpanda Mkoa wa
Katavi imemhukumu kijana,
Baraka  Juma (22) mkazi wa kijiji
cha Nkungwi wilayani humo,
kifungo cha maisha jela  baada ya
kupatikana na hatia ya kosa la
kumlawiti mtoto wa kike mwenye
umri wa  miaka minne  baada  ya
kumhadaa na kumlewesha bia.

Akisoma  hukumu hiyo juzi,
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Chiganga Tengwa
alisema ameridhishwa na
ushahidi pasipo kutia shaka
uliotolewa mahakamani hapo na
upande zote  mbili za mashitaka
na utetezi.

“Nimelazimika kutoa adhabu kali
kwa mshtakiwa baada ya
mahakama  hii kumtia hatiani  ili
iwe  fundisho si kwake  tu, lakini
pia kwa wengine wenye tabia
kama  yako .... kitendo
ulichomtendea mtoto  huyo ni
cha kinyama hustahili kuonewa
huruma, “ alisema Tengwa.
Awali Mwendesha Mashitaka,
Mkaguzi wa Polisi, Lazaro
Masembo alidai mahakamani hapo
kuwa mshitakiwa alitenda kosa
hilo Aprili 2 mwaka huu nyumbani
kwa wazazi wa mtoto huyo
ambako mtuhumiwa alikuwa
ameajiriwa na wazazi wake kama
mfanyakazi wa ndani.

Ilidawa  mahakamani  hapo kuwa
siku hiyo  ya tukio mama mzazi wa
mtoto huyo alikuwa amekwenda
kijiji cha jirani kutembelea ndugu
zake ambapo alimwacha mtoto
wake huyo  chini ya uangalizi wa
mshitakiwa.

Pia nyumbani hapo  ilidaiwa
mahakamani  hapo kuwa
kulikuwa  na  msichana  aitwaye
Nyasolo Doya (18 ) ambaye
alikuwa mgeni wa nyumba hiyo
ambaye alifikia hapo kujifungua.

Kwa mujibu wa Mwendesha
Mashtaka, Masembo, mtuhumiwa
alimwita mtoto huyo  sebuleni
ambako alikuwa amekaa na kisha
akaanza kunywesha bia aina ya
Balimi kisha  akamlawiti  huku
mtoto akipiga kelele kwa
maumivu akisikika akisema,
“mama  nakufa.”

Mahakama  hiyo  ilielezwa kuwa
kufuatia kelele za kilio cha
mtoto huyo, msichana Nyasolo
Doyo  alishtuka na kulazimika
kukimbilia  sebuleni ndipo
alipomshuhudia  mshitakiwa
akimwingilia mtoto  huyo huku
akiwa amevua  nguo zake.
Mwendesha Mashtaka Masembo
alisema Nyasolo alipomsihi Baraka
amwachie mtoto huyo aligeuka
‘mbogo' na kumtishia  kuwa iwapo
atatoa siri  hiyo kwa wazazi wa
mtoto huyo  atamuua, ndipo
msichana huyo aliponywea kwa
hofu ya tishio  hilo la kuuawa.

Mahakama hiyo  ilizidi
kufahamishwa kuwa mama mzazi
wa mtoto huyo alirejea nyumbani
kwake saa mbili usiku na ndipo
alipomwona binti yake  huyo
akitembea kwa kuchechemea
mwendo  uliomshtua  mama  huyo
na akaamua kumuuliza msichana
Nyasolo ambaye alimsimulia
mkasa wote huo wa kusikitisha.

Mwendesha Mashtaka alidai
mahakamani hapo kuwa mama
huyo alilazimika kumpigia simu
baba mdogo wa mtoto huyo
ambae anaishi kijiji cha jirani
ambae alifika nyumbani  hapo saa
nane usiku na ndipo walipoamua
kumfungia mtuhumiwa  mlango
wa chumba chake kwa nje na kisha
walienda kutoa taarifa kwa
uongozi wa kijiji.

Katika shauri hilo upande wa
mashtaka ulikuwa na mashahidi
watano mmojawapo akiwa daktari
aliyemfanyia  uchunguzi wa
kitabibu mtoto huyo na
kuthibitisha kuwa alikuwa
ameingiliwa na mwanaume katika
sehemu zake za siri ambapo
mshitakiwa hakuwa na shahidi
yeyote.

Katika utetezi wake, mshitakiwa
aliiomba mahakama imwachie
huru kwa kile alichokieleza kuwa
alisingiziwa tu.