WAFANYAKAZI TRL WATISHIA KUGOMA

WAFANYAKAZI wa Kampuni
ya Reli nchini (TRL)
wametishia kuingia katika
mgomo kwa kile walichodai
uongozi wa kampuni
kushindwa kutekeleza maombi
yao, ikiwa ni pamoja na
mkataba wa hali bora,
nyongeza ya mshahara na
kuwaondoa wazee ambao
wameshastaafu, lakini
wanaendelea kufanya kazi kwa
mkataba.


Kwa sasa, Chama cha
Wafanyakazi wa Reli (TRAWU)
kiko katika hatua za mwisho
za maandalizi ya shauri kwa
ajili ya kuwasilisha Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi Mahala
pa Kazi (CMA) kesho.


Akizungumza na gazeti hili
jana, Mwenyekiti wa TRAWU
Kanda ya Dar es Salaam, Shehe
Shughuli alisema wako katika
maandalizi ya mwisho na
kwamba kesho watawasilisha
CMA shauri lao kutokana na
kile kilichoelezwa wafanyakazi
wa TRL kutoridhika na
maamuzi ya mwajiri wao.


Juzi, viongozi wa TRAWU
walikutana na wafanyakazi ili
kuwapa taarifa juu ya kikao
walichokaa na uongozi wa
kampuni Julai 18 na 19 mwaka
huu katika baraza la
majadiliano ambapo madai ya
wafanyakazi yalijadiliwa, hata
hivyo maombi ya wafanyakazi
yaligonga mwamba.


Majibu
hayo yalipokelewa vibaya na
wafanyakazi waliopaza sauti
wakitaka uitishwe mgomo.


Walielezwa kuwa uongozi
umekataa kuongeza mishahara
yao kutoka Sh 200,000
wanayolipwa sasa kwa kima
cha chini hadi Sh 500,000
walichokiomba.

Hata hivyo
uongozi haukutaka kufanya
maongezi kwa madai kwamba
hakuna fedha. Aidha, suala la
kuwaondoa wastaafu katika
ajira ya mkataba liliibua
manung'uniko, ikidaiwa wazee
waliostaafu bado wapo kazini
wanawazuia wafanyakazi
walioko masomoni na wengine
waliohitimu kushindwa
kupandishwa vyeo, kwani
wanaofanya kazi kwa mkataba
hawataki kuachia madaraka.


Kuhusu mkataba wa hali bora,
TRAWU ilipeleka
mapendekezo 21 lakini ni
mapendekezo mawili
yaliyopita ambayo ni likizo ya
wanaume, wake zao
wanapojifungua kwa kupata
likizo ya siku nne na pia
mfanyakazi atakapoumia
kazini aweze kulipwa.


"Tulipendekeza mfanyakazi
atakapostaafu apewe
mishahara ya miezi mitatu
mara miaka aliyokaa kazini
lakini imekataliwa wao
wakataka iondolewe kabisa
wakati iliyokuwepo ni kupata
mshahara wa mwezi mmoja
mara miaka yako kazini,"
alisema Shughuli.

Alisema
wafanyakazi hawakuridhishwa
na maamuzi ya uongozi hivyo
siku yoyote watagoma baada
ya kupata taratibu zote za
kisheria kwa sababu maombi
yao yote yamekataliwa.