Mapya Yafichuka Mabomu ya Arusha

*Wataalamu kutoka China watua
kuchunguza
*Polisi watamba kufichua siri ya
milipuko yote
TAARIFA za awali kutoka kwa
makachero wa Jeshi la Polisi nchini
zimefanikiwa kubaini mtandao wa
ulipuaji mabomu katika jiji la
Arusha, imefahamika.

Mpaka sasa
taarifa zinadai mtandao uliohusika
na milipuko miwili iliyotokea kwa
nyakati tofauti jijini hapa ulipangwa
ndani ya jiji la Arusha.

Mlipuko wa kwanza ulitokea katika
Kanisa la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, Olasiti, Mei 5, mwaka
huu na kuua watu watatu, wakati
mlipuko wa pili ulitokea Uwanja wa
Soweto Juni 15, mwaka huu na kuua
watu wanne, huku majeruhi wa
matukio yote wakifikia zaidi ya 100.

Akizungumza katika kikao cha
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa
Arusha (RCC) jana jijini hapa, Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Magesa
Mulongo, alisema mbinu hizo
zimejulikana kutokana na wananchi
waliojitokeza kuwasilisha ushahidi
kwa vyombo vya dola.

Alisema mpaka sasa ushahidi
unaonyesha kuwa mtandao wa
waliolipua wa mabomu hayo
ulianzia jijini Arusha, na kikubwa
kabisa wanawashukuru wakazi wa
Arusha waliokuwa wakifika kutoa
ushahidi wa wahusika.

"Ukweli wa mambo haya utajulikana
hivi karibuni na Serikali itamchukulia
hatua mtu yeyote atakayebainika
kuhusika na mtandao huo, bila
kujali wadhifa wake.

Mambo haya
yamedhalilisha na kufedhehesha
Taifa," alisema Mulongo.

Akiwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa,
aliendelea kubainisha kuwa
upelelezi wa matuko hayo mawili
unaendelea kwa umakini mkubwa
na kikubwa kinachoangaliwa ni
kuepuka kukamata watu
wasiohusika.

"Tunachukua umakini ili waliofanya
hivi vitendo vya kinyama
wasiendelee kutamba, kwani
wanajua tukikamata wasiohusika
wao watajiona wameshinda
hawajakamatwa," alisema Mulongo.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa
aliwataka pia wanasiasa nchini
kutoigeuza milipuko ya mabomu
hayo kama njia ya kujitafutia
umaarufu wa kisiasa.

"Kugeuza tukio hili la kinyama kuwa
agenda ya kisiasa kunaidhalilisha
Tanzania nje ya nchi na kuleta athari
za kupoteza wageni," alisema
Mulongo.

Mulongo alisema taarifa za awali za
kikachero zinaonyesha kuwa bomu
lililorushwa katika viwanja vya
Soweto lilitengenezwa China.

Mkuu huyo wa mkoa alisema, tayari
wataalamu kutoka China
wamekwisha wasili jijini Arusha kwa
ajili ya kufanya utambuzi wa taasisi
iliyonunua bomu hilo.

Mulongo katika hotuba yake
aliendelea kuwataka wanasiasa
kuacha dharau na kueneza maneno
yasiyo na ukweli juu ya Serikali,
badala yake aliwataka kuheshimu
taratibu za nchi ili vyombo vya dola
visilazimike kutumia nguvu
kukabiliana na watu au kikundi
kitakachovunja sheria zilizowekwa.

"Hivi ndugu zangu, lazima tufike
mahali tujiulize hawa wanasiasa
wanaotumia uongo na nguvu nyingi
kuchafua nchi huko duniani,
wanafanya hivi kwa faida ya nani?"
alihoji Mulongo.

Bomu hilo lilirushwa katika mkutano
wa Chama cha Demokrasia na
Maendelo (CHADEMA), wakati
kikihitimisha kampeni zake za
uchaguzi mdogo wa udiwani katika
kata nne jijini Arusha Juni 15, mwaka
huu.

Hata hivyo, siku mbili baada ya
mlipuko huo, chama hicho kilitoa
shutuma nzito dhidi ya Jeshi la
Polisi na kueleza kuwa askari wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),
ndiye aliyerusha bomu hilo.

Mwenyekiti wa chama hicho taifa,
Freeman Mbowe, aliwaeleza
waandishi wa habari kuwa chama
chake kinao ushahidi wa picha na
sauti unaothibitisha kwamba polisi
ndio wahusika wa mlipuko huo.

Hata hivyo, chama hicho kimegoma
kukabidhi ushahidi huo kwa jeshi
hilo kwa maelezo kuwa ushahidi
huo hauwezi kutolewa kwa polisi,
ambao ni watuhumiwa wa tukio
hilo.

Chama hicho kilitoa sharti kwa Rais
Jakaya Kikwete kuunda Tume ya
Mahakama itakayohusisha majaji
waadilifu na kusema kuwa kipo
tayari kutoa ushahidi huo mbele ya
tume hiyo na si polisi.

Mbali na bomu hilo, bomu jingine
lilirushwa katika Kanisa la Mtakatifu
Joseph Mfanyakazi, Olasiti na
kusababisha watu watatu kufariki
ambapo nalo liligundulika
kutengenezwa nchini Urusi.