Birthday ya Mandela yapangwa

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
ameambia taifa hilo lianze kujiandaa
kwa sherehe ya siku ya kuzaliwa ya
Mandela tarehe 18 mwezi Julai.
Mandela ambaye anaheshimika sana
kote duniani, atafikisha umri wa miaka
95,lakini kwa sasa angali mahututi
hospitalini mjini Pretoria.

Alilazwa hospitalini tarehe 8 mwezi
Juni akiwa na maradhi ya mapafu.
Kauli ya Zuma inakuja baada ya mke
wa zamani wa Mandela Winnie
Mandela, kukashifu chama ha ANC
kwa kumnasa kwa video Mandela,
walipomtembelea kwake nyumbani
mwezi Aprili.

Kanda hiyo ilionyesha Mandela akiwa
na mshangao na bila ya tabasamu
wakati wa ziara ya mmoja wa vigogo
wa ANC nyumbani kwake.
Winnie Madikizela-Mandela, alisema
"kweli siwezi kueleza ambavyo familia
ilihisi uchungu kuhusiana na kanda
hiyo, na haikupaswa kwa jambo hilo
kufanyika.''

Ikijibu tuhuma hizo, chama cha ANC
kilitetea ziara hiyo, kikisema kuwa
haikuwa na njama ya kutaka kujitafutia
umaarufu.

Hapo Jumatatu, rais alitoa taarifa
kusema kuwa wananchi wa Afrika
Kusini waanze kujiandaa kwa sherehe
za kuzaliwa kwa Madiba.

"lazima sote tufanye angalau jambo
zuri kwa sababu ya utu kwa siku hiyo
kama ujumbe wetu mzuri kwa
Mandela,'' alisema Zuma.

Mandela anasifiwa sana kwa
kuongoza vita dhidi ya utawala wa
ubaguzi wa rangi, nchini Afrika Kusini
na kisha kuhubiri maridhiano licha ya
kufungwa jela kwa miaka27.

Alituzwa tuzo ya amani ya Nobel
mwaka 1993 na kisha kuchaguliwa
kama rais mwaka uliofuata.

Aliondoka
mamlakani mwaka 1999 baada ya
kutawala kwa muhula mmoja.