Tanzania Yamjibu Kagame

SERIKALI ya T anzania imeipa
onyo kali nchi ya Rwanda
ikiitaka isijaribu kuota ndoto za
kuishambulia kijeshi,
vinginevyo itajibu mapigo kwa
nguvu zote na kuhakikisha
kuwa imeichakaza.
Kauli hiyo ya kwanza nzito
imetolewa jana na Wizara ya
Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa
Kimataifa kufuatia taarifa ya
matamshi makali yanayodaiwa
kutolewa na Rais Paul Kagame wa
Rwanda, dhidi ya Rais Jakaya
Kikwete na kutishia kuishambulia
Tanzania.

Akizungumza na Tanzania Daima
jana jijini Dar es Salaam,

Msemaji
wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally,
alisema ingawa Serikali ya
Tanzania hadi sasa inajua haina
ugomvi wowote na Rwanda, lakini
amekiri kuwapo kwa kile
alichokiita 'kupishana lugha' kwa
Rais Jakaya Kikwete na Paul
Kagame.

Mkumbwa alikiri Serikali ya
Tanzania kunasa matamshi
yanayodaiwa kutolewa na Rais
Kagame katika moja ya hotuba
zake aliyoitoa Juni 30, nchini
kwake wakati akihutubia katika
hafla moja ya vijana.

Kwa mujibu wa hotuba hiyo,
ambayo kwa wiki sasa
imesambazwa katika baadhi ya
mitandao ya kijamii, Kagame
anadaiwa kusikika akitoa
matamshi ya vitisho dhidi ya Rais
Kikwete, kwamba anamsubiri
katika wakati aujuao na
kumchapa.

Baadhi ya maneno yanayodaiwa
Rais Kagame aliwaambia vijana
waliokutana katika mkutano wao
uliojulikana kama 'Youth Konnect'
na kufadhiliwa na mke wake,
Janet Kagame, yanasema: "Huyu
mtu mliyemsikia akiwa upande
wa Interahamwe na FDLR na
akashauri
majadiliano….majadiliano?"
Aidha, Kagame anadaiwa kusema
kuwa hatakuwa tayari kujadili
jambo hilo, isipokuwa atamsubiri
Rais Kikwete sehemu muafaka na
'kumtandika'.

"Sitapoteza muda wangu
kumjibu Kikwete, inajulikana
maana kuna mahali hataweza
kuvuka…haiwezekani,"
alikaririwa akisema Rais Kagame,
akilenga kumtisha Rais Kikwete.


Mbali na Kagame, baadhi ya
viongozi kadhaa wa serikali ya
Rwanda wamekuwa
wakimshambulia Rais Kikwete
wakimpachika majina ya kejeli ya;

"Rais mhurumia magaidi,
wauaji wa kimbari, mkorofi na
mwenye dharau."

Mkumbwa hata hivyo alisema
Serikali ya Tanzania haina sababu
ya kuingia katika vita na Rwanda,
kwa sababu tu ya ushauri alioutoa
Rais Kikwete wa kuitaka ikutane
na wapinzani wake wanaoishi
ndani ya nchi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC),
kujadiliana kuhusu amani ya nchi
za Maziwa Makuu.


Alisema msimamo wa Tanzania
utabaki kuwa uleule wa kuitaka
nchi hiyo ikubali kukaa meza
moja na wapinzani wake, ili
kumaliza migogoro inayoendelea
katika nchi hizo za maziwa
makuu, ambao unaungwa mkono
na jumuiya ya kimataifa na SADC.

"Unajua mgogoro wa DRC na
Rwanda hauwezi kumalizika
bila ya nchi hizo kukaa meza
moja na wapinzani wao ili
kupata suluhu ya kudumu,"
alisema Mkumbwa.

Aliwataka Watanzania kuwa
watulivu na kuendelea na kazi zao
kama kawaida, kwani serikali yao
iko makini katika kulinda mipaka
yake.


Chanzo cha mzozo
Msuguano baina ya nchi hizi mbili
ulianza siku chache tu baada ya
kumalizika kwa kikao cha
viongozi wa nchi za Maziwa
Makuu na ambacho kilihudhuriwa
pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Ban Ki-Moon, chini ya
uenyekiti wa Rais wa Uganda,
Yoweri Museveni.


Rais Kikwete wakati akimtaarifu
Rais Museveni kile walichokuwa
wamekijadili katika kikao hicho
kwa vile aliketi kwa muda kwa
kuwa alichelewa kuwasili, alisema
ni vema serikali za Rwanda na
Uganda zifungue mlango wa
mazungumzo na waasi wao na
akaanza kutaja majina ya vikundi
vya uasi vya nchi hiyo vilivyopo
nchini DRC.

Habari zinasema kauli ya Rais
Kikwete iliungwa mkono na Rais
Museveni akisema: "Bila
mazungumzo hatutafika popote
pale".


Hata hivyo, matamshi hayo
yalijibiwa kwa ukali na serikali ya
Rwanda, kiasi cha kumlazimu
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, kutoa tamko bungeni.


Kwa kauli yake, Membe alisema
serikali ilikuwa imeshangazwa na
shutuma hizo za Rwanda kwani
halikuwa jambo baya kutoa
ushauri uliolenga kuleta mapatano
na kuepusha umwagaji zaidi wa
damu wa wananchi.

Akaongeza kuwa, ilikuwa ni
wajibu wa Serikali ya Rwanda
kuupokea ama kuukataa, na wala
si kutoa maneno ya kejeli na
vitisho.


Kauli ya Zitto

Akizungumzia kauli hiyo ya
vitisho, mwanasiasa machachari
hapa nchini na Naibu Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Zitto
Kabwe, alisema ushauri wa Rais
Kikwete kwa Rwanda ulikuwa wa
busara mno na akashangaa kuona
nchi hiyo jirani ikitoa vitisho,
kejeli, dharau na ukosefu wa
adabu kwa Kikwete.


Katika moja ya tamshi lake
alilolitoa jana katika mitandano ya
kijamii, Zitto ambaye ni Mbunge
wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA)
alisema Marekani wanaongea na
waasi wa kundi la Taliban, hivyo
hakuna dhambi kwa Rwanda pia
kufanya hivyo.


"Pia kama hutaki ushauri si
unakataa tu, sasa kuanza
kurushiana maneno ya nini
tena? Hutaki ushauri basi.

Maneno ya kila siku ya nini?
Tangu Kikwete amesema kule
Addis, hajasema tena.


Membe
(waziri) akajibu Dodoma Tanzania
haijasema tena. Kigali inasema
mambo haya kila siku kwa ajili ya
nini?

"Taliban na Al Qaeda si wale
wale? Wale watoto waliozaliwa
mwaka 1994 na wakimbizi wa
Kihutu waliopo Kongo nao ni
wauaji? Tufikiri vizuri mambo
haya. Kuna 'genociders'
wasakwe, wakamatwe
wahukumiwe. Kuna watu wana
haki kabisa ya kutaka kushiriki
kwenye siasa za Rwanda na
wanazuiwa, wameshika silaha.

Hawa lazima wakae meza moja
wakubaliane," alisema Zitto.


Mwanasiasa huyu alisema kwa
sasa serikali za nchi hizo mbili
zinatakiwa kuingia katika vita ya
kupambana na kuondoa umasikini
wa watu wake na si vita ya mtutu
wa bunduki.

"Busara itumike kwa viongozi
'neutral' kama Uhuru Kenyatta
kuwaweka pamoja Kagame na
Kikwete wamalize tofauti zao.

Haya maneno hayana maana
yoyote," alisema.


Alisema vita haitamuumiza Rais
Kagame wala Rais Kikwete na
familia zao, bali itaumiza
wananchi wa kawaida wa mikoa
ya Kagera na Kigoma na mikoa ya
mpakani ya Rwanda.

"Vita itaturudisha nyuma sana
kwenye juhudi za maendeleo.

Vita itazima harakati za
kujenga demokrasia nchini.
Busara itumike tu ," alisema
Zitto.