MZIMU wa serikali tatu bado
unaendelea kukitesa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), ambapo jana,
Katibu Mkuu wa Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye, alipinga tena uwepo
wa serikali tatu na kudai kuwa
waliotoa maoni hayo ni wazee
wanaosubiri kufa.
Akizungumza jijini
Dar es Salaam katika kongamano la
Umoja wa Vijana (UVCCM) la kujadili
mchakato wa Katiba Mpya, katika
ukumbi wa Arnatouglo, Nnauye
alisema nia ya serikali tatu ni kuleta
matabaka ambayo yatasababisha
migogoro.
"Wazee hawa wanaosubiri kufa
wanataka kutuletea matabaka, vijana
ndio nguvu kazi ya taifa, kitendo cha
kuwepo kwa serikali tatu ni
kusababisha mgogoro, kwa nini
wasingevunja Muungano enzi za
ujana wao? Wamenufaika na
Muungano kwa kipindi cha miaka
50, sisi vijana wanataka kutuachia
mgogoro!"alisema Nnauye.
Nape alisema kuvunjwa kwa
Muungano kutasababisha mgogoro
mkubwa wa rasimu kutokana na
muda ambao Muungano huo
umedumu.
Alisema kuundwa kwa serikali tatu si
sera ya CCM kama wanavyodai
wapinzani, bali ni maoni ya watu
waliyoyawasilisha katika ukusanywaji
wa maoni ya Rasimu ya Katiba
mpya.
"Sera ya CCM ni kuongoza serikali
mbili na si tatu, na hii sera
tutaendelea kuitetea na kuilinda
mpaka mwisho wa dunia,
tunachoamini katika chama chetu
hatuogopi kutetea sera ambazo
tumezitoa wenyewe," alisema
Nnauye.
Alisema ni vyema zikamalizwa
kasoro zilipo katika mfumo wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na
si kuongeza madaraka yasiyo na tija.
Nape alisema kitendo cha Tume ya
Jaji Joseph Warioba kusema
imetumia sheria ya mwaka 1964
kuwa kigezo cha kuundwa kwa
serikali tatu si sahihi, kutokana na
makubaliano ya mwaka huo
kwamba ni serikali mbili.
Kiongozi huyo wa CCM pia
alishangazwa na kitendo cha Rasimu
ya Katiba mpya kutamka wazi idadi
ya mikoa pamoja na wilaya ambazo
zitatumika katika uchaguzi na
kwamba mwenye jukumu hilo ni
Rais Jakaya Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
"Serikali ya Muungano chini ya
mfumo wa serikali tatu itaelea katika
madaraka, kwani serikali ya
Tanganyika itakuwa haiwezi
kuwatetea wananchi, hali
itakayosababisha kuwepo kwa
mgogoro mkubwa wa urasimu
ambao ni adui wa maendeleo,"
alisema Nnauye.
Aidha alisema kuwa kuvunjika kwa
Muungano kutasababisha kuiburuza
Serikali ya Zanzibar kiuchumi, kwani
asilimia 95 ya uchumi wa visiwani
unategemea Tanzania Bara.
Alisema kuwa sera nzuri ya kuwa
kiongozi ni kuwatetea wananchi na
si kuwazidishia mizigo.
Akizungumzia suala la mgombea
binafsi, Nnauye alisema CCM
hakiogopi mgombea binafsi, kwani
hata akigombea chama hakitapata
hasara yoyote.
Nape alisema sera ya CCM ni
kukataa wagombea binafsi
wanaouza unga na si kukataa
mgombea binafsi kama ambavyo
vyama vingine vya siasa vinavyodai
katika vyombo vya habari.
Alisema katika Rasimu hiyo sura ya 9
inazungumzia umri wa Mbunge
kuwa kuanzia miaka 25, lakini kwa
CCM suala hilo si sahihi, kwani
wabunge wenye miaka 21
wanawajibika vizuri kuliko wazee.
Kufuatia kauli hiyo mmiliki wa makampuni ya IPP Mzee Reginard Mengi amejibu kwa Kutweet.
Chanzo:Mwananchi