SHEKHE AMWAGIWA TINDIKALI.

Shekhe Mkuu wa Wilaya ya
Arumeru, Said Juma Makamba
amejeruhiwa vibaya kwa
kumwagiwa maji yanayohisiwa
kuwa tindikali na watu
wasiojulikana juzi usiku akiwa
nyumbani kwake jijini Arusha.


Shekhe Makamba, ambaye
amelazwa katika Wodi ya
Majeruhi kwenye Hospitali ya
Mkoa wa Arusha ya Mount Meru,
amejeruhiwa vibaya maeneo ya
usoni, kifuani na mgongoni huku
akiendelea na matibabu.


Akizungumza kwa tabu, shekhe
huyo alisema tukio hilo lilitokea
saa 5 usiku wa kuamkia jana
nyumbani kwake kwa Mromboo
Arusha, wakati akijiandaa kulala
baada ya kutoka kuswali Swala ya
Tarawei.


Shekhe Makamba ambaye pia ni
Imamu wa Msikiti wa Sekei mjini
Arusha, alisema baada ya swala
hiyo alirejea nyumbani kwake
akisindikizwa na vijana wawili
ambao walikuwa wakiswali
pamoja na kuingia ndani ya
nyumba yake ili kulala.

Alisema hata hivyo, kabla ya kulala
alikwenda kujisaidia katika choo
cha nje na kwamba wakati akirudi
ili aingie ndani akipitia nyuma ya
nyumba ghafla alimuona mtu
akiwa amesimama jirani na
mlango.


Alieleza kuwa wakati akitaka
kumwangalia zaidi alishtukia mtu
huyo akiinua mkono na kumwagia
maji yaliyompatia maumivu
makali usoni na kifuani.


''Wakati natoka msalani
nikipitia uwani kwangu niliona
kama mtu ameinama pembeni
yangu wakati najaribu
kumsogelea ili nijue ni nani
nilihamaki mtu huyo
akinimwagia maji
yaliyonisababisha maumivu
makali sana yenye asili ya moto
na ngozi kuanza kubabuka,''
alisema shekhe huyo.


Aliongeza kuwa baada ya tukio
hilo alianza kupiga kelele kuomba
msaada ambapo majirani
walijitokeza na kumpa msaada wa
kumpeleka hospitali, kwa vile
wakati huo macho yake yalikuwa
hayaoni na wakati wote alikuwa
akilia.


Pamoja na kujeruhiwa vibaya
sehemu za usoni, kifuani na
mgongoni, pia ana majeraha
kwenye mikono na machoni na
hali yake bado ni mbaya japo
madaktari wanaendelea kumpatia
matibabu.


Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa
wa Arusha, Abdallah Masoud
akizungumzia tukio hilo alieleza
kushitushwa nalo akisema
limefanana na lile la Katibu wa
Bakwata Mkoa wa Arusha,
Abdulaziz Jonjo ambaye mwaka
jana alilipuliwa kwa bomu
nyumbani kwake akiwa amelala.


Alisema kuwa matukio hayo
yamekuwa yakijirudia huku
wahusika wakishindwa kutiwa
mbaroni na kudai kuwa matukio
hayo yanahusiana na masuala ya
kigaidi. Aliongeza kuwa pamoja na
kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi,
lakini wamekuwa hawapati
matunda ya kukamatwa kwa
watuhumiwa ingawa alisema
wanajulikana.


Kwa upande wake, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus
Sabas alisema polisi wameanza
uchunguzi wa tukio hilo na
kwamba taarifa zitatolewa pindi
washukiwa watakapotiwa mbaroni
kwani uchunguzi bado unaendelea
na kwamba hakuna mtu
anayeshikiliwa hadi sasa.