MAJAMBAZI wapatao 10 waliokuwa
na silaha za kivita aina ya SMG 6
na LMG 2 wameteka magari
mbalimbali yakiwamo mabasi
mawili ya abiria na kupora
bunduki ya Jeshi la Polisi aina ya
SMG katika pori la Hifadhi ya
Biharamulo mkoani Kagera.
Akiongea na waandishi wa habari
ofisini kwake, Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Kagera, Philip
Kalangi, alisema tukio hilo
limetokea jana majira ya saa 2:30
asubuhi katika Kijiji cha
Kasindaga, eneo lijulikanalo
kama Mlima wa Simba kwenye
pori la Hifadhi ya Biharamulo.
Majambazi hao licha ya kupora
bidhaa mbalimbali za abiria,
walimpiga risasi na kumjeruhi
vibaya shingoni abiria mmoja
aliyefahamika kwa jina la
Frederick Rugahiula (47) mkazi wa
Bukoba, mkoani Kagera.
Kamanda Kalangi alitaja mabasi ya
abiria yaliyotekwa kuwa ni RS,
lenye namba za usajili T 495 AGT,
lililokuwa likitokea Bukoba
kuelekea jijini Dar es Salaam na
NBS T 644 BUR, lililokuwa
likitokea Bukoba kuelekea
Arusha.
Alisema baada ya kuteka mabasi
hayo majambazi hao
wanaoshukiwa kuwa ni raia wa
nchi moja jirani kutokana na
lafudhi ya maneno waliyokuwa
wakiongea, waliwashusha abiria
na kuwapora simu za mikononi
pamoja na fedha taslimu.
Pia
walipora bunduki ya Jeshi la Polisi
aina ya SMG yenye namba
14302551 iliyokuwa mikononi mwa
polisi.
Alisema wakati wakiwa katika
harakati za kuwapora abiria,
askari polisi waliokuwa katika basi
la Mohammed Trans lililokuwa
nyuma ya mabasi hayo,
waligundua kuwa wenzao
wametekwa, ndipo walipoanza
kuwashambulia majambazi hao na
kuzuka majibizano makali ya
risasi.
Kamanda huyo aliongeza kuwa
askari polisi wapatao wanne
waliokuwa wakisindikiza mabasi
hayo walizidiwa nguvu kutokana
na uchache wao, hivyo
wakaamuru kugeuza basi hilo na
kukimbia kwa ajili ya kutafuta
msaada zaidi.
Akielezea tukio hilo lilivyotokea,
Kamanda Kalangi alisema, kwanza
majambazi hayo yaliteka gari
dogo na kuzuia njia kana kwamba
limeharibika, hivyo mabasi
yalipofika yalilazimika kusimama
na ndipo yalipotekwa.
Hadi sasa hakuna mtu
aliyekamatwa kuhusiana na tukio
hilo na kuwa msako mkali
unaendelea kwa kushirikiana na
askari wa wanyamapori katika
eneo la Hifadhi ya Burigi na pori la
Biharamulo.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi
linahitaji ushirikiano wa pamoja
katika kukabiliana na matukio ya
uhalifu, kwa kuzingatia kuwa
watendaji wake ni wachache na
maeneo ni makubwa.