Rais Jakaya Kikwete amefanya
mazungumzo kwa njia ya simu na
Rais wa Sudan, Omar Bashir,
kuhusu kuuawa na kujeruhiwa
kwa askari wa Tanzania, walioko
katika ulinzi wa kimataifa wa
amani katika jimbo la Darfur.
Taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa
vyombo vya habari jana, imeeleza
kuwa katika mazungumzo hayo,
Rais Kikwete alimtaka Rais Bashir
kuchukua hatua za haraka
kuwasaka na kuwakamata
waliohusika na kitendo hicho
kiovu, na kuwafikisha mbele ya
sheria haraka iwezekanavyo.
Rais Bashir amekubaliana na Rais
Kikwete na kumuahidi kuwasaka
hadi kuwakamata wale wote
waliohusika na kuwachukulia
hatua za kisheria.
Alimueleza Rais Kikwete kuwa
binafsi anaamini waliohusika ni
wahalifu, kusisitiza kuwa lazima
watasakwa hadi kukamatwa na
kuchukuliwa hatua.
Alimpa pole Rais Kikwete kwa
tukio hilo la kusikitisha, ambapo
wanajeshi wa Tanzania walienda
nchini Sudan kulinda amani na
usalama wa wananchi wa Sudan.
Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN), Ban Ki-moon,
alimpigia Rais Kikwete na kumpa
pole kwa mkasa huo mkubwa na
wa kusikitisha, ambao
umewatokea Watanzania hao
wakati wakitekeleza jukumu lao la
kulinda amani nchini Sudan.
Hadi sasa hakuna kikundi
chochote kilichokiri kuhusika na
shambulio hilo, ingawa kumekuwa
na hali ya kutupiana lawama baina
ya vikundi vya kiserikali na vya
waasi katika jimbo la Darfur.
Mapigano baina ya vikundi vya
kikabila na koo mbalimbali,
yamesababisha mapigano na
uvunjifu mkubwa wa amani na
usalama katika jimbo la Darfur
kwa muda wa miaka 10 sasa.
Mara nyingi mapigano na tofauti
zao hizo zimesababisha vifo na
uvunjifu wa amani kwa wananchi
wa Sudan na wageni pia.
Mwishoni mwa mwaka jana
wanajeshi wanne kutoka Nigeria,
waliuawa karibu na El Geneina,
Magharibi mwa Darfur, ambapo
pia inaelezwa na AU kuwa
wanajeshi wapatao 50, wameuawa
tangu kikosi hicho cha Umoja wa
Afrika kinachoundwa kwa chini ya
Umoja wa Mataifa (UNAMID),
kianze operesheni yake mwishoni
mwa 2007.
Taarifa za UN pia zinaeleza kuwa
kabla ya mashambulizi
yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha
Tanzania Jumamosi iliyopita,
wanajeshi sita wanaolinda amani
waliuawa tangu Oktoba mwaka
huu, ambapo pia inasadikiwa
kuwa watu wapatao 300,000
wameyakimbia makazi yao.
Hata hivyo, kiini cha mgogoro huo
inasadikiwa kuwa ni ugomvi wa
ardhi na rasilimali zilizoko katika
jimbo hilo nchini Sudan.
Miili ya maaskari hao saba wa
Tanzania, inatarajiwa kuwasili
nchini Ijumaa, Julai 19 kwa ajili ya
maziko.