Mgombea Urais wa Democratic
Progressive Party (DPP) nchini Malawi, Peter
Mutharika, amesema hakuna sababu za kufanya
majadiliano kuhusu Ziwa Malawi ambalo
Tanzania wanaliita Ziwa Nyasa.
Mutharika, ambaye ni mwanasheria, aliyasema
hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
juzi Mkoa wa Kati.
Akikaririwa na gazeti la Nyasa Times,
Mutharika alisema Tanzania haina cha
kuambulia kwa Ziwa Malawi.
Kiongozi huyo ambaye hakuwapo katika
mkutano wa Rais Joyce Banda na wapinzani
kuzungumzia mustakabali wa ziwa,
aliwahakikishia Wamalawi kuwa wasiwe na
wasiwasi wa mvutano huo.
Mutharika ziwa lote ni mali ya Malawi na
akisisitiza kuwa, Tanzania haina hata punje ya
eneo.
“Hakuhitajiki majadiliano, Ziwa Malawi ni mali
ya Malawi, litakuwa la Malawi,” alisema
Mutharika ambaye alichukua masomo ya Sheria
Tanzania.
“Tanzania inatumia nafasi ya udhaifu wa
uongozi wetu, lakini ukweli, hawana hata tone la
eneo... Tutakapoitwa kwenye uchaguzi ujao
mwakani, tutamaliza haya yote. Nitaleta meli
nyingi kwa ajili ya maendeleo ya uchumi,
kutengeneza ajira za kutosha kwa vijana,”
alisema Mutharika huku akishangiliwa na
wafuasi wake.
Tanzania inataka kugawana ziwa, lakini Malawi
imegomea mpango huo na suala hilo liko katika
majadiliano ambayo Banda alisema kama
mwafaka haukupatikana ifikapo Septemba 30,
Malawi itapeleka suala hilo Mahakama ya Kimataifa (ICJ).