Takriban waumini 44 wameuawa kwa
kupigwa risasi wakiwa msikitini
Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, kwa
mujibu wa maafisa wa jimbo la
Borno.
Mauaji hayo yalifanyika wakati wa
maombi ya asubuhi Jumapili , ingawa
taarifa zimejitokeza Jumatatu ,
kutokana na hitilafu ya mawasiliano
kwani jimbo hilo liko chini ya sheria ya
hali ya hatari.
Shambulizi lilifanyika katika mji wa
Konduga, ulio umbali wa kilomita 35
kutoka mji mkuu wa jimbo hilo ,
Maiduguri.
Washambulizi wanasemekana kuwa
wanachama wa kundi la wapiganaji la
Boko Haram, ambalo liliwaua maelfu
ya watu tangu mwaka 2009.
Gazeti la Daily Post, liliripoti kuwa
watu wengine 26 walikuwa
wanatibiwa kwa majeraha waliyopata
wakati wa shambulizi hilo hospitalini
Maiduguri.
Mwanachama wa kikundi cha vijana
kinachotoa ulinzi kwa raia, aliambia
shirika la habari la Associated Press,
kuwa wapiganaji wao wannne
waliuawa walipojaribu kutoa kilio cha
kutaka usaidizi.
Raia wengine kumi na wawili,
waliuawa katika kijiji cha Ngom
kinachopakana na Maiduguri.
Rais Goodluck Jonathan alitangaza
sheria ya hali ya hatari katika majimbo
matatu Kaskazini Mashariki mwa nchi
mnamo mwezi Mei wakati wanajeshi
walipofanya operesheni dhidi ya
wapiganaji wa kiisilamu.
Boko Haram linapigania eneo la
Kaskazini mwa nchi likitaka kujitawala
kwa kutumia sheria za kiisilamu.
Mwandishi wa BBC mjini Lagos,
anasema kuwa wakati kundi hilo
limekuwa likishambulia makanisa, pia
limekuwa likishambulia misikiti.
Habari za mashambulizi hayo
zilijitokeza wakati kanda ya video ya
kiongozi wa kundi hilo Abubakar
Shekau, ilipotolewa akidai kundi hilo
kuhusika na mashambulizi hayo
ikiwemo kushambulizi dhidi ya vituo
vya polisi na kambi za jeshi.