POLISI FEKI WENGINE 7 WAKAMATWA.

SIKU chache baada ya
kukamatwa kwa askari
feki wa usalama
barabarani, Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es
Salaam, imewakamata
watuhumiwa saba wa
ujambazi, wakiwa na
sare za Polisi, huku
mwingine akijifanya
ofisa Usalama wa Taifa.

Akizungumza na
waandishi wa habari
ofisini kwake jana,
Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar
es Salaa, Suleiman Kova
alisema watuhumiwa
hao walikamatwa
wakiwa na sare za Polisi
jozi mbili.

Watuhumiwa hao ni
Khamis Mkalikwa (40),
Magila Werema (31),
Nurdin Bakari (46),
Materu Marko (32), Louis
Magoda (34), Amos Enock
(23) na Amiri
Mohammed (45), wote
wakazi wa jijini Dar es
Salaam.

Sare hizo, kwa mujibu
wa Kamanda Kova, ni
zenye cheo cha Sajenti
wa Kituo, huku jozi moja
ikiwa na jina
linalosomeka SSGT A.M
Mduvike.

Watuhumiwa hao
walikamatwa jana katika
eneo la Kiluvya, baada
ya askari kuweka mtego,
ambao ulifanikiwa
kuwanasa.

Alisema watu hao
walikuwa wakitumia
silaha, sare za jeshi la
Polisi na redio ya
mawasiliano katika
uhalifu wao na hivyo
kuwafanya baadhi ya
watu kutupia lawama
Jeshi la Polisi kwa
kujihusisha na uhalifu.
Alisema watuhumiwa
hao, wanahusishwa na
uhalifu katika maeneo ya
Boko, Tegeta, Mbweni,
Bahari Beach, na maeneo
mengine ya jiji. Alisema
watu hao ni hatari zaidi.
Watuhumiwa hao
walikuwa wakitumia gari
aina ya Cresta GX, 100
yenye namba T 546 BWR
na baada ya kuona
wamezingirwa na askari
maeneo hayo, walifyatua
risasi moja hewani,
lakini askari
walipambana nao na
kufanikiwa kuwakamata.
“Mbali na vitu hivyo pia
wamekamatwa na
bastola moja aina ya
Brown yenye namba
B.3901, ambayo ilikuwa
na risasi nne na ganda
moja, tunawashikilia
kwa upelelezi na baada
ya kukamilika
watafikishwa
mahakamani,” alisema
Kova.

Katika hatua nyingine,
Kamanda Kova alisema
wanamshikilia
mtuhumiwa Alquine
Masubo (42) maarufu
kama Claud, kwa kosa la
kujifanya ofisa wa
Usalama wa Taifa.
Claud ambaye ni mkazi
wa Yombo Buza,
alikamatwa akiwa na
vielelezo mbalimbali
pamoja na nyaraka za
idara hiyo, ambapo
baada ya kuhojiwa
alikiri kuwa yeye si
mfanyakazi wa idara
hiyo.

Kova alisema
mtuhumiwa huyo
alipopekuliwa zaidi,
alikutwa na bastola aina
ya Browing yenye namba
A. 956188-CZ83 ikiwa na
risasi 12 ndani ya kasha
lake.
“Alipopekuliwa
nyumbani kwake
alikutwa na bastola
nyingine aina ya
Maknov yenye namba
BA4799 ikiwa na risasi 19
na kitabu cha mmiliki
chenye namba CAR
00071678, ikiwa na jina
la P.1827 LT COL
Mohammed Ambari,
jambo ambalo
haliwezekani kwa mtu
mmoja kumiliki silaha
mbili,” alisema Kova.
Mtuhumiwa huyo pia
alikutwa na kitambulisho
cha Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) chenye
namba 7001- E. 1075 na
kompyuta mpakato aina
ya Toshiba.

“Huyu ni tapeli wa siku
nyingi na taarifa zake
tulikuwa nazo, anatumia
kivuli cha idara ya
usalama wa taifa
kufanya utapeli, lakini
sasa ndiyo mwisho wake
na wananchi wamjue”
alisema.

-Habari leo