Kutokana na mabadiliko hayo, mfumo wa tathmini endelevu (CA),unaopima maendeleo ya mwanafunzi akiwa shuleni, ndio utatumika kumpa mwanafunzi asilimia 40 zilizobaki na atapaswa kujua alichopata katika alama hizo kabla ya kuingia kwenye mtihani wa mwisho.
Akitangaza mabadiliko hayo jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema mabadiliko hayo yataanza na wanafunzi wanaoanza mtihani wa kidato cha nne Jumatatu.
Profesa Mchome alisema katika mabadiliko hayo, Wizara imeweka utaratibu wa jinsi mwanafunzi atakavyopata asilimia 40 ya mtihani wa mwisho, kutokana na kazi atakazokuwa amefanya tangu alipojiunga sekondari.
Kwa kidato cha nne, asilimia 15 kati ya 40, mwanafunzi atatakiwa azipate katika mtihani wa Taifa wa kidato cha pili; huku katika matokeo ya mtihani wa kidato cha tatu, kwa mihula yote miwili, atatakiwa awe na asilimia 10, kila muhula akipata alama tano.
Mtihani wa Majaribio (mock) kwa kidato cha nne, mwanafunzi atatakiwa apate asilimia 10 na kazi za mradi alama tano. Kwa mujibu wa Profesa Mchome, matokeo ya kidato cha sita kwa sasa yanafuata mfumo huo na utaendelea kama muundo wa sasa ulivyo.
Mfumo huo utatumika hadi kwa wanafunzi wa kujitegemea ambao alama zao zitatokana na matokeo ya mitihani ya awali.
Madaraja mapyaProfesa Mchome alisema kuanzia sasa kwa vidato vya nne na sita, alama za ufaulu katika masomo zitaanzia A, B+,B, C, D, E na F, ambapo mwachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana kwa kidato cha nne na cha sita.
Mfumo huo ni tofauti na zamani, ambapo alama za masomo ya kidato cha nne ilikuwa A, B, C, D naF, wakati kidato cha sita ilikuwa A, B, C, D, E, S na F.
"Katika alama hii ya B, kundi la kwanza la B litakuwa la wanafunzi waliopata alama kuanzia 50 hadi 59 na lingine la B+ litakuwa la waliovuka wigo wa B na kufikia wa 60 hadi 74," alisisitiza Mchome.
Alisema pamoja na kuwa na mwachano wa alama 26, alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia 75 hadi 100, ambapo waliofaulu kwa kiwango hicho walikuwa wachache na hivyo Serikali imeonahakuna haja ya kubadili alama hiyo, badala yake juhudi ziendelee kuongeza kiwango cha ufaulu, ili kupata wanafunzi wengi zaidi katika daraja hilo.
Alama C yenye maana ya ufaulu mzuri itaanzia 40 hadi 49, D ambayo ni ufaulu hafifu itaanzia 30hadi 39, E ufaulu hafifu sana itaanzia 20 hadi 29 na F ufaulu usioridhisha, itaanzia 0 hadi 19.
Muundo wa madarajaDaraja la kwanza kwa mujibu wa mfumo huo mpya, daraja la kwanza ambalo ni la kundi la wanafunzi walio na ufaulu, uliojipambanua na bora sana. Daraja la pili litakuwa kundi la ufaulu mzuri sana na daraja la tatu,kundi la ufaulu mzuri na wa wastani.
Daraja la nne litakuwa kundi la ufaulu hafifu na daraja tano litakuwa la ufaulu usioridhisha. Mtihani kidato cha 4 Wakati huo huo, jumla ya watahiniwa 427,906 ambao kati yao 367,399 ni watahiniwa wa shule na 60,507 wa kujitegemea wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne kuanzia Novemba 4 hadi 21.
Mchome alisema idadi hiyo ya watahiniwa ni pungufu ya watahiniwa 53,508, sawa na asilimia 11.1 ikilinganishwa na 481,414 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka jana.