NAIBU MKUU WA USALAMA LIBYA AACHIWA BAADA YA KUTEKWA

Naibu mkuu wa usalama wa taifa nchini Libya, Mustafa Noah, ameachiliwa huru siku moja baada ya kutekwa na watu wasiojulikana wakiwa na silaha karibu na uwanja wa ndege wa Tripoli.

Wakati akitekwa hakuwa na walinzi wake.

Libya imekuwa katika hali ya wasiwasi tangu watu arobaini wauawe na mamia wengine kujeruhiwa katika mapigano makali Ijumaa iliyopita.

Mapigano hayo yaliwahusisha wanamgambo na waandamanaji, ambao walikuwa wakijaribu kuwafukuza wanamgambo kutoka mji mkuu Tripoli.

Serikali imekuwa ikijitahidi kuwafukuza wanamgambo hao.

Mgomo wa kutaka wanamgambo waondolewe kutoka Tripoli, umedumu kwasiku tatu.

Waziri Mkuu, Ali Zeidan, alitekwa nyara kwamuda mfupi mwezi uliopita.