KILI STARS YAANZA CHALENJI KWA DROO

TANZANIA Bara 'Kilimanjaro Stars' jana ilianza kwa sare baada ya kufungana bao 1-1 na Zambia katika mchezo wa kwanza wa michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

Kilimanjaro Stars katika kipindi cha kwanza ilionekana kuutawala zaidi mchezo huo huku ikifanikiwa kuingia hadi katika eneo la hatari la Zambia, lakini walishindwa kutumia vema fursa hizo.

Zambia ndio ilikuwa ya kwanza kuziona nyavu za Bara kwa bao la Ronald Kampambe katika dakika ya41.

Bao hilo la kichwa lilitokana na pasisafi kutoka kwa kiungo Felix Katongo. Dakika tatu baadaye Zambia, mabingwa wa Afrika mwaka 2012 na timu mwalikwa katika michuano hiyo, ilifanya shambulio la kushtukiza golini mwa Bara, lakini kipa Ivo Mapunda aliondoa hatari hiyo.

Baada ya mapumziko, dakika ya 51, Kilimanjaro Stars ilisawazisha bao hilo lililofungwa na beki Said Morad kwa kichwa, kutokana na krosi ya Salum Abubakar na kumkuta Morad aliyechupa na kupiga kichwa.

Iwapo Bara ingetumia vema nafasi ilizozipata, ingeweza kutoka na mabao mengi katika mchezo huo wa kwanza kwa timu zote katika Kundi B.

Mshambuliaji Mrisho Ngasa alikosabao la wazi akiwa amebakia peke yake na kipa wa Zambia, naye Haruna Chanongo iwapo angetumia vema nafasi aliyoipata ya kuwatoka mabeki wa Zambia na kubaki na kipa, basi Kilimanjaro Stars ingeweza kutoka na mabao zaidi ya mawili.Kipa Ivo alionekana kuibeba zaidi Kilimanjaro Stars baada ya kuokoa mipira ya hatari mingi. Hata hivyo,Kocha wa Kilimanjaro Stars, Kim Paulsen alikiri kuwa kipindi cha mwanzo wachezaji wake walishindwa kucheza vema, na pia kulalamikia umakini wa kutofunga akimtolea mfano Ngasa.

Kim alisema katika kipindi cha kwanza, kila timu iilionekana kucheza kwa umakini huku timu yake ikiwa imetengeneza mazingira mazuri zaidi ya kushinda.

"Naona kuwa wachezaji wangu walishindwa kumalizia tu ila kipindicha kwanza wamecheza vema na pia wameonesha kuusoma mchezona kucheza vizuri zaidi kipindi cha pili," alisema Kim.

Naye kiungo Salum Abubakar anayechezea Azam FC, aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo, alisema ulikuwa mchezo wenye changamoto kubwa hasa uwanja kuwa na tope kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jana kwenye Uwanja wa Machakos.

Alisema kuwa wachezaji wenzake walijitahidi kuonesha mchezo safi na kutoka na sare hiyo.

Awali, Burundi iliishinda Somalia kwa mabao 2-0, hivyo kuongoza katika Kundi hilo la B ikiwa na pointi tatu, wakati Bara na Zambia zimegawana pointi moja. Bara itashuka tena dimbani keshokutwa kuivaa Somalia wakati Burundi itaikabili Zambia.