ATUPWA NJE YA TIMU KWA KUONESHA ISHARA YA KUMUUNGA MKONO MOSRI

Mchezaji soka mmoja katika moja ya vilabumaarufu nchini Misri ametupwa nje ya mechi za klabu hiyo baada ya kuonekana kumuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi.

Klabu ya Al Ahly, imesema kuwa Ahmed Abdul Zaher, hatashiriki mchuano wa FIFA wa klabu bingwa duniani baada ya kupiga saluti ya vidole vinne mnamo siku ya Jumapili.

Mchezaji huyo alikuwa anasherehekea bao lake la mchuano wa mabingwa wa Afrika ambapo Al Ahly ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Orlando Pirates wa Afrika Kusini.

Ishara hio imekuwa ikitumika kama ishara ya kumuunga mkono bwana Morsi.

Ishara hiyo pia ilitokana na maandamano ya wafuasi wa Morsi waliotawanywa na maafisa wa usalama mnamo mwezi Agosti baada ya kukesha katika eneo walilosema alikuwa amezuiliwa Morsi.

Rais Morsi alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia, na sasa anakabiliwa na kesi ya kuchochea mauaji ya waandamanaji wakati wa ghasia zilizotokea mjini Cairo mwaka jana.

Yeye mwenyewe aling'olewa kutoka uongozini mwezi Julai.

Abdul Zaher alisherehekea kwa ishara ya vidole vinne baada ya kuingiza bao la Al Ahly la pili ambapo waliibuka washindi dhidi ya Orlando Pirates.

"ndio nilitoa ishara hiyo ya Rabaa," alinukuliwa akisema kwenye mtandao wa FilGoal.

"lakini sikunuia kuzua hisia za kisiasa kwa mtu yeyote, nilichonuia ni kumkumbuka mtu yeyote aliyefariki, awe raia wa kawaidaau hata polisi.

''Mnamo siku ya Jumatatu maafisa wa klabu ya Al Ahly, walisema kuwa Ahmed Abdul Zaher hatashirikishwa kwenye mechi itakayochezwa nchini Morocco.