VIONGOZI WA SADC WAFIKIA MAKUBALIANO

Viongozi wa mataifa ya kusini mwa afrika SADC na wenzao wa mataifa ya maziwa makuu wamekubaliana kuhusu maswala kumi na moja ambayo yalikuwa yakijadiliwa katika mkutano wa Kampala kati ya waasi wa M23 na serikali ya DRC.

Maamuzi hayo yaliyotokana na mkutano wa viongozi hao mjini Pretoria Afrika Kusini, yamesema kuwa wale wote walioshiriki katika mzozo huo wataingia katika makubaliano kwa masharti kwamba waasi wa M23 wasitishe mashambulizi.

Na baada ya kutanga kumaliza uasi wao, ina maana kwamba M23 wameafikia moja ya masharti ya kutangaza rasmi kwamba watafuata njia za kisiasa kuafikia malengo yao.

Kundi la M23 limekuwa likishambuliwa na vikosi vya umoja wa mataifa ambavyo vimewafurusha wapiganaji hao kutoka ngome yao ya mwisho mashariki mwa Congo.Hata hivyo Rais wa Rwanda Paul Kagame hakuhudhuria kikao hicho.

Kagame ni jirani mkuu wa DRC Congo na amekuwa akituhumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ingawa daima amekuwa akikana madai hayo.