JK ASEMA TANZANIA HAITOKI, NA HAITOTOKA EAC

RAIS Jakaya Kikwete amesema Tanzania imo, itaendelea kuwemo na haina mpango wa kujiondoa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, licha ya vitimbi vinavyofanywa na viongozi wa nchi za Kenya, Uganda na Rwanda. Katika hotuba yake kwa Bunge jana, Rais Kikwete alisema wazi kuwa nchi hizo zimekiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika mambo manne kati ya mambo manane ambayo wameyajadili katika vikao vyao vya utatu.

"Tanzania hatuna mpango wa kutoka katika jumuiya ya Afrika Mashariki, tumo na tutaendelea kuwemo," alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa hatuwezi kujiondoakwani Tanzania haijafanya jambo lolote baya dhidi ya jumuiya hiyo au dhidi ya nchi yoyote mwanachama.


Badala yake Rais Kikwete alisema Tanzania imekuwa mwanachama mwaminifu, mvumilivu na mtiifu kwa jumuiya hiyo ndio maana vitendo vinavyofanywa na viongozi wa nchi tatu wanachama, Uhuru Kenyata (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame (Rwanda),vinazua maswali mengi ambayo hayana majibu.

"Tunajiuliza maswali mengi hadi tunakosa majibu, wanachukia nchi yetu, wanataka kuunda jumuiya yao au wananichukia mimi mwenyewe?"Alihoji Rais Kikwete hasa akielezea mshangao wake kwa viongozi hao kukaa katika vikao vitatu bila kushirikisha viongozi wa Tanzania na Burundi.

Alisema madai ya viongozi hao kwamba huo ushirikiano wa utatu huo ni wa nchi ambazo ziko tayari kuharakisha maendeleo ya Jumuiya hiyo, ni uwongo kwani haiwezekani hawaaliki baadhi ya viongozi wa ndani ya Jumuiya halafu wadai nchi ambazo hazikualikwa hawana utayari.

Rais Kikwete pia alitumia hotuba hiyo kukanusha madai kwamba Tanzania imekuwa kikwazo kuchelewesha maendeleo ya jumuiya hiyo, na akasema maadai hayo hayana ukweli wowote kwani Tanzania inachopigania ni kwa nchi wanachama kuheshimu mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo.

Alisema Tanzania haiwezi kuhangaika kwa kutumia muda na fedha zake katika kuijenga jumuiyahiyo, halafu iwe nchi ya kwanza kuidhoofisha "Haiwezekani tutumie dola za marekani milioni 12 kila mwaka kuchangia jumuiya hii halafu tuidhoofishe."

Kikwete hakumng'unya maneno, aliposema kinachoonekana kuwakera viongozi wa nchi zingine ndani ya Jumuiya hiyo, ni msimamo wa Tanzania katika kupinga kuharakisha kuundwa kwa shirikisho, hasa katika eneo la umiliki wa ardhi, uhamiaji na ajira.


Rais Kikwete alisema anapata taabu kuamini kutofautiaa katika misimamo ya nchi, ndio kuwe chanzo cha nchi hizo tatu kukataa kushirikiana na Tanzania, hata katika mambo ambayo haina mvutano nayo.

Alisisitiza kuwa msimamo wa Tanzania ni kuona jumuiya hiyo inajengwa hatua kwa hatua kama ilivyoanishwa kwenye mkataba na sio kuruka baadhi ya hatua. "Hatuna tatizo na kuundwa kwa shirikisho, tatizo letu ni kuruka hatua zilizoanishwa.

"Hatua hizo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na baadaye ndipo kuundwa kwa Shirikisho la Kisiasa ambako, kutafikiwa baada ya kura ya maoni itakayopigwa na wananchi wa nchi wanachama.


Rais alisema Tanzania haikuunga mkono kuharakisha shirikisho kabla ya hatua zingine kutekelezwa, kwa vile inaamini shirikisho hilo la kisiasa ni lazima lijengwe katika msingi imara wa kiuchumi na ndio maana wanaona kuna ulazima wa kuimarisha hizo hatua zingine.

"Kwa msimamo wetu shirikisho ni hatua ya mwisho, huo ndio msimamo wa Watanzania," alisema Rais Kikwete.

Alionya kuwa suala hio likiharakishwa kuna hatari ya jumuiya hiyo kuvunjika kwani mambo yanayozua mvutano siku zote ni ya uchumi na wala sio ya kisiasa.

"Kwa kweli kama hawata badilika sijui mambo yatakuwaje huko mbele? alionya Rais Kikwete na kusisitiza kuwa jumuiya hiyo itakuwa ya makundi kati ya Tanzania na Burundi na kundi lingine litakalohusisha nchi hizo tatu.

Aliongeza kuwa Tanzania haitaki yaliyotokea 1977 yatokee tena na akasisitiza kuwa itaendelea kushiriki katika Jumuiya hiyo na kutekeleza itifaki zote zilizoanishwa kwenye Mkataba.

Alisema Tanzania itahakikisha haidhoofishi Jumuiya wala kuwa chanzo cha kufa kwake.


"Hata kamaikidhoofika au kufa hatutaki Tanzania inyoshewe kidole kuwa ndio chanzo cha kufa kwake. Ndio maana hatutachoka kuzungumza nao, nimeshazungumza na baadhi yao na nitaendelea kuzungumza nao."

Utatu ulivyoanza Nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zimeshafanya vikao vitatu huko Mombasa, Kampala na juzi kimefanyika mjini Kigali Rwanda. Katika vikao hivyo viongozi wa nchiwaliamua mambo manane ya msingi kwa kile walichoita ni kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa EAC.

Mambo hayo ni kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura, ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini, kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda, kuanzisha Himaya Moja yaUshuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote.

Mengine ni kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki ambapo wameunda kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho, kuharakisha uanzishwaji wa hati ya pamoja ya kuishi ndai ya nchi hizo tatu (visa) ya pamoja ya utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kuwa hati yakusafiria katika nchi zao; na kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.


Rais Kikwete alisema orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya.

Alisema mambo manne kati ya hayo manane, hayamo kwenye mashartiya kutokufanyika bila ya kuihusishaau kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mambo hayo ni uzalishaji na usambazaji wa umeme, ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda na ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura ambalo pia alisema Tanzania haina tatizo nalo kwa vile sio mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais alisema katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hana maneno nayo.

Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati yakusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani waliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze.

Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha na kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki, Rais Kikwete alisema nchi hizo zimekiuka uamuzi wa pamoja. Hata hivyo RaisKikwete alikiri kushangazwa na kuuliza: "Kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi.

Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na wao baadae Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla."


-Habari leo