Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 8:30 usiku.
Alisema watu wasiofahamika walifika kanisani hapo na kidumu cha mafuta ya petroli pamoja na mpira uliotumika kuingizia mafuta ndani ya kanisa hilo ambapo katika tukio hilo viti 20 vya plastiki vimeteketea kwa moto.
Kamanda Minangi alisema mpaka sasa wamekamata watu wanaowatilia shaka kuhusika na tukio hilo.
Mchungaji wa kanisa hilo, Fidelisi Kalinga, alisema hawana uhasama na majirani zao na wanashirikiana vizuri, ila alikiri kuwapo kwa uhasama wa kiimani na kupokea vitisho vinavyoashiria uvunjifu wa amani.