Liverpool walibanwa na Everton katika pambano la watani wa jadi kaskazini mwa England, ambapo walipata bao la kusawazisha dakika za mwishoni na kunusuru pointi moja.
Katika mechi mbili za Jumapili hii, Manchester City walionesha umahiri wa ajabu kwa kuwafyatua wakali wenza wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur kwa mabao 6-0 wakati Manchester United wakibanwa kwa sare nchini Wales mbele ya Cardif.
Olivier Giroud alifunga mabao mawili ya Arsenal dhidi ya Southampton Jumamosi hii na kuwahakikishia Washika Bunduki waLondon ushindi muhimu dhidi ya timu inayokuja juu sana kwa uimara, chini ya kocha Mwargentina, Mauricio Pochettino.
Arsenal waling'ara huku mchezaji wake muhimu wa siku nyingi, Theo Walcott akirejea uwanjani baada ya kuwa nje kwa majeraha kwa miezi miwili, ambapo aliingia kipindi cha pili.Kwa matokeo hayo, Arsenal hawajafungwa nyumbani katika mechi za EPL tangu walipopoteza katika mechi ya kwanza kabisa dhidiya Aston Villa.
Kocha Arsenal Wenger alifurahi kupata ushindi muhimu na mgumu, baada ya kuwa wamepoteza mechi iliyopita dhdi ya Man United katika dimba la Old Trafford na Jumanne hii wanajiandaa kuwakaribisha Marseille ya Ufaransa katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
LIVERPOOL WABAKI NAFASI YA PILI
Liverpool wanaowafukuzia Arsenal walishindwa kwenda na kasi inayotakiwa, kwani walitoka sare ya 3-3 na wenzao wa Mercyside, Everton ambapo wenyeji walishadhani wangeibuka washindi kwa mabao ya akina Kevin Mirallas na Romelu Lukaku aliye kwa mkopokutoka Chelsea ambaye alifunga mabao mawili.
Liverpool walipata mabao yao kupitia kwa Coutinho, Luis Suárez na Daniel Sturridge aliyewanusuru na kichapo katika dakika ya 89 ya mechi hiyo ya kusisimua kwenye dimba la Goodison Park.
Kwa matokeo hayo, Liverpool wanashika nafasi ya pili kwa pointi 24, zikiwa ni nne nyuma ya Arsenal wakiwa wamelingana kimichezo.
Suarez alirejea Liverpool kwa ndege binafsi ya mmiliki wa Liverpool, John Henry baada ya kushiriki mechi ya kuwapeleka Uruguay kwenye fainali za Kombe la Dunia Brazil 2014 Alhamisi. Everton wanashika nafasi ya saba kwa sare hiyo, jambo ambalo bado ni faraja kwa kocha Roberto Martinez.
CHELSEA NA MOURINHO KWA RAHA ZAO
Chelsea waliokuwa wageni wa West Ham Jumamosi hii walifanikiwa kupata pointi tatu na mabao matatumuhimu katika mechi ambayo WestHam hawakupata bao lolote.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Frank Lampard aliyepachika mawili,moja kwa penati na jingine lilifungwa na Mbrazili Oscar.
West Ham ni klabu ya zamani ya Lampard aliyoanza kuchezea katika ligi kuu lakini hakuwa na huruma kuwakabili kwa nguvu. Kocha Jose Mourinho alionekana mwenye furaha na katika sura mpya, wakati mwenzake Sam Allardyce aliishia kusikitikia matokeo.
Kwa ushindi huo Chelsea wanashika nafasi ya tatu kwa pointi 24 sawa naLiverpool.
KARAMU MAN CITY DHIDI YA SPURSKocha wa Tottenham Hotspurs, Andre Villas-Boas aliondoka katika dimba la Etihad akiwa hana raha, akisema kila kitu kilikuwa kibaya kwao, baada ya vijana wake kupoteza kwa mabao 6-0 dhidi ya Manchester City.
Jamaa hao wa Eastlands walikuwa katika morali kubwa tangu mwanzo, ambapo Jesus Navas ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa saba katika EPL kufunga bao mapema zaidi, ikiwa ni sekunde ya 14 tu ya mchezo.
Mhispania huyo alifunga bao kutokana na kosa la kipa Hugo Lloris aliyepatiwa mpira na kuupiga mguuni mwa Sergio Aguero, lakini mbali kidogo na goli naye akasogea na kujaribu kufunga, Lloris akautema na kuusukuma mpira uliomfikia Navas aliyefunga bao zuri na katika kona ya ajabu.
Mabao mengine yalipachikwa na Sandro wa Spurs aliyejifunga, Aguero mawili, Alvaro Negredo na Navas kupigilia msumari wa mwisho dakika ya 90. Kocha ManuelPellegrini alisema vijana wake hawangeweza kucheza vizuri zaidi ya hapo.
Hii ni mara ya kwanza tangu 1992 kwa Spurs kufungwa vibaya jinsi hiyo, na inashangaza kwa sababu walikuwa wakiutawala mchezo zaidi ya wenyeji wao na hata walijaribu kufanya mabadiliko ya wachezaji bila mafanikio yoyote.
Kwa kichapo hicho, Man City wanashika nafasi ya nne kwa pointi 22 wakati wakiwaacha Spurs wakiugulia katika nafasi ya tisa, jambo ambalo si kawaida katika miaka ya karibuni.
MAN UNITED WABANWA NA CARDIF
Manchester United walijaribu kila hali kujihakikishia ushindi mwingine muhimu kwenye ligi lakini walihangaishwa na baadaye kutulizwa na Cardiff kwenye mechi ya Jumapili hii.
United walitangulia kufunga katika dakika ya 15 kupitia kwa Wayne Rooney ambaye nusura apewe kadi nyekundu kwa rafu mbaya na ya makusudi katika dakika za kwanza dhidi ya Jordon Mutch Cardiff katikauwanja wa Cardiff City nchini Wales.
Hata hivyo bao hilo lilisawazishwa na Frazier Campbell dakika ya 33 kabla ya Patrice Evra kufunga kwa kichwa kona ya Rooney muda mfupo tu kabla ya mapumziko.
Wakati kocha wa Man U, David Moyes akidhani kwamba wangeondoka wakiwa washindi, mchezaji Kim Bo-Kyung aliyetokea benchi alifunga bao katika dakika zamwisho na kuwapa raha wenyeji na washabiki waliofurika uwanjani.
Matokeo hayo yanawafikisha Manchester United katika nafasi ya sita.
MATOKEO MENGINE YA EPLKwenye mechi nyingine wikiendi hii, Fulham waliendelea na hali mbaya baada ya kufungwa wakiwa nyumbani na Swansea kwa bao 2-1.
Hull walipotea mechi kwa bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace, Newcastle wakawaadhibu Norwich 2-1 wakati Stoke wakiwafunga Sunderland bao 2-0.
Matokeo ya mechi hizo yanawafanya Newcastle kushina nafasi ya nane kwa pointi zao 20 wakifuatiwa na Spurs wenye pointi sawa nao, Swansea ni wa 10 kwa pointi 15 wakati West Bromwich Albion wanaopepetana na Aston Villa Jumatatu hii wanashika nafasi ya 11 kwa kujikusayia pointi 14.
Nafasi ya 12 inashikwa na Villa wenye pointi 14 sawa na Hull huku wakifuatiwa na Stoke na Cardiff waliokikusanyia pointi 13 kila moja.
Norwich wana pointi 11 katika nafasi ya 16 wakati West Ham itabidi wajiulize kulikoni kwa sababu wapo nafasi ya 17 wakiwa napointi 10.
Hao wapo sawa na Fulham walio katika eneo la hatari la zile timu tatu mbovu kwa pointi hizo hizo 10 wakati Crystal Palace na Sunderlandwanafungana kwa pointi saba kwenye nafasi mbili za mwisho.